Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NYUMA YA PAZIA: Mungu mbariki Messi, dakika 90 za mwisho

Lionel Messi 1140x640 Lionel Messi

Mon, 19 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mwandishi mrembo wa kituo cha Televisheni cha Publica cha Argentina, Sofia Martinez alikuwa amesimama hatua moja kutoka kwa Lionel Messi. Peke yao. Machozi yalikuwa yanakaribia kumtoka. Na Messi mwenyewe alionekana mwenye hisia kali. Alikuwa anatabasamu, huku machozi yakikaribia kumtoka.

Sofia alimwambia Messi; “Kitu cha mwisho ambacho ninataka kukwambia, na sio swali, lakini nilitaka kukwambia, Fainali ya Kombe la Dunia inakuja, ni kweli Waargentina wote wanataka kushinda kombe hili.

“Nataka kukwambia bila ya kujali matokeo, kuna kitu ambacho mtu hawezi kukiondoa kutoka kwako na ni ukweli kwamba umeingia katika mioyo ya Waargentina. Kila mmoja wao. Naongea ukweli. Hakuna mtoto ambaye havai jezi yenye jina lako, haijalishi kama ni kweli feki au orijino. Hakuna ambaye anaweza kukuondoa moyoni na hii ni shukrani kwa furaha kubwa uliyoleta kwa watu wengi.

“Nataka kwa umakini mkubwa uyachukue maneno haya moyoni mwako kwa sababu naamini kuna kitu muhimu pengine kuliko kushinda Kombe la Dunia na tayari unacho. Hivyo asante sana nahodha wetu.” Alimalizia Sofia.

Binafsi Sofia aliuongelea moyo wangu. Aliongea kwa niaba ya mioyo ya mashabiki wa soka wanaoufahamu mchezo wenyewe. Ni kweli kwamba historia ya Messi haitafutika hata kama atashindwa kutwaa Kombe la Dunia hapo kesho.

Lakini subiri kwanza, mpaka ashindwe ndipo tutaendelea kuyarudia maneno ya Sofia. Kwa sasa Messi amebakiza saa kadhaa tu kuchukua Kombe la Dunia. Dunia inasubiri. Kila mtu anasubiri. Wasiosubiri ni watu wachache tu. Wanajulikana. Lakini zaidi ni wale wanaotoka katika kambi ya Cristiano Ronaldo.

Kuna hisia kwamba endapo Messi atatwaa taji hilo kesho basi mjadala wa nani zaidi kati ya Messi na Ronaldo utakuwa umekufa rasmi. Binafsi siamini hilo. Mimi ni shabiki mkubwa wa Ronaldo, lakini hapana shaka Messi ni zaidi ya Ronaldo. Tumeshajadili hili mara nyingi.

Kinachosubiriwa kwa sasa ni namna ya kuwafunga mdomo baadhi ya mashabiki waaminifu wa soka la zamani ambao wanaamini kwamba Messi hauwezi kumweka kundi moja na Diego Maradona na Pele kwa sababu hajawahi kutwaa Kombe la Dunia.

Na sasa Messi amebakiza dakika 90 au 120 kuchukua kombe hilo. Ndani ya uwanja, itawezekana? Ndio inawezekana. Wanacheza na moja kati ya timu ngumu duniani. Wafaransa. Mambo mawili yanaweza kumbeba Messi na wenzake.

Kwanza kabisa hakuna timu nyingine ambayo imeweza kutetea Kombe la Dunia nje ya Brazil ambayo ilifanya hivyo mwaka 1958 na kisha ikatetea 1962. Huenda Wafaransa wakakutana na bahati mbaya hiyo kwa mara nyingine.

Pia michuano ya mwaka huu imekuwa migumu kutabirika. Namna ambavyo timu za kawaida zimefanya mambo mengi makubwa. Sawa, mastaa wameng’ara, lakini michezo mingi imekuwa ya kitimu zaidi huku wale ambao hawatabiriki wakishinda mechi au kutoka sare.

Namna gani Hispania, Ujerumani, Brazil na England hazikucheza nusu fainali ni kwa sababu mchezo wenyewe umekuwa mgumu. Namna gani Japan, Morocco, Croatia wamecheza michuano hii na kuwang’oa vigogo? Inaashiria namna ambavyo mchezo wenyewe hautabiriki.

Lakini hata hawa Waargentina wenyewe waliingia kwa pupa katika michuano hii na kuangukia pua katika pambano la kwanza tu dhidi ya Saudi Arabia. Na ni hapohapo ndipo unapoweza kudhani kwamba labda Mungu amewapangia kitu Waargentina. Namna walivyopoteza pambano lile na kuchekwa, lakini sasa wapo fainali, Mungu ndiye anajua.

Kuna walioanza kwa mikwara na njiani wakaonekana ni tishio. Hispania alimpiga Costa Rica mabao 7-1. Brazil akamnyanyasa Korea Kusini. Muingereza akamnyanyasa Muiran kwa kumchakaza mabao mengi. Wote hao hawakufika nusu fainali. Labda kuna kitu ambacho Argentina wamepangiwa.

Lakini walau safari hii Messi anaonekana kuwa ana askari wa kwenda nao vitani kuliko ilivyokuwa katika fainali ya mwaka 2014. Pale alikuwa na wachezaji wengi wenye majina, lakini hawakuwa na madhara katika Kombe la Dunia. Sergio Aguero na Gonzalo Higuain hawakuwa na madhara makubwa kama ambayo Julian Alvarez au Lautaro Martinez walivyoonesha.

Kina Rodrigo De Paul na wengineo wamefanya kazi kubwa kumsaidia Messi kuanzia pale walipokosea dhidi ya Saudia hadi kesho watakapocheza fainali yao dhidi ya Ufaransa. Kikosi chao kimejaa wachezaji wanaopiga soka la shoka zaidi kuliko kutegemea zaidi vipaji pekee.

Kwa upande wa Messi hapana shaka amebakisha dakika 90 za maisha yake. Anaweza kukosa taji hili na heshima yake itabakia pale pale hasa ukizingatia kwamba amekuwa na fainali bora za Kombe la Dunia kuliko fainali za michuano mingine yoyote ambayo amewahi kuchukua.

Kama Mungu anaweza kutusikiliza, ukweli ni kwamba michuano hii itakuwa imekamilika kwa utamu zaidi kama Messi akiwa na kitambaa begani akinyanyua Kombe la Dunia. Pengine ndicho kitu pekee kilichobakia katika maisha yake ya soka.

Lakini vile pengine ndicho kitu pekee kilichobakia kwa mamilioni ya wafuasi wake duniani. Ni kama vile ambavyo mamilioni ya wafuasi wa Pele na Maradona wamekuwa wakitambia Kombe la Dunia ambalo mastaa hawa wamechukua.

Lakini Mungu anaweza kumpa Messi Kombe la Dunia kwa sababu kuna Messi mmoja tu ambaye, hili litakuwa pambano lake la mwisho la Kombe la Dunia. Pale Ufaransa kuna mastaa wengi ambao wamewahi kuchukua Kombe la Dunia miaka minne tu iliyopita.

Lakini wana vizazi vya kina Aurelien Tchouameni ambao wanaweza kulichukua kombe hili tena na tena katika siku za usoni. Messi hana fursa hiyo. Wafaransa wameikamata dunia katika soka. Jaribu kutazama ni fainali ngapi wameingia kuanzia mwaka 1998.

Columnist: Mwanaspoti