Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NYUMA YA PAZIA: Kwaheri, Tchau, Goodbye Edson Arantes Do Nascimento 'Pele'

Pele Vs Putin Pele

Sun, 1 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Imeondoka alama ya kila kitu katika mpira wa miguu na maisha kwa ujumla. Edson Arantes do Nascimento alijukana kama Pele amefariki dunia. Ni alama ya kila kitu. Anawakilisha kila kitu na kila harakati ya maisha. Amemaliza uhai wake juzi katika kitanda cha Hospitali ya Albert Einstein pale Sao Paulo.

Zaidi ya miaka 45 tangu aachane na soka vizazi vilivyofuata vilimjua Pele. Vilimtazama katika mikanda ya soka, vilimtazama katika vitabu, vilimtazama kwa makini popote alipokwenda na kuhudhuria. Wachache walimuona akiwa uwanjani anacheza, wengi hawakumuona.

Mwanadamu yeyote anayekumbukwa na kuhusudiwa na watu wengi ambao hawakumuona basi ujue alikuwa ni alama ya alichofanya. Pele aliacha alama nyingi. Sitaki kuandika namba nyingi za uwanjani kwa kile hasa alichokifanya. Kwa kifupi tu ni kwamba alitwaa Kombe la Dunia mara tatu. Hakuna mchezaji aliyewahi kufanya hivyo.

Lakini kwa wastani wa mabao na mechi alizocheza, inatajwa kwamba Pele ana wastani wa kufunga bao moja kwa kila mechi. Haya yote yalichangia kumfanya Pele awe alama ya dunia lakini kuna mengi ambayo yamewafanya wazee wa zamani kuturithisha kumjua Pele.

Pele alikuwa mwanasoka wa kwanza supastaa duniani. Ni kweli mchezo wa soka ulikuwepo kabla yake. Ni kweli walikuwepo wachezaji wazuri kabla yake. Lakini Pele anabakia kuwa mchezaji wa kwanza supastaa duniani.

Pele alikuwa mchezaji wa kwanza jina lake kuwa kubwa nje ya mipaka ya nchi yake kisha likatambaa dunia nzima. Vijijini kote. Katika kila mchezo au fani kuna mtu wake. Katika ngumi alama ni Muhammad Ali. Katika muziki alama anaweza kuwa Michael Jackson. Katika soka alama ni Pele.

Ya kila kitu, Pele alikuwa mweusi. Mastaa wote wakubwa waliowahi kutokea katika uso wa ulimwengu walikuwa Wazungu. Akina Ferenc Puskas, kina Lionel Messi, hasimu wake, Diego Maradona, Johan Cruyff, Cristiano Ronaldo na wengineo walikuwa wazungu. Lakini Pele alikuwa mweusi.

Pele ni miongoni mwa alama chache za watu weusi ambazo zililetea heshima ngozi yenyewe. Ni miongoni mwa watu wachache weusi ambao uwezo wao uliwanyamazisha wazungu katika zama za ubaguzi uliotopea.

Lakini zaidi alianza kufanya hivyo akiwa na umri mdogo. Pele alicheza fainali ya kwanza Kombe la Dunia akiwa na umri wa miaka 17 tu. Na ndiye ambaye alikuwa staa wa timu. Jaribu kufikiria kijana mdogo mwenye umri wa miaka 17, mweusi na anayecheza katika zama za ubaguzi, anashinda kila majaribu na kutwaa Kombe la Dunia huku akiwa staa mkubwa.

Hawa kina Kylian Mbappe, Lionel Messi na wengineo waliowahi kutwaa Kombe la Dunia walishindwa kufanya hivyo wakiwa na umri huo. Na hata katika umri huo hawakuweza kuitwa katika timu zao za taifa, achilia mbali kupangwa au kuwa mastaa wa timu. Pele aliweza.

Na sio Pele alikuwa ni mchezaji pekee mwenye kipaji Brazil, hapana, walikuwepo lakini Pele alikuwa mkubwa zaidi. walikuwepo akina Jarzinho, Vava, Garrincha, Tostao, Carlos Alberto na wengineo.

Si ajabu kama Pele asingekuwepo kuna mwingine ambaye angechomoza kuwa staa ambaye tunamfahamu. Hata hivyo, uwepo wa Pele ulifunika majina mengine kiasi kwamba wote tulimfahamu zaidi Pele kuliko wachezaji wenzake ambao nao walikuwa katika bora zaidi.

Lakini Pele aliyafanya hayo akitokea katika umaskini. Hii ni alama nyingine ya uimara wa binadamu. Alitokea katika umaskini uliotopea katika kitongoji cha Bauru jijini Sao Paulo na kuja kuiweka dunia katika viganja vyake vya mkononi. Sio wanadamu wengi wamefanikiwa kupindua historia za maisha yao kama Pele alivyofanya.

Alipata pesa yake ya kwanza kwa kufanya kazi kama mtumishi katika kibanda cha kuuza chai. Utotoni baba yake hakuweza kumnunulia viatu vya soka na badala yake Pele alicheza na soksi ambazo alizijaza makaratasi. Safari yake ya kwanza Sweden na Timu ya Taifa ya Brazil ndio ilikuwa safari yake ya kwanza kutoka nje ya Brazil.

Wakati akicheza soka Pele ndiye alikuwa mchezaji anayelipwa zaidi duniani. Jaribu kuona namna ya alikotoka na alikofika. Wanadamu wengi wanaoacha alama kama yeye huwa wanatoka katika aina hii ya maisha na kubadili mkondo wa historia.

Baada ya kuachana na soka Pele aliendelea kuwa alama ya mwanamichezo bora na mtu muungwana katika soka. Tofauti na hasimu wake wa karibuni, Diego Maradona aliyetaliwa na matumizi ya dawa za kulevya na kashfa mbalimbali, Pele aliendelea kutambulika kama mwanadamu muungwana ambaye alitumwa kisha kujituma katika kazi mbalimbali za kijamii.

FIFA ilipendelea kumuweka mbele zaidi Pele katika shughuli mbalimbali na popote ambapo Pele alikwenda alitambulika kama Mfalme. Wazungu, Waarabu, Wahindi, Waswahili na wetu wengine walipenda kumuona Pele. Popote alipopita walimshangilia. Kinachofurahisha ni kwamba sio wengi walipata bahati ya kumuona.

Mimi ni mmoja tu kati ya watu wengi ambao wameishia kumuona Pele katika mikanda ya Video. Lakini kwa wale ambao hawajamuona wanaweza kumfahamu vema kupitia maoni ya watu wengine. Mmoja kati ya watu ambao niliwahi kusikiliza maoni yao kuhusu Pele ni nahodha wa zamani wa England, Sir Bobby Moore ambaye alitwaa Kombe la Dunia na England mwaka 1996 pale Wembley.

Huyu aliwahi kusema “Pele ndiye mchezaji aliyekamilika zaidi ambaye nimewahi kumuona, alikuwa na kila kitu. Alitumia miguu yake yote miwili, alikuwa anafanya maajabu hewani, alikuwa na uwezo mkubwa wa kuwapita watu kwa akili yake.

Alikuwa na uwezo mkubwa wa kuwakimbia wapinzani wake. Alikuwa na futi tano na inchi nane tu lakini alionekana kama vile bonge la jitu uwanjani. Alikuwa na uwiano mzuri wa kila kitu na maono yasiyopimika. Alikuwa ni mchezaji mkubwa kwa sababu angeweza kufanya kila kitu uwanjani.”

Baada ya kila kitu katika mambo haya Pele alienda kuwa mkubwa nje ya uwanja. Mithili ya Rais wa nchi. Hata hivyo, kuna vitu viwili ambavyo Pele hakuweza kuvifanya. Labda kwa sababu Mungu hawezi kukupa kila kitu au labda kwa sababu hakuamua kufanya.

Pele hakuweza kuwa kocha wala kuwa mchambuzi wa soka. Kama alikaa studio basi ilikuwa ni kwa sababu ya kuulizwa maswali yanayohusu yeye mwenyewe na maisha yake.

Ni tofauti na mastaa wengi wakubwa waliokwenda kuwa makocha au wachambuzi.

Pele amekwenda. Amewafuata marafiki zake. Amewafuata akina Nelson Mandela na Muhammad Ali ambao walikuwa alama ya mtu mweusi katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na unyanyasaji mwingine wa madaraja ya binadamu.

Pele alikuwa zaidi ya mwanasoka. Alikuwa alama. Apumzike kwa amani Edson Arantes do Nascimento ‘Pele’. Waswahili tunasema ‘Kwaheri’ Wareno wanasema ‘tchau’, Waingereza wanasema goodbye.

Columnist: Mwanaspoti