Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NYUMA YA PAZIA: Simulizi ya kutisha ya Jack "Wheelchair"

Wilshere Pic Simulizi ya kutisha ya Jack "Wheelchair"

Sun, 27 Feb 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Miongoni mwa binadamu waliozaliwa siku ya mwaka mpya yumo Jack Andrew Garry. Jina la mbele unaweza kuchagua moja kati ya haya mawili. Unaweza kumuita Wilshere au Wheelchair. Historia ya maisha yake ya soka inanitia huzuni kidogo.

Jack, mfupi kama alivyo alikuwa na kipaji maridhawa. Ukitumia jina la Wilshere utamkumbuka kwa kipaji chake maridhawa. Mguu wa kushoto, umiliki wa mpira uliotukuka, kasi ya kuelekea katika lango la adui, ubora wa kufikiria kwa haraka.

Hata katika pambano la Barcelona dhidi ya Arsenal, huku Xavi Hernandez na Andres Iniesta wakiwa katika ubora wao, Jack aling’ara katikati yao. Angeweza kuchukua mpira katikati yao na kuondoka zake kwa amani. Angeweza kuwapiga chenga na kuondoka zake kwa amani. Sio Emirates, hapana, ni Camp Nou.

Chini ya Arsene Wenger, Jack alikuwa katika mikono salama. Anaweza kuwa kipaji cha mwisho cha uhakika kuibuka katika timu ya watoto ya Arsenal kabla ya kuibuka kwa hawa kina Bukayo Saka na Emile Smith Rowe.

Kila mwaka mpya unapofika, Jack huwa anasheherekea siku ya kuzaliwa kwake. Alizaliwa Januari Mosi, 1992. Baada ya kukiona kipaji chake akiwa na Arsenal usingeweza kutazamia kwamba ‘birthday’ yake ya mwaka huu Jack angekuwa anakwenda kucheza katika timu ya AFG ya Denmark.

Ana miaka 30 tu. Ni miaka ambayo ongeza miaka saba mbele yake, Cristiano Ronaldo bado anafunga mabao Manchester United. Zlatan Ibrahimovich anacheza AC Milan. Pierre-Emerick Aubameyang anatamba na Barcelona akiwa na miaka 32.

Mastaa wengi wamevuka miaka 30 ya Jack na wanacheza timu kubwa barani Ulaya. Nini kimetokea kwa Jack? Ni stori ya kuhuzunisha tu kwamba Jack amepitia mengi. Alipaswa kwa sasa kuwa amekamata dimba la Arsenal au timu nyingine kubwa kama ilivyo kwa kina Luca Modric ambao ni wakubwa kwake.

Jack ameandamwa na majeraha, usela na upotevu wa fomu ulioshangaza. Akiwa bado ndani ya Arsenal tena katika umri mdogo Jack tayari alikuwa msela. Aina yake ya maisha yake ni kama maisha ya Wayne Rooney. Watoto wa ghetto.

Chini ya Arsene, Jack ameshawahi kukutwa akivuta sigara katika klabu za usiku mara kadhaa huku akiwa amezungukwa na warembo lukuki. Ameshawahi kupigana mara kadhaa nje ya klabu za usiku. Ni maisha ambayo haujawahi kusikia Ronaldo au Lionel Messi wakiishi.

Jack msela hasa. Ndani na nje ya uwanja. Hata aina yake ya mchezo, achilia mbali kipaji chake maridhawa lakini Jack ni msela. Akiudhika anacheza soka la nguvu na la ovyo ambalo linahatarisha afya yake mwenyewe. Ni msela hasa.

Lakini zaidi ni kwamba majeraha yamekatili kipaji cha Jack. Ametumia muda mwingi kukalia kiti cha wagonjwa hospitalini (wheelchair) pengine kuliko kucheza soka lenyewe. Haishangazi kwamba Waingereza wenyewe huwa wanamuita Jack Wheelchair badala ya Jack Wilshere.

Usingeweza kuamini kwamba katika umri wa miaka 26 tu Arsenal walimruhusu Jack kuondoka bure Arsenal. Kabla ya hapo ungetazamia miaka hiyo Arsenal wangekuwa wanapokea ofa ya Pauni 100 milioni kumruhusu Jack kwenda Real Madrid au Barcelona ama Manchester City.

Kuanzia hapo Jack alianza kutangatanga. Alianzia West Ham. Akaishia kuwa Wheelchair badala ya Wilshere. Alicheza mechi 16 tu ndani ya misimu miwili. Ingawa mkataba wake ulikuwa wa miaka mitatu lakini baada ya miaka miwili West Ham wakamfungulia mlango wa kutokea.

Akaenda zake Bournemouth Januari, mwaka jana, baada ya kukaa karibu msimu mzima bila ya kucheza soka. Mwishoni mwa msimu wakaachana naye. Kuanzia hapo mpaka wiki iliyopita Jack hakuwa na timu. Miezi minane hakuwa na timu.

Ni nyakati hizi Jack anadai kwamba mke wake, Andriani Michael alikuwa anamshukia kwa maswali magumu akimuuliza kulikuwa na umuhimu gani wa yeye kuendelea kufanya mazoezi peke yake huku timu zikiwa hazimtaki?

Mwanaye Archie mwenye umri wa miaka tisa naye alikuwa anamuuliza maswali magumu. Alikuwa akimuuliza “baba kwanini hauwezi kwenda kucheza Marekani, au La Liga? Kwanini hakuna timu ambayo inakutaka?”

Vaa viatu vya Wilshere unapoulizwa maswali haya na mwanao. Kwamba ‘Kwanini hakuna timu inayokutaka?’ Swali gumu.

Kuanzia hapo Jack alikuwa akifanya mazoezi na Arsenal. Mzunguko wake wa maisha ulimrudisha alikoanzia. Kuna wakati nilikuwa najipa matumaini kwamba labda Mikel Arteta angeona kitu kwake na kumchukua kama mchezaji huru ili awasaidie wakati kina Granit Xhaka wanapofanya ujinga uwanjani. Hata hivyo, inaonekana Arteta hakuona kilichomridhisha licha ya kwamba aliwahi kucheza naye enzi hizo.

Na sasa Jack ameamua kusaini mkataba wa miezi sita katika klabu ya AGF inayocheza Ligi Kuu ya Denmark. Sio tatizo. Mpanda ngazi hushuka. Lakini sio kushuka kwa namna ambayo Jack ameshuka. Kutoka kuwasumbua kina Xavi na sasa kucheza Ligi Kuu ya Denmark ilipaswa iwe kwa mchezaji mwenye miaka 35 sio 30.

Miaka 30 ni umri ambao mchezaji anapaswa kuwa katika ubora wake wa hali ya juu kabla ya kuanza kushuka. Ni huzuni.

Kwa watu wengine wanaweza kudhani Jack ni mkubwa sana kwa sababu wameanza kumsikia zamani. Hapana. Walipoanza kumsikia zamani alikuwa mtoto tu lakini wala si miaka mingi iliyopita.

Jack anaingia katika faili langu kama wachezaji wanaotamanisha kujua ingekuwa vipi kama wangebaki kuwa fiti wakacheza soka lao kwa asilimia 100. Jack alikuwa mchezaji wa Kiingereza lakini mwenye damu ya Brazil au Hispania.

Hakufanana na viungo wengi wa Kiingereza ambao ni hodari wa kucheza soka la msingi tu (basic football). Jack angeweza kuiweka dunia mfukoni kama angeamua kutokuwa msela, lakini pia angeepuka majeraha ya mara kwa mara.

Nyakati hizi alipaswa kuwa nahodha wa timu ya taifa ya England huku akicheza soka la juu katika timu kubwa. Mwenyewe anafahamu hilo. Labda amekwenda Denmark kwa ajili ya kujiweka fiti na kurudi katika Ligi Kuu ya England.

Vyovyote ilivyo hawezi kuwa Jack ambaye tulimfahamu wakati akianza chini ya Arsene Wenger.

Kuna mastaa wengi ambao tumewahi kuona ubora wao kwa asilimia mia. Kina Rooney, Ronaldo, Messi na wengineo. Hata hivyo, Jack anaingia katika faili la mastaa ambao tumebaki kujiuliza lile swali maarufu. Ingekuwa vipi kama angekuwa fiti muda wote?

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz