Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NYUMA YA PAZIA: Mnara kwa Roman Abramovich tafadhali..

Abra Pic Roman Abramovich

Sun, 6 Mar 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mara ya mwisho walitwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England mwaka 1955. Marekani walikuwa wanaongozwa na Rais, Dwight D. Eisenhower. Kuanzia yeye mpaka leo Marekani imeongozwa na marais 11 tofauti.

Na mara ya mwisho walipotwaa ubingwa wa England, Waziri Mkuu wa Uingereza alikuwa Sir Winston Churchill. Kuanzia hapo Uingereza imeongozwa na mawaziri wakuu 14 tofauti mpaka sasa katika zama hizi za Boris Johnson. Nyakati zimekwenda wapi?

Nazungumzia mara ya mwisho Chelsea kuchukua ubingwa wa England kabla ya mtu anayeitwa Abramovich kutua klabuni hapo. Aliinunua Chelsea mwaka 2003 kwa Pauni 140 milioni. Zilikuwa pesa nyingi nyakati hizo.

Chelsea walikuwa wapinzani wagumu wa kawaida katika Ligi Kuu ya England kabla ya Abramovich. Kuanzia hapo ndani ya miaka 19 ya utawala wa Abramovich kama tajiri wa Darajani, Chelsea imetwaa mataji 21. Ni mataji mengi kuliko miaka ambayo Abramovich ameitwaa klabu.

Juzi ni huzuni kwamba Abramovich ametangaza kuiuza Chelsea. Ni huzuni hasa. Uwe shabiki wa Chelsea au shabiki wa klabu nyingine ya soka la Kiingereza. Abramovich ni tajiri halisi wa soka ambaye Chelsea inapaswa kumjengea mnara.

Abramovich aliiendesha Chelsea kibepari tangu pale alipoikuchua mwaka 2003 mpaka juzi alipotangaza kuiuza. Ni tajiri wa mpira hasa ambaye anawapiku matajiri wengi wanaomiliki klabu hata kama wamemzidi pesa.

Njiani Abramovich hakusita kufanya mambo mawili katika kuitawala Chelsea. Kwanza ni kutia pesa kwa kununua mastaa wa bei mbaya. Utawakumbuka wengi aliowanunua lakini wachache aliwanunua kwa jeuri zaidi.

Kumbuka jinsi alivyoikatili Liverpool kwa kumnunua Fernando Torres katika dirisha la Januari akiwa katika ubora wake. Kuna ukatili kama huu aliowahi kuufanya? Halafu kuna ule wa kumnunua rafiki yake kutoka Ulaya Mashariki, Andriy Shevchenko bila hata idhini ya kocha wake, Jose Mourinho.

Hakuna aliyetazamia Sheva kucheza Chelsea nyakati hizo, lakini Roman alitoa pesa ili aungane na rafiki yake Stamford Bridge. Kisa kingine? Wake zao walikuwa marafiki nyakati hizo. Akamtoa Sheva Milan huku mashabiki wa Milan wakilalamika. Nguvu ya pesa.

Ukianza kuandika rundo la mastaa ambao Abramovich aliwanunua utawakuta wengi. Mastaa ambao bila ya yeye kamwe wasingegusa jezi ya Chelsea. Mastaa wa kiwango cha dunia ambao bila ya Abramovich wangeishia kucheza Barcelona, Real Madrid, AC Milan ya wakati huo, Arsenal, Manchester United, Juventus au Bayern Munich. Yeye aliwaleta mastaa hawa darajani.

Achilia sifa hiyo Abramovich alikuwa na sifa ya kuchukua uamuzi mgumu. Ndani ya miaka 19 Chelsea imefundishwa na makocha 13. Hakutaka hiki kitu kinachoitwa miradi (projects) kama ambavyo Mikel Arteta amevumiliwa kwa sasa Arsenal.

Abramovich alikuwa anatumbukiza pesa halafu anataka matokeo. Kama usingempa matokeo angekuonyesha mlango wa kutokea. Hii ndio namna ya kuendesha soka kibepari. Namna ya kuendesha soka kibiashara zaidi.

Ni tofauti na kina Steve Kroenke ambao walimvumilia Arsene Wenger kwa kukaa miaka 14 bila ya taji la Ligi Kuu England huku wakitukuza historia yake. Abramovich hakuwa mtu wa hivi. Iliwasaidia makocha na wachezaji kupambana. Hakukuwa na kocha aliyejisikia salama kwa sababu alisoma historia za waliotangua.

Kati yao walikuwepo rafiki zake. Mfano, Abramovich alikuwa rafiki mzuri wa Frank Lampard akiwa kama mchezaji. Alikuwa anapanda naye boti lake la kifahari (yacht) na kula bata katika fukwe za Ibiza. Baadaye akawa kocha wake. Matokeo yalipokuja kuwa ovyo akamfukuza.

Hata Jose Mourinho pia alikuwa rafiki yake. Haikumzuia kumfukuza. Baadaye Mourinho wakati yupo Real Madrid akakiri kwamba alikuwa rafiki wa karibu na Abramovich na alikuwa anaongea naye mara kwa mara. Baadaye akarudi tena Chelsea lakini mambo yalipokwenda kombo akamfukuza tena.

Na sasa Abramovich ameondoka Chelsea. Kipi kitafuata? Ni swali zito. Swali ambalo linawanyima usingizi na hamu ya kula mashabiki wa Chelsea. Haliwezi kuwanyima kula wachezaji wa Chelsea wala benchi la ufundi. Wana mikataba yao na klabu. Lakini ni mashabiki ndio ambao wana mikataba ya mioyo na klabu hizi.

Mpaka tutakapojua mtu ambaye atauziwa timu ndipo tunaweza kuhisi kitu ambacho kitafuata. Kwa sasa tunaweza kubashiri haya mambo mawili. Jambo la kwanza ni timu kwenda kwa mwekezaji ambaye sio Mwarabu. Chelsea wanaombea wapate mwekezaji Mwarabu kwa sababu mara zote Waarabu wanajua kumwaga noti.

Hata hivyo, Chelsea inahusishwa na tajiri kutoka Uswisi. Tatizo hapa ni kwamba nje ya Abramovich hatujawahi kuona tajiri mwingine asiye Mwarabu ambaye anamwaga sana fedha. Inawezekana familia ya Glazer imemwaga sana pesa Old Trafford lakini watu wanaamini zaidi katika Abramovich.

Zipo nyakati ambazo hata kuna klabu zetu nyingine zilitaka kumilikiwa na matajiri kutoka Uarabuni na ikishindana basi Russia kwa sababu walikuwa wanauona mfano kutoka kwa Abra-movich. Bahati mbaya Chelsea haiwezi kurudi kwa M-Russia mwingine kwa sababu matajiri wote wa Russia kwa sasa wanaonekana ni marafiki wa Vladimir Putin.

Lakini kwa klabu ambazo zinamilikiwa na Wamarekani inaonekana kama vile ni watu mabahiri. Arsenal, Liverpool na Manchester United kwa nyakati tofauti wamewahi kulalamikia matajiri wao. Najua kwamba Chelsea haitamani hili.

Hatujui kama Chelsea itampata tajiri ambaye atafuata nyayo za Abramovich katika umwagaji wa pesa pale inapohitajika. Hatujui. Endapo kama Chelsea itamkosa tajiri wa namna hiyo basi itarudi kwa wale matajiri ambao wanazijenga timu kwa uvumilivu na ‘project’ maalumu.

Binafsi naamini katika sera za Abramovich kwa sababu katika kipindi cha utawala wake Chelsea imechukua mataji mengi kuliko klabu zote za England. Wanafuatiwa na Manchester United, Manchester City, Liverpool kisha Arsenal. Hii inaonyesha wazi kwamba sera za Abramovich zimefanikiwa katika soka la England na pia Ulaya ambako ametwaa Ligi ya Mabingwa mara mbili huku akiingia fainali tatu. Licha ya kukashfiwa kwa kufukuza makocha mara kwa mara na pia kununua wachezaji wa bei mbaya kwa kusaka mafanikio ya muda mfupi, bado inaonekana kwamba sera zake zimefanikiwa.

Tutakapotazama nyuma wote ambao sio mashabiki wa Chelsea tunajua dhahiri katika mioyo yetu kwamba tunatamani kuwa na tajiri kama Abramovich. Hata Chelsea wanajua kwamba watammisi sana Abramovich. Kwa sasa wanachopaswa ni kumjengea mnara tu nje ya Stamford Bridge. Yeye ndiye aliyeibadili kwa kiasi kikubwa katika historia yao.

Columnist: Mwanaspoti