Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NYUMA YA PAZIA: Naenda kumtazama Simeone akicheza dhidi ya Dunia nzima

Diego Simeone.jpeg Kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone

Sun, 10 Apr 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Naelekea Madrid na nitakuwepo Madrid Jumatano ijayo kumtazama Diego Simeone, Kocha wa Atletico Madrid akicheza dhidi ya kila mtu. Dhidi ya Man City, dhidi ya wachezaji wake, dhidi ya mashabiki wake, dhidi ya mashabiki wa timu pinzani, dhidi ya dunia.

Jumanne hii iliyopita alimuacha mdomo wazi, Kelvin De Bruyne. Kelvin katika umri wake wa sasa wa miaka 29 alisikika akisema: “Nimewahi kucheza na timu nyingi zinazojilinda sana dhidi yetu, lakini sikuwahi kukutana na timu ambayo ilicheza bila ya washambuliaji.”

Huyu ndiye Diego halisi tuliyemfahamu. Alitushangaza Jumanne usiku pale Etihad. Alipaki basi haswa. Alipaki katika namna ambayo hata Jose Mourinho alishaachana nayo kitambo. Aliweka mistari miwili ndani ya boksi lake kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi ya Man City kuanzia dakika ya kwanza hadi ile ambayo kipenga cha mwisho kingepulizwa.

Wapo walisifu mbinu zake. Lakini subiri kwanza. Tukumbuke kwamba mabingwa wa Hispania walikuwa wanacheza dhidi ya mabingwa wa England. Ligi mbili kubwa duniani. Inakuwaje timu moja inajiona kibonde kiasi kile cha kutengeneza mistari miwili mbele ya kipa wao, Jan Oblak huku wakiwa hawachezi pungufu?

Man City ni hatari, sawa. Timu nyingi zinakabiliana na Man City kwa kujilinda, lakini sio kwa namna ambayo Diego ametuonyesha. Angeweza kufanya kitu kizuri zaidi. Kuna klabu nyingi ambazo zina kiwango chini ya Atletico, lakini zinafanya vizuri zaidi dhidi ya Man City wakiwa Etihad au wakiwa katika viwanja vyao vya nyumbani.

Katika soka la kisasa unapocheza na timu kali kama Man City au Liverpool wote tunajua kwamba wapinzani watarudi nyuma. Lakini baada ya kurudi nyuma kuna kitu itabidi kifanyike wakati ukiwa na mpira. Kuna muundo mzuri ambao inabidi uutengeneze kwa ajili ya kushambulia. Diego hakutuonyesha kitu kama hicho.

Kuna namna ambavyo Man City huwa wanafungika. Namna ambavyo unaweza kufanya uhamisho wa mpira kwa haraka kutoka nyuma kwenda mbele. Unawakuta Man City wakiwa matatizoni. Haishangazi kuona msimu huu katika Ligi Kuu ya England wamepoteza mechi tatu na kutoka sare nne.

Timu nyingi ambazo zimepata mabao au matokeo ni zile ambazo zipo chini ya Atletico kwa kila aina ya uwezo. Kuanzia pesa, wachezaji, ukubwa wa uwanja na kila kitu. Kwanini Diego hatuonyeshi uwezo wake katika hilo? Nadhani ni kitu ambacho hana ubora nacho lakini kimekuwa kikitukera sisi wengine.

Katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kuna timu kadhaa ziliwahi kutoka Ulaya Mashariki na kupata matokeo Etihad. Lakini pia tunaweza kujiuliza, tangu Pep aichukue Manchester City hajawahi kuchukua ubingwa wa Ulaya. Timu ambazo zinamzuia kufanya hivyo huwa zinafanyaje? Kwanini Diego asiige hilo? Ni swali jingine.

Ninachoamini ni kwamba wachezaji wake hawataki kucheza hivyo. Wachezaji wake ni binadamu wa kawaida ambao wamezaliwa wakiwa na hisia za majivuno. Wamezaliwa na vipawa vikubwa. Kwanini wacheze kwa hofu ya kuhofia wapinzani wao. Siamini kama kina Joao Felix, Koke, Lorento, Luis Suarez na wengineo wanapenda kucheza vile ambavyo Diego anataka.

Nadhani Joao Felix angekuwa hatari zaidi kama angekuwa anacheza Liverpool au Manchester City ama Bayern Munich. Akili yake ingekuwa inaonyesha ufundi mkubwa eneo la mbele. Lakini tulimshuhudia Jumanne usiku akicheza karibu na mabeki wake wa kati kuizuia Manchester City. Sio haki. Sio sawa.

Najua mashabiki wa Atletico ni watiifu kwa Diego, lakini siamini kama wanapenda sana kile ambacho anafanya katika mechi kubwa. Labda wangependa kama ambavyo kile ambacho kina Jurgen Klopp na Pep Guardiola wanafanya kwa wengine. Siku moja wangependa kuamka na kuikuta timu yao ikitawala mchezo kwa soka safi na pasi nyingi.

Huku kwa wapinzani wangependa hivyo. Kwa mfano, Pep angeweza kuwa tayari kushambuliwa ili naye apate nafasi ya kushambulia vizuri. Hata hivyo haikuwezekana. Atletico walikuwa wameubana uwanja kikatili na waliamua kutocheza soka. Waliamua kuwa maadui wa mpira wa miguu.

Na kwa wachezaji hiki ndicho ambacho Kelvin De Bruyne alikuwa amelalamikia. Kumbe naye angependa kushambuliwa na wachezaji waliopania wa Atletico Madrid, lakini bahati mbaya hawakupewa maelekeo hayo. Kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya soka aliona timu ikicheza bila washambuliaji.

Kwa sisi watu wa kawaida ambao sio mashabiki wa Man City wala Atletico tulitaka kuona soka. Soka ambalo tulikuja kuliona saa 24 zilizofuata kati ya Chelsea dhidi ya Real Madrid. Soka ambalo tumekuwa tukiliona katika mechi nyingi ambazo tunatazama bila ya kujali matokeo yatakuwa vipi. Soka ambalo timu zinacheza.

Kunaweza kuwa na kibonde dhidi ya mtawala, lakini kibonde atajaribu kumuweka chini mtawala. Inaweza kuwa kwa mbinu za kujilinda kama ilivyokuwa kwa Diego, lakini pindi ambapo wangeupata mpira wangeweza kujaribu kufanya kitu. Diego hakujaribu kufanya kitu cha maana.

Nitakuwepo Wanda Metropolitan Jumatano ijayo kuona Diego atajaribu kufanya nini. Ni kitu ambacho watu wengi tunasubiri kuona. Man City itabaki kuwa ileile. Itabaki kuwa timu yenye hamu ya kupiga pasi nyingi na kuelekea katika lango la adui. Itabaki kuwa timu ambayo haitaridhika na bao moja walilofunga Etihad. Ni hapo ndipo tunasubiri kuona Diego atakuwa mtu wa namna gani.

Katika uwanja unaochukua mashabiki zaidi ya 60,000 wa timu pinzani kina De Bruyne wataendelea kucheza vilevile tu kama wanavyocheza Etihad. Je, Diego ataenda kubadilika? Ataishambulia City? Kama akiishambulia atatoa mianya ambayo hakuitoa Etihad.

Kama tofauti pekee itakuwa ni mashabiki, basi ni kitu ambacho kitachekesha sana. Kwamba hakushambulia Etihad kwa sababu alikuwa ugenini? Kwamba atashambulia Wanda Metropolitan kwa sababu atakuwa nyumbani? Sidhani kama wachezaji wakubwa kama wa Man City na kocha mkubwa kama wa Man City ataona kuna tofauti kubwa kati ya nyumbani na ugenini.

Nitakuwepo Wanda kujaribu kuona kile ambacho Diego atatupa baada ya kile alichokifanya katika mechi ya kwanza. Siamini kama atakuwa na maajabu makubwa zaidi ya kucheza kwa machale kama ilivyokuwa katika mechi ya Etihad. Siamini kama mashabiki wanaweza kuwa tofauti kubwa mbele ya kina De Bruyne.

Lakini, hapohapo nataka kuona hatima ya Diego na watu wake wa Atletico. Najua wanampenda sana, lakini mpaka lini watavumilia aina yake ya soka dhidi ya wakubwa? Wataendelea kuvumilia kile wanachokiona huku wakijidanganya kuwa wao ni timu kubwa? Hapana, timu kubwa haichezi kama wao walivyocheza dhidi ya Man City.

Lakini, hapohapo wote tujiulize. Manchester United wanasaka kocha, umewahi kusikia wanahusishwa na Diego? PSG wanakaribia kumfukuza kocha, umewahi kusikia wanahusishwa na Diego? Wakati Arsenal walipomfukuza Unai Emery uliwahi kusikia walihusishwa na Diego? Kuna kitu hakipo sawa kwake.

Columnist: Mwanaspoti