Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NYUMA YA PAZIA: Salah anavyoupima ukubwa wa Liverpool akiwa Yaounde

Salah Pic Mohammed Salah

Sun, 30 Jan 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Yupo katika kambi ya Misri pale Yaounde, na wakati mwingine lakini Mohamed Salah bado anawaachia Liverpool mtihani mzuri darasani. Yupo kilomita 4,561 kutoka Liverpool lakini Salah ameendelea kuwaachia Liverpool mtihani mkubwa wa maisha yao.

Wao ni wakubwa kama wanavyosema? Wana ukubwa wa mataji au ukubwa wa kiuchumi? Wanastahili kuishi maisha ya kisasa au maisha ya kizamani? Wana ubavu wa kuwa wakubwa ndani na nje ya uwanja kama rafiki zao Manchester United?

Salah anamaliza mkataba wake na Liverpool mwakani. Ndio, haujasoma vibaya, mwakani. 2023. Wakati huo atakuwa na umri wa miaka 30. Kwa sasa Salah anaweza kuwa mmoja kati ya wachezaji wawili bora duniani. Achana na Lionel Messi na Cristiano Ronaldo ambao jua linazama mbele ya macho yao. Liverpool mpaka sasa hawajafikia masharti ya mkataba mpya wa Salah. Mtihani unakuja katika ukweli kwamba kwa sasa Liverpool hawawezi kumpoteza Salah. Ni lazima wambakishe klabuni kwao kwa sababu hawa ni aina ya wachezaji ambao hauwezi kukubali kuwapoteza.

Kwa mfano, kama ukiamua kumuuza Salah kukwepa asiondoke bure mwakani, unaweza kumnunua mchezaji gani wa kuziba pengo lake? Klabu zinaweza kuuza wachezaji wake mahiri na kumnunua Salah kwa ajili ya kuziba pengo. Lakini Liverpool inaweza kumnunua nani kwa ajili ya kuziba pengo la Salah?

Kwa mfano, PSG wanaweza kumruhusu Kylian Mbappe aondoke na wakageuza jicho lao kwa Salah kwa ajili ya kuziba pengo lake. Je Liverpool inaweza kumruhusu Salah aondoke na kisha pengo lake kuzibwa na Mbappe? Haiwezekani.

Lakini sasa Liverpool wameingia katika mtego wa kulazimika kutanua misuli yao kumbakisha Salah. Wanahitaji asaini mkataba mpya lakini kama unaona mpaka sasa hajasaini basi ujue mambo ni magumu katika maongezi yao na kambi ya Salah.

Walimpa mkataba wa awali akiwa ni mchezaji mzuri wa kawaida. Lakini sasa wanalazimika kumpa mkataba huku akiwa na kile kiwango ambacho kinaitwa World Class. Hapa ndipo tatizo lilipo kwa Liverpool hasa ukizingatia kwamba hakuna akina Salah wengi huko nje ambao wanaweza kuziba pengo. Wanalazimika kumbakisha kwa aina ya mishahara ambayo tumeisikia akina Ronaldo na Messi wakipewa. Nyakati hizi wakala wa Salah ana kila sababu ya kutamba. Ana kila sababu ya kutaka mteja wake alipwe sawa na Neymar au Mbappe au Hazard. Siamini kama kuna shabiki wa Liverpool anayeweza kutaka Liverpool ibadilishane Salah na Neymar. Wote wangependa kubaki na Salah.

Kufikia hatua hii ndipo ambapo Liverpool inapaswa kwenda na ukubwa wake. Hawa kina Madrid, Barcelona, Manchester United, Manchester City na wengineo walikuwa na ubavu mkubwa wa kubakisha mastaa wao kwa mishahara mikubwa. Vipi kwa Liverpool? Ni hadithi ile ile ya kumfuga Chatu akawa mkubwa lakini mwishowe ukashindwa kumpa unga wa kutosha.

Kuna mambo ambayo Liverpool baada ya miaka 30 ya kukosa ubingwa wa England kisha wakauchukua misimu miwili iliyopita lazima waanze kwenda nayo. Kwanza kabisa lazima waendelee kuutanua uwanja wa Anfield. Haitoshi kwa utanuzi walioufanya mpaka sasa ambapo unachukua mashabiki 53,394. Inabidi waendelee. Lakini hapo hapo kuna huu mtihani wa kuwabakisha wachezaji wa aina ya Salah. Najua hata akina Trent Alexander-Arnold ndiko wanakoelekea. Lazima ubakishe wachezaji wa kariba hii kwa mishahara mikubwa ambayo wanaitaka. Vinginevyo ukubwa wako unakuwa feki tu.

Lakini hapo hapo Liverpool pia lazima ijiingize katika soko la kununua wachezaji wa kariba ya World Class. Sikumbuki mara ya mwisho Liverpool ilimnunua mchezaji gani ambaye ni World Class. Kitu ambacho inaweza zaidi ni kuwageuza wachezaji kuwa na hadhi hii lakini sio kununua wachezaji wa hadhi hii. Hawa akina Fernando Torres, Luis Suarez, Salah, Sadio Mane, Virgil van Dijik na wengineo wote wamegeuzwa kuwa world class baada ya kufika Liverpool. Huu ni wakati ambapo inabidi waanze kuwanunua wachezaji wakiwa na hadhi hizi tayari. Ndio maana halisi ya ukubwa.

Lakini pia wanapowafikisha wachezaji katika hadhi hii ni lazima wajue namna ya kuwalinda. Tunaweza kuwasamehe kuhusu Torres na Suarez ambao inawezekana waliondoka baada ya kukosa mataji lakini tofauti yao na Salah ni kwamba tayari amewapa taji la Ligi Kuu ya England na pia lile la Ulaya.

Manchester United ilikuwa na uwezo huu. Mchezaji pekee ambaye aliwatesa katika kumbukumbu yao ni Cristiano Ronaldo ambaye aliamua kwenda Real Madrid mwaka 2009. Na hata hivyo Ronaldo hakuondoka kwa sababu za kushindwa mshahara na United. Alikuwa na ndoto tu ya kwenda Madrid.

Ni kama ambavyo inakaribia kutokea kwa Mbappe. Sio kwamba PSG wameshindwa kumpatia mkataba mpya wa pesa nyingi, hapana, ni kwa vile tu mchezaji mwenyewe ana kiu ya kukipiga Real Madrid. Hii ni tofauti na Salah ambaye hatujasikia kwamba ana kiu ya kukipiga kwingine lakini anaonekana tu anataka mshahara mkubwa.

Liverpool wanaweza kutoa Pauni 400,000 kwa wiki kwa Salah? Ni swali gumu lakini ni ukweli ambao lazima wapambane nao. Vinginevyo katika hesabu za kawaida wanaweza kujikuta wakitumia pesa nyingi kupata mbadala wa Salah pengine kuliko pesa ambazo wangeweza kuzitumia kumpa Salah mshahara mkubwa. Natazamia kama wakimpa mkataba mpya anaweza kuwa miongoni mwa wachezaji watatu wenye mishahara mikubwa zaidi duniani. Kama uwanjani yupo katika orodha hiyo kwanini katika orodha ya mishahara akosekane?

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz