Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NYUMA YA PAZIA: Pogba, Manchester United ni pipa na mfuniko wake

Paul Labile Pogba Paul Labile Pogba

Sun, 27 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Bill Gates na Aliko Dangote wanaweza kuwa marafiki. Wanastahili. Waingereza wana msemo wao kwamba ‘They deserve each other’. Lakini hata maskini na mimi wanastahili kuwa marafiki. Ndege wafananao wakati mwingine wanaruka pamoja.

Unataka kusikia mazungumzo tofauti kutoka wachezaji? Unataka kusikia mahojiano tofauti kutoka kwa wachezaji? Basi ni nyakati hizi wanapokuwa katika kambi za timu za taifa. Wanarudi makwao na kukutana na waandishi wa habari tofauti ambao wamezoea kukutana nao kila wikiendi.

Kule ndipo ambapo wachezaji wanafunguka hasa kuhusu maisha yanayoendelea katika klabu zao. Sijui wanadhani kwamba ghafla wanakuwa wamehamia katika dunia tofauti. Wakati mwingine akili zao zinakuwa ndogo.

Kwa mfano, majuzi akiwa katika kambi ya timu ya taifa ya Ufaransa, Clairefontaine, nimemsikia Paul Pogba akilalamika kwamba miaka mitano yote ambayo amekaa Manchester United katika ujio wa pili ni kama vile imepotea bure.

Katika Kiingereza sahihi alisema ‘they were wasted’. Yaani amepoteza muda bure tu. Katika tafsiri nyingine anaamini kwamba labda angekuwepo kwingine huenda angekuwa amepata mafanikio kwa kutwaa mataji makubwa.

Na labda katika tafsiri nyingine mbili nyingine ni kwamba huenda yeye angekuwa mchezaji mkubwa kuliko alivyo sasa. Na labda kwamba huenda angetwaa tuzo zake binafsi. Lawama hizi inaonekana anaitupia zaidi Manchester United kuliko anavyojitupia mwenyewe.

Ukweli ambao haufahamu ni kwamba yeye na Manchester United wanapswa kuwa marafiki. They deserve each other. Kila mmoja amemstahili mwenzake katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Hakuna anayeweza kumlaumu zaidi mwenzake. Wanastahili kuwa marafiki wa karibu.

Katika hali ya kawaida hakuna anayeweza kujitapa kwamba yeye ni zaidi ya mwenzake. Sana sana kidogo Man United wanaweza kumwambia Pogba kwamba wameijaza vyema akaunti yake ya benki kila wikiendi. Hata wakati alipokuwa akitumia muda mwingi saluni kuliko uwanjani.

Pogba hawezi kuilaumu Man United wakati hajawahi hata kufikia nusu ya kiwango cha Yaya Toure akiwa na Manchester City. Hajawahi walau kufunga mabao kumi ya ligi ndani ya msimu mmoja. Hajawahi kuwa na mwendelezo wa ubora (consistency) akiwa na Man United.

Kipaji kipo katika miguu yake na kichwa chake. Katika ubora wake kuna viungo wachache unaoweza kuwalinganisha na Pogba. Lakini mechi ya leo angeweza kuwa kiungo bora duniani, mechi ya wikiendi ijayo angeweza kuwa mmoja kati ya viungo bora duniani.

Pale Chelsea kuna Mfaransa mwenzake mweusi mwenye asili ya Afrika, Ng’olo Kante. Kila wikiendi Ng’olo ni yuleyule tu. Chelsea ishinde, itoke sare, ifungwe N’golo anaendelea kuwa yuleyule kama Pogba angeweza kuwa na mwendelezo wa N’golo tu basi nadhani angestahili kusema yote aliyoyasema akiwa Paris hapo juzi.

Moja kati ya sababu ambazo zimeifanya Man United kuwa kama ilivyo ni kuwa na wachezaji kama kina Paul Pogba nyakati hizi. Wachezaji wanaojali zaidi staili zao za nywele kuliko vipaji vyao na juhudi. Kitu cha kushangaza zaidi ni kwamba wachezaji wenyewe hawa ndio muhimu zaidi uwanjani upande wao.

Hatuwezi kumshangaa Pogba peke yake. Man United nayo inabidi tuishangae. Wameruhusu maringo haya ya Pogba. Kwa muda mrefu wameshindwa kutengeneza timu imara tangu Sir Alex Ferguson. Kuna mambo mawili wameyafanya na sitaki kuigusa menejimenti zao zaidi.

Hawajawahi kuwa na mradi wa makusudi wa kuirudisha Manchester United inakostahili. Mara kadhaa wamebadilisha makocha bila ya kujua mwelekeo wao. Afadhali wangeamua kumuamini David Moyes kwa muda mrefu huenda angewatengenezea kitu.

Wakahamia kwa Louis Van Gaal. Kisha wakaenda kwa Jose Mourinho. Halafu wakarudi kwa Ole Gunnar Solskjaer. Muda wote huo timu haikupata mwelekeo. Na hata walipoamua kumchukua kocha wa muda, Ralf Rangnick inaonekana uamuzi wao haukuwa sahihi. Achilia mbali hao makocha lakini Man United imefanya uamuzi mbovu pia katika kusajili wachezaji mbalimbali ambao ni wa kawaida tu mbele ya dunia ya timu kama Manchester City na Liverpool. Bahati mbaya zaidi kwao ni kwamba wametumia pesa nyingi kununua wachezaji wenyewe na inawalipa mishahara mikubwa.

Hapa ndipo anapojitokeza mchezaji kama Pogba na kudai kwamba Man United wamempotezea muda kwa sababu anajiona staa mkubwa kuliko mastaa waliopo Man United kwa sasa. Asingesema hivyo mbele ya kina Paul Scholes, Roy Keane, David Beckham, Dwight Yorke, Andy Cole na wengineo.

Si ajabu asingepata nafasi katika kikosi hiki. Man United ndio wamempa mdomo Pogba. Haishangazi ninaposema kwamba ‘they deserve each other’. Kila mmoja anamstahili mwenzie. Ni kesi tofauti na ile ambayo inaendelea pale Anfield kati ya Mohamed Salah na Liverpool.

Kule ni kweli kwamba kila mmoja anamstahili mwenzie katika ubora wao. Salah amegoma kusaini mkataba mpya mpaka sasa akidai alipwe kiasi cha Pauni 500,00 kwa wiki na majogoo hao wa Anfield. Hauwezi kumlaumu Salah wala kuilaumu Liverpool.

Hawa wawili wote wanahitajiana. Liverpool wanamhitaji Salah na Salah anaihitaji Liverpool. Huyu mmoja ameifanya Liverpool kuwa moja kati ya klabu bora duniani na hii klabu imemfanya Salah kuwa mmoja kati ya wachezaji bora zaidi duniani kwa sasa.

Inawezekana kwa sasa wote wakawa sahihi kama wakivimbiana. Kila mmoja amemfaa mwenzake lakini ni katika misingi ileile ya urafiki wa Dangote na Gates. Sio misingi ya kimaskini kama hii hapa ambayo inaendelea Old Trafford.

Mwisho wa siku nadhani Pogba anaondoka Old Trafford mwisho wa msimu. Mkataba wake umekaribia kukata roho. Lakini ukitaka kupima kwamba hata yeye mwenyewe alikuwa tatizo pale Trafford jaribu kupima ni klabu ngapi ambazo zinapapatika kumtaka Pogba kwa sasa.

Mpaka sasa hatujui kama atarudi Juventus au ataenda kwao Ufaransa kucheza PSG au atakwenda Hispania kucheza Real Madrid au Barcelona. Ukweli ni kwamba amepoa. Anavuna alichopanda. Ni kama ambavyo Man United yenyewe nayo imepoa. Umeona kuna wachezaji wangapi siku hizi wanaoitamani Manchester United kama ilivyokuwa zamani?

Nadhani Man United na Pogba wasichekane sana. Wamefikishana hapo walipo. Kwa sababu hatujasikia lolote kutoka kwa Man United labda tumseme zaidi Pogba ambaye ndiye amekimbilia kwao Ufaransa na kutoa kauli nzito ya shutuma kwa Man United kwamba eti amepoteza bure miaka yake mitano aliyocheza hapo. Sio kweli. Wamepotezeana muda.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz