Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NYUMA YA PAZIA: Kuna dunia ya Ronaldo halafu kuna yetu

F9C285CA AC5F 4C14 8EB8 8BC47A996B00.jpeg Cristiano Ronaldo

Sun, 11 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Hutokea ghafla wakati mwingine dunia zinakuwa mbili bila ya kujijua. Rafiki yangu mmoja aliwahi kuniambia kwamba vichaa huwa wanatuona sisi ni vichaa. Wanaamini kwamba wao wapo sahihi na sisi ndio tuna matatizo. Dunia mbili tofauti.

Ni kama zilivyo dunia mbili za sasa. Dunia ya Cristiano Ronaldo. Labda anaishi na mama yake, dada yake, watoto wake na mpenzi wake kipenzi, Georgina. Halafu kuna dunia nyingine ambayo tunaishi sisi sote wengine tuliobaki.

Dunia ya Ronaldo inamwambia kwamba yeye hajaisha. Yeye ni Ronaldo yule yule aliyetua uwanja wa ndege wa Manchester akitokea kwao Madeira kusaini Manchester United. Dunia yake mwenyewe inamwambia yeye ni Ronaldo yule yule ambaye alitua uwanja wa ndege ya Madrid akitokea Manchester mwaka 2009 kujiunga na Real Madrid.

Baada ya Erik Ten Hag kujaribu kumuaminisha Ronaldo kwamba amekaribia siku zake za mwisho kucheza soka la kiwango cha juu, sasa ni zamu ya kocha wake wa Ureno, Fernando Santos kujaribu kumuaminisha Ronaldo kwamba zama zake zimefika mwisho.

Katika dunia hii ya sisi wengine, Ronaldo sio yule ambaye tulimfahamu na kumpenda. Santos naye anaamini vile vile. Alijaribu kufumba macho katika mechi tatu za kwanza na kumuanzisha Ronaldo. Mechi zote Ronaldo hakuna alichofanya zaidi ya kusingizia amefunga bao katika pambano dhidi ya Uruguay. Halikuwa bao lake lilikuwa la Bruno Fernandes.

Pambano la mwisho la makundi alitolewa akazira. Na katika pambano la mtoano dhidi ya Uswisi, Santos aliamua kung’ata jongoo kwa meno kwa kumweka nje Ronaldo. Hapa kuna jambo moja la msingi. Jamie Carragher aliwahi kuungana mkono mawazo yangu.

Carragher alisema wazi kwamba Ronaldo alikuwa amewekwa benchi sio kwa sababu alikasirika kwa kutolewa katika mechi iliyopita, hapana, ni kwa vile kiwango chake kilikuwa dhaifu katika mechi alizopangwa. Nadhani Santos alitumia mwanya huo kumwacha nje Ronaldo.

Ukweli ni kwamba Ronaldo aliye na miaka 24 usingeweza kumweka nje kwa sababu yoyote ile. Hata kama alikuwa amepiga buti chupa za maji pale katika benchi usingediriki kumweka nje katika mechi ijayo. Subiri kwanza, hata tukio lenyewe lisingeweza kutokea kwa sababu kwanza Ronaldo mwenyewe asingetolewa katika siku husika.

Na majuzi baada ya kuwekwa nje katika pambano dhidi ya Uswisi imeelezwa kwamba Ronaldo alikuwa anataka kuondoka zake kambini na kurudi nyumbani Ureno. Lakini kumbuka kwamba picha zinamuonyesha Ronaldo akiwa peke yake mara baada ya kumalizika kwa pambano hilo huku wenzake wakiwa wanashangilia.

Dunia ya Ronaldo inamuambia kwamba Ronaldo ni yule yule. Ni dunia inayomwambia kwamba Ronaldo anastahili kuanza mechi na anastahili kumaliza mechi. Ni dunia ambayo inamwambia Ronaldo hastahili kuingia uwanjani kipindi cha pili. Ni dunia ambayo pia inamwambia Ronaldo kwamba hastahili kutolewa uwanjani kipindi cha pili.

Kibinadamu Ronaldo ana ugonjwa. Ana ugonjwa wa kutokubali matokeo. Ugonjwa huu unatokana na ukweli kwamba Ronaldo ni mpambanaji ambaye anajiamini. Lakini kujiamini kwake kulikopitiliza kumesababisha asimamishe mshale wa saa.

Licha ya aliyecheza nafasi yake, Goncalo Ramos kufunga mabao matatu katika pambano dhidi ya Uswisi bado nadhani Ronaldo hakuona kama uamuzi wa kocha ulikuwa sahihi. Huyu ndiye Ronaldo wa leo. Anaamini kwamba dunia inamkosea.

Kwa sasa anakorofishana na kila mtu anayewaza tofauti kuhusu yeye. Amekorofishana na kocha wa United, amekorofishana na wachezaji wenzake wa zamani kina Gary Neville na Wayne Rooney ambao walizungumza ukweli wao kuhusu yeye. Amekorofishana na wachambuzi wengine ambao walizungumza ukweli kuhusu yeye.

Na sasa imekuja kuwa zamu ya Santos. Hawa wote ambao wamezungumza tofauti kuhusu yeye wanaishi katika dunia yetu. Sio dunia ambayo inamchukia Ronaldo bali ni dunia ambayo imeamua kuukubali ukweli. Ronaldo tunampenda sana lakini muda umefika wa kukiri kwamba nyakati zake zimepita.

Ronaldo anakichukulia kitu hiki kama suala binafsi. Hapana, ni ukweli. Kama ingekuwa ni amri zetu basi wachezaji kama Ronaldo na Lionel Messi tungependa wagande katika umri wa miaka 24 kwa muda mrefu wa maisha yao. Hata hivyo siku huwa hazigandi.

Kinachotokea kwa sasa ni kwamba Ronaldo anamuweka wakati mgumu kila mtu aliyempenda. Hataki kila mtu atoe mawazo yake. Zaidi ni kwamba ataendelea kutuweka katika wakati mgumu. Kwa mfano, hasimu wake mkubwa Messi amekubali hata kabla ya kuanza kwa michuano hii kwamba atastaafu soka la kimataifa pindi michuano hii ya Qatar itakapomalizika.

Hadi sasa Ronaldo hajaonyesha dalili yoyote kwamba atastaafu kucheza soka la kimataifa pindi michuano hii itakapomalizika. Mbaya zaidi ni kwamba pindi anapoendelea kuwepo bado ataidai nafasi yake mbele ya akina Rafael Leao au Goncalo Ramos.

Kumpunguzia lawama kocha nadhani ni bora Ronaldo angetoka katika dunia yake akarudi katika dunia yetu. Kati yaa mambo ambayo tunatamani Ronaldo ayafanye katika dunia yetu ni kustaafu katika soka la kimataifa na pia kwenda zake Saudi Arabia kuchukua pesa.

Kwa sasa sio kwa Manchester United tu, Ronaldo hawezi kucheza hata katika klabu za kawaida za soka la Ulaya. Hawezi kucheza hata Brighton and Hove. Mchezo wenyewe umekuwa na mahitaji makubwa na Ronaldo atatimiza miaka 38 Februari 5 mwakani.

Kama akienda katika timu nyingine ya Ulaya, iwe Napoli, Lazio, Leicester City au Borrusia Dortmund Ronaldo ataendelea kuishi katika maisha yale yale kama ya Ten Hag. Makocha watamlazimisha kutompanga baadhi ya mechi, kuna mechi watataka aingie kipindi cha pili, kuna mechi watamtoa kipindi cha pili.

Kama hayupo kwa ajili ya haya ni wakati sahihi wa kurudi katika dunia yetu akaenda zake Saudi Arabia ambapo kuna mkataba mnono wa kufungia maisha ya soka ambao unamsubiri. Bado utakuwa mkataba ambao utamfanya awe mchezaji anayelipwa zaidi duniani.

Lakini akumbuke tu, pia kuwaachia kina Leao na Ramos. Hata yeye wakati fulani aliachiwa timu na kina Luis Figo, Manuel Rui Costa, Nuno Gomes na wengineo. Soka ni mchezo wa kubadilishana vijiti. Ni wazi kwamba kijiti chake kimefika mwisho. Kama anaweza kurahisishia mambo basi hizi ni nyakati bora zaidi kwake.

Columnist: Mwanaspoti