Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NYUMA YA PAZIA: Ronaldo ameegesha mtego wa panya kwa Wareno

Ronaldo UEFA Cristiano Ronaldo

Sun, 25 Sep 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Sir Alex Ferguson alimvumilia Paul Ince wakati akiwa mchezaji hadi pale aliposhindwa. Alikuwa mkubwa klabuni. Mkubwa katika kiasi ambacho aliwaambia wachezaji wenzake wamuite ‘The Governor’. Kina Ryan Giggs walikuwa wanapigwa makonzi na Ince.

Baadaye Sir Alex akaamua kumuuza Ince kwenda Inter Milan. Ombea hali hii itokee klabuni na isitokee katika timu ya taifa. Na hata kama ikitokea katika klabu basi ombea awepo kocha imara na chuma kama Sir Alex Ferguson.

Majuzi nilikuwa namsikia Cristiano Ronaldo mahala. Amedai kwamba atacheza katika Fainali za Kombe la Dunia Qatar 2022. Na amedai baada ya hapo anatazamia kuwepo katika michuano ya Euro 2024. Nilitabasamu. Usidhani ni kauli nyepesi.

Ni kauli ambayo inamuweka kocha katika wakati mgumu. Ronaldo ni mkubwa. Ni ‘mungu mtu’ pale Ureno na duniani kwa ujumla. Ni miongoni mwa wachezaji bora zaidi kuwahi kutokea katika historia ya soka. Yeye na hasimu wake, Lionel Messi wameishi katika dunia yao kwa miaka mingi.

Kocha wa soka anasimama mbele ya wachezaji wake, anapanga kikosi. Anahitaji kutazama darini wakati akitaja kikosi chake huku majina ya Ronaldo na Messi yakiwa hayapo ingawa wamevaa viatu vyao vya mechi kwa ajili ya pambano muhimu la soka.

Erik Ten Hag ameuma jongoo kwa meno pale Old Trafford na Ronaldo anasugua benchi. Hata hivyo maisha hayawi hivyo katika timu za taifa. Klabuni inaweza kuwa rahisi lakini katika timu za taifa wachezaji wanaheshimiwa zaidi.

Ronaldo wa leo hana kasi, hana mwendo. Hana makali. Anasubiri kuvizia. Wakati huohuo mpira wa kileo una mahitaji makubwa. Unahitaji watu wanaokaba kwa pamoja, wanaoshambulia kwa pamoja, wanaoziba nafasi za adui kwa pamoja. Ten Hag ameamua kinachotakiwa.

Swali ni kama Fernando Santos wa Ureno anaweza kuamua kinachotakiwa. Ana vijana wengi wanaotamba duniani kwa sasa. Wana kasi na wanaweza kumfanyia kazi yake kuliko Ronaldo. Santos anakabiliwa na mambo mawili.

Jambo la kwanza hatuna uhakika kama Ronaldo ana ulazima katika kikosi kitakachokwenda Qatar. Hata hivyo, orodha ya wachezaji 26 wanaotakiwa kwenda Qatar ni kubwa. Ni ngumu kumuacha Ronaldo katika orodha ya wachezaji hiyo, hasa vilevile ukizingatia kwamba yeye ni nahodha.

Lakini mtihani wa pili ni kumchagua Ronaldo kucheza mechi. Ana uthutubu wa kufanya kile ambacho Ten Hag anafanya Old Trafford? Ronaldo ni ‘mungu mtu’ Ureno, lakini anashikilia rekodi zote muhimu Ureno.

Ronaldo ameichezea Ureno mechi 189 na ndiye mchezaji aliyeichezea Ureno mechi nyingi zaidi katika taifa hilo. Lakini ameifungia Ureno mabao 117 na ndiye anaongoza kwa kufunga mabao mengi zaidi katika taifa hilo ambalo kumbuka limewahi kutuletea kina Luis Figo, Eusabio, Nuno Gomes, Pedro Pauleta na wengineo.

Unaweza kumuweka nje Ronaldo? Kuna makocha huwa wanashindwa. Sifahamu kama ingekuwa Jose Mourinho huwa ana ubavu huu kuanzia katika klabu hadi timu ya taifa. Sir Alex pia anaweza kufanya hivyo. Lakini sio kila kocha anaweza kufanya hivyo. Wengine hawawezi kutanua mbawa zao.

Wakati huohuo mbele kuna machaguo mengi. Kuna vijana ambao damu zinachemka kwa sasa. Wanaweza kukupa mambo mengi uwanjani zaidi ya Ronaldo. Bahati nzuri Wareno wana kizazi kizuri kwa sasa.

Sitaki kuzungumzia kuhusu maeneo ya nyuma hadi katikati lakini mbele Wareno wana Ruben Neves, Joao Felix, Rafael Leao, Diego Jota, Concalo Ramos, Bruno Fernandes, Bernardo Silva, Renato Sanches na sasa Fabio Vieira wa Arsenal ameingia katika chati. Ronaldo anaweza kukubali kucheza dakika 10 za mwisho?

Nilimtazama Ronaldo katika mechi mbili dhidi ya Southampton na Real Sociedad. Alipenyezewa mipira miwili ambayo Diogo Jota angeweza kufanya madhara zaidi, lakini ilionekana waziwazi kwamba miguu ilikuwa imemsaliti. Alishindwa hata kutuliza.

Kinachonichekesha zaidi ni kwamba Ronaldo amedai anataka kucheza katika fainali za Euro 2024. Kwa sasa ana miaka 37, lakini wakati huo fainali zitakapokuwa zinachezwa atakuwa na miaka 39. Kuna maswali mengi.

Ina maana baada ya Kombe la Dunia hataki kustaafu. Kuna uwezekano mkubwa kocha asiwe Santos lakini kocha yeyote ambaye atakuwepo wakati huo ana uwezo wa kuchukua uamuzi wa Ten Hag? Nadhani kwa wakati huo Ronaldo atakuwa hastahili hata kuitwa kikosini, lakini je, kocha wa wakati huo anaweza kuwa na ubavu wa kumtupa hata kama Ronaldo atajisikia kuwa fiti?

Binafsi naamini kwamba Ronaldo kwa sasa atakuwa anawaweka katika wakati mgumu makocha. Ten Hag tayari anaonekana ameshachukua uamuzi mgumu ambao bahati yake unaonekana kufanya kazi. Kwa mfano, baada ya kuamua kumtema Ronaldo bado United imeshinda mechi mbili za mwisho dhidi ya Arsenal na Southampton.

Kitu cha msingi ambacho Ronaldo anaweza kufanya kwa Ureno mbele ya safari ni kustaafu tu. Hii itawapunguzia makocha muda wa kufanya uamuzi mgumu. Kwa sasa makocha watamuonea aibu na hata mashabiki watamuonea aibu. Hakuna ambacho wanaweza kumfanya kwa sababu ni fahari yao.

Ronaldo ni alama kubwa zaidi ya Ureno kwa sasa duniani. Ni alama kubwa zaidi ya Mourinho na ni alama kubwa zaidi pengine kuliko klabu zao tatu kubwa Porto, Sporting Lisbon na Benfica.

Tatizo kubwa kwa Ronaldo ni mshindani. Anapenda mapambano. Anaupenda mchezo wenyewe. Hata hivyo licha ya kuupenda sana mchezo wenyewe na kisha kuendelea kujifua lakini bado wakati ni ukuta. Muda umemsaliti na ni bora tu angerusha taulo na kumalizia maisha yake ya soka katika klabu moja ya Saudi Arabia ambayo ingemlipa pensheni kubwa kuwahi kutokea katika soka.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz