Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NYUMA YA PAZIA: Kumbe ndoa ya Simeone na Atletico bado ni changa

Simeone Pic Kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone

Sun, 17 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Niliona kwa macho yangu. Mita chache kutoka nilipokaa. Diego Simeone akiwapigia makofi mashabiki wa Atletico Madrid makofi zikiwa zimebaki dakika tatu kabla ya pambano dhidi ya Manchester City kumalizika. Wakalipuka kwa makofi mengi. Uwanja mzima. Majukwaa yote. Subiri, sio kwamba alikuwa amewahamasisha washangilie zaidi ili wapate bao la kusawazisha matokeo ya Etihad. Hapana. Alikuwa anawashukuru kwa kusimama nyuma ya timu yao kwa muda wote mpaka dakika hizi ambazo pambano lilikuwa linakata roho. Ilinishangaza sana. Sikutegemea.

Mashabiki wote walikuwa wamesimama. Wao walikuwa kama vile wanamjibu kwamba wamefurahia walichokiona hata kama wanaondoka katika michuano. Kwetu angejibiwa kwa kejeli na matusi juu. Na wapo ambao wangemwambia “Hatukutakii.” Lakini hapa majukwaa ya Wanda Metropolitano yalikuwa yamesimama kumshukuru ingawa walikuwa wanakaribia kutolewa katika michuano mikubwa duniani kwa tofauti ya bao moja tu.

Kuanzia hapo nilikata tamaa. Kwamba yamekuwa mawazo yangu kwa muda mrefu kuona Simeone anaondoka Atletico Madrid. Kwamba labda sasa imetosha kwa mashabiki kuona Diego akiichezesha timu kigumu zaidi katika staili ya kujihami hasa anapocheza dhidi ya timu kubwa.

Nilishangaa. Urafiki wa Simeone na mashabiki wa Atletico umepitiliza. Ni ndugu wa damu waliopitiliza. Wana urafiki wa machozi, jasho na damu. Kwa mashabiki wa Atletico, Simeone ni shujaa, Simba wa vita, mpiganaji. Ni mwenzao. Mashabiki wengi wa Atletico ni wale wa daraja la kati na daraja la chini la maisha. Wale wa Real Madrid ni wa daraja la juu.

Nilidhani kwamba Atletico labda walikuwa wanakaribia kumchoka Simeone. Nilikosea sana. Jumatano usiku pale Wanda Metropolitano niligundua kwamba mapenzi baina yao yanaongezeka. Wana nyimbo zaidi ya nne za kumtukuza licha ya staili yake hiyo hiyo ya soka. Kwao ni ‘Mungu mdogo.’Pia nimegundua kwamba wote wana tabia moja. Mashabiki na Diego. Tabia ambayo wamewaambukiza wachezaji. Baada ya pambano kumalizika niliona kitu cha ajabu ambacho sijawahi kukiona popote kwingine. Labda kwa sababu sijawahi kuingia Uwanja wa Anfield. Mashabiki hawakuondoka uwanjani na badala yake wote wakaanza kuimba nyimbo za kuitukuza timu yao.

Wachezaji walikuwa wamesimama uwanjani kwa utulivu wakiangalia majukwaani mashabiki wakiimba. Ilikuwa ni kama vile walikuwa wanapokea saluti kutoka kwa mashabiki. Kilichonishangaza zaidi ni kwamba Jumanne usiku Real Madrid walikuwa wameitoa Chelsea pale Santiago Bernabeu, lakini mashabiki hawakushangilia sana kama hawa ambao timu yao ilikuwa imeondoshwa mashindanoni.Baadae nikakumbushwa kwamba Atletico hawawezi kuachana

kirahisi na Simeone kwa sababu amewatoa jalalani. Kabla hajafika yeye walikuwa hoi kweli kweli. Ubingwa wa mwisho wa La Liga ulikuwa mwaka 1996. Yeye ndiye aliyewapatia tena mwaka 2014. Ina maana miaka 18 baadae. Na msimu uliopita aliwapa tena.

Katika kombe la mfalme maarufu kama Copa de la Rey pia walikuwa wamechukua mara ya mwisho 1996, lakini yeye aliwarudishia mikononi 2013 ikiwa ni mwaka mmoja kabla hajawarudishia La Liga. Kumbe ilikuwa katika maandalizi ya kuwarudishia La Liga.

Kwa kuamini kwamba Simeone alikuwa amewarudisha mjini, huku klabu ikianza kuwa tajiri tena. Atletico waliamua kumfanya Simeone awe kocha anayelipwa zaidi duniani kwa sasa. Jaribu kufikiria. Mbele ya Jurgen Klopp, mbele ya Pep Guardiola. Mbele ya kila kocha.

Lakini kitu kingine ni kwamba Simeone alikuwa mchezaji wao. Mwenye tabia hizi hizi kama wachezaji wao wa sasa wakorofi au kama mashabiki wao wakorofi. Alikuwa mfia timu angeweza kufanya kila kitu kwa ajili ya timu kwa ajili ya kupata

ushindi. Ku-mbe amekuwa mwenzao tangu akiwa kocha na sasa mchezaji. Ndani ya uwanja katika pambano hili dhidi ya City, Simeone alinishangaza. Alifanya kile kitu ambacho wiki iliyopita niliandika hapa kwamba makocha wakubwa wanafanya. Alilinda kwa nidhamu na kushambulia vyema. Ilikuwa mechi tofauti kabisa na ile ya Etihad. Na unajiuliza, kwanini Simeone hafanyi vile siku zote? Kwanini hasa? Timu ngapi zimewahi kufunga mabao Etihad?

Wachezaji mafundi anao kikosini na walionyesha hivi dhidi ya City Jumatano usiku pale Wanda Metropolitano. Joao Felix, Koke, Antoine Griezman, Luis Suarez na wengineo wengi. Kwanini anashindwa kucheza mpira na kuiweka timu pinzani majaribuni? Angeweza kupata bao moja Etihad na si ajabu asingetoka.

Makocha wenzake wametengeneza fikra hizi katika viwanja vyote viwili. Kiwanja cha nyumbani na kiwanja cha ugenini. Ndio maana Jurgen Klopp aliondoka na mabao mawili katika uwanja wa Etihad wiki iliyopita. Ni kitu cha kawaida kwa timu kubwa kwenda Etihad na kufunga na mabao. Sasa kwanini Simeone alikwenda na kutengeneza mistari miwili mbele ya kipa wake, Jan Oblak huku akiwa hana mpango wa kushambulia?

Ndoto yangu ya kuona Atletico inachukua kocha mpya kijana ambaye ataifanya icheze soka la kusisimua kumbe inabidi isubiri kwanza. Kwamba wamsake kocha kama Klopp au Pep kwa ajili ya kucheza soka maridadi la kusisimua inabidi nisubiri sana. Haitatokea kwa sasa hivi. Wao wanasisimuliwa na aina ya mpira ambao Simeone anawachezesha.

Uwanja wa Wanda Metropolitano bado unajaa mashabiki 68,000 na zaidi kushuhudia mpira huu huu wa Simeone na mashabiki wanaonekana kuridhika na wanachokiona. Na hata mpira unapoisha wanakuwa na hamu ya kuiona timu yao ikicheza tena wikiendi ijayo.

Lakini zaidi ni kwamba juzi Alhamisi nilikuwa Nou Camp nikishuhudia Barcelona wakichapwa mabao 3-2 na Frankfurt. Naweza kusema kwamba kwa nilichokiona Bernabeu, Wanda Metropolitano na Nou Camp basi mashabiki wa Atletico ndio mashabiki bora zaidi katika soka la Hispania.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz