Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NYUMA YA PAZIA: Neymar, hayupo motoni wala peponi, tumsubiri Qatar 2022

Neymar Bresil Neymar Jr

Mon, 4 Jul 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Jinsi maisha yanavyokwenda kasi. Rafiki yangu, Neymar hayupo peponi wala motoni kwa sasa. Erling Haaland amehama. Tumepiga sana kelele na kujaribu kufikiria maisha yatakwenda vipi pindi akianza kuvaa jezi ya Man City chini ya Pep Guardiola.

Rafiki yetu mwingine, Kylian Mbappe ameamua kubaki alipo na ametushtua. Lionel Messi alikula sherehe ya ‘birthday’ Ibiza mapema wiki hii. Ametimiza miaka 35 na anaelekea ukingoni. Hatma yake haisisimui.

Cristiano Ronaldo hatujali kuhusu hatma yake. Akiondoka Manchester United sawa, akibaki sawa. Hatma yake haisisimui. Ameshafunga ukurasa wa maisha yake ya soka. Tumeshajua Ronaldo alikuwa nani katika soka. Februari mwakani atatimiza miaka 38.

Mkononi katika orodha hii tunabakiwa na rafiki yangu, Neymar. Ana miaka 30 kwa sasa. Ni miaka ambayo Messi na Ronaldo walikuwa moto. Ni miaka ambayo imemkuta Neymar akiwa amepoa tofauti na ambavyo tulikuwa tunafikiria.

Baada ya Ronaldo na Messi tulidhani dunia ingeshikwa na Neymar. Na mchezaji anapoishika dunia huwa haiwi ndani ya uwanja tu. Hata nje ya uwanja huwa anatingisha. Inakwenda katika aina yake ya maisha lakini pia katika masuala ya uhamisho.

Ni katika miaka hii ndipo ambapo tungeona kuwa Neymar hagusiki katika dirisha kama hili. Majuzi nimesikia akihusishwa na Newcastle United. Leo Neymar wa kuhusishwa na timu ambayo haichezi hata Ligi ya Europa? Sawa, hata kama kuna matajiri wameinunua Newcastle, lakini tulikuwa hatutazamii Neymar ahusishwe huko.

Halafu hapo hapo nikasikia kwamba matajiri wa PSG hawamtaki tena. Hawataki kumuweka katika mipango yao. Ni namna gani maisha yameenda kasi kwa Neymar kiasi hiki, inashangaza sana. Tulitazamia kwamba huu ndio ungekuwa muda wa Neymar kutuyumbisha.

Tulitazamia kwamba labda huu ndio ungekuwa muda wa Neymar kujaribu kurudi Hispania na kuvunja rekodi nyingine ya uhamisho wa dunia. Ni kama vile Ronaldo de Lima alivyoondoka Barcelona akaenda Inter Milan kisha akarudi Real Madrid.

Tulidhani kwamba huu ndio ungekuwa muda mwafaka kwa jina la Neymar kuhusishwa kwenda Manchester City au kwingineko. Haikuwa hivyo. Leo Neymar amepoa na hata PSG wenyewe hawana hofu naye. Kinachonisikitisha zaidi ni miaka yake. Hawezi kutushtua tena.

Kitu kibaya zaidi ni kwamba Neymar hajatimiza malengo akiwa na PSG. Walimchukua kwa rekodi ya uhamisho ya dunia kwa ajili ya kuwashindisha taji la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Kabla yake PSG haikuwahi kuwa na shida ya ubingwa wa Ufaransa.

Walishashinda ubingwa wa Ufaransa wakiwa na kina Zlatan Ibrahimovich, Edinson Cavani na wengineo. Walichotaka katika mradi huu wa Neymar hadi wakaenda kuvunja rekodi ya uhamisho ya dunia ililkuwa ni kuchukua ubingwa wa Ulaya.

Lakini mpaka sasa hajawawezesha kufanya hivyo. Sio yeye peke yake, hata rafiki yake, Mbappe hajawawezesha kufanya hivyo. Na baadaye akaja rafiki mwingine, Lionel Messi lakini hajawawezesha kufanya hivyo. Messi hauwezi kumlaumu kwa sababu tunajua anaelekea ukingoni. Neymar ndio haswa aliletwa kwa jukumu kama hili.

Achilia mbali hili, lakini Neymar ameshatimiza miaka 30, huku akiwa bado hajachukua tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia wala Ulaya. Kama ambavyo masuala yake ya uhamisho yalivyopoa basi ndivyo ambavyo maisha yake ya soka ndani ya uwanja yalivyopoa.

Huu ni msimu mwingine ambao hakuna unachoweza kuhesabu kwa Neymar. Ametwaa ubingwa wa Ufaransa na hii si habari mpya. Ukicheza PSG moja kwa moja unatwaa ubingwa huu. Katika miaka saba waliingiliwa mara moja tu na Lyon msimu uliopita.

Hajatwaa ubingwa wa Ulaya. Hajatwaa Europa. Hakuna ambacho kinaweza kumpeleka katika mapambano ya kuwania tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia. Labda anaweza kusubiri michuano ya Kombe la Dunia pale Qatar akiwa na kikosi cha Brazil.

Ambacho sijafahamu ni kama Mwanasoka Bora wa Dunia mwaka huu anaweza kutokana na michuano hiyo. Katika Ligi ya Ufaransa Neymar anaweza kusahau. Hauwezi kuwania tuzo ya Mwanasoka wa Dunia kwa kutwaa ubingwa wa Ufaransa.

Msimu huu ulioisha Neymar amefunga mabao 13 katika mechi 22 za PSG. Muda mwingi alikuwa katika kitanda cha hospitali akijaribu kuponya majeraha. Sidhani kama Kombe la Dunia litamsaidia kuwa mwanasoka bora wa dunia.

Wakati huo huo kuna wachezaji ambao wapo katika nafasi nzuri zaidi. Karim Benzema unawezaje kumuweka nyuma ya Neymar? Ametwaa ubingwa wa La Liga lakini pia wa Ulaya akiwa na Real Madrid. Kuna akina Kelvin de Bruyne na Mo Salah ambao wana kila sababu ya kuwa katika tatu bora.

Hapo ndipo unapokiri ugumu wa maisha kwa Neymar. Kwa msimu huu hakuna ndoto ambayo anaweza kuipeleka karibu na tuzo binafsi. Mwakani anatimiza miaka 31 na unashangaa kwamba pamoja na kuimbwa kwa kuwa na kipaji kikubwa lakini hakuwahi kutwaa tuzo hii.

Neymar anaweza kuwa jina kubwa katika soka la Brazil baada ya kupita kwa akina Rivaldo, Ronaldo de Lima, Ronaldinho, Kaka na wengineo lakini wote hawa walipata tuzo ya mwanasoka bora wa dunia kasoro yeye.

Nadhani tunaweza kusema kwamba Neymar ni mchezaji ambaye maisha yake ya soka yanaelea tu mpaka sasa. Maisha yake bora ya soka ni pale alipocheza sambamba na Lionel Messi na Luis Suarez akiwa na Barcelona na wakatwaa ubingwa wa Ulaya mwaka 2014.

Pengine labda angebaki na Barcelona halafu Messi akaondoka yeye angeutwaa ufalme wa Catalunya. Labda PSG haikuwa sehemu sahihi kwake. Yote haya tunakosa majibu halisi kwa sababu kila wakati maisha yake ya soka yanaonekana kuelea.

Na sasa katika dirisha kama hili la uhamisho tunakosa utamu wa maisha ya nje ya ligi kwa sababu jina lake limetulia. Hakuna kelele. Labda baada ya wiki tatu zijazo tunaweza kupokea kitu tofauti kuhusu yeye lakini kwa hali ilivyo sasa ni wazi kwamba ametuangusha.

Columnist: Mwanaspoti