Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NYUMA YA PAZIA: Kuanzia Lebron James hadi Harry Kane ubabe ubabe tu

Lebro James Bro.jpeg Lebron James

Sun, 19 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Aprili 5, 1984, siku saba kabla Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine hajafariki kwa ajali ya gari pale Morogoro, Kareem Abdul-Jabbar alikuwa akiweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote katika mchezo wa kikapu, NBA, nchini Marekani.

Miaka 38 baadaye, rekodi hii imevunjwa Februari 7 mwaka huu. Namaanisha wiki iliyopita. Aliyevunja ni LeBron James. Alihitajika kufunga pointi 36 dhidi ya Oklahoma wiki iliyopita kufikia na kupita idadi ya pointi 38,387 ambazo Kareem alitupia hadi alipoamua kustaafu kikapu mwaka 1989.

Ilimchukua LeBron misimu 20 ya NBA kuvunja rekodi hii. Lakini hata hivyo angalia watu waliopita hapa katikati bado walishindwa kuivunja. Kina Shaquille O’Neil, kina Michael Jordan, kina Hakeem Olajuwon. Wote hawa walishindwa mpaka LeBron alipoweza. Labda kwa sababu LeBron amedumu kwa muda mrefu katika mchezo.

Tuna bahati ya kuishi katika nyakati ambazo rekodi zinavunjwa. Bahati iliyoje. Katika soka maisha yamekuwa haya haya tu. Tunaishi katika zama ambazo vijana wa sasa wanavunja rekodi. Ni rekodi za miaka mingi lakini tunajiuliza kwanini zinavunjwa sasa na sio miaka ya tisini.

Siku mbili kabla ya LeBron hajavunja rekodi hii, Harry Kane wa Tottenham Hotspur alikuwa akivunja rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote klabuni kwake. Alivunja rekodi iliyowekwa kwa zaidi ya miaka 50 na mkongwe, Jimmy Greaves. Wakati Greaves aliondoka klabuni akiwa amefunga mabao 266, Kane amefunga mabao 267.

Kwa sasa Kane anaisaka rekodi ya mfungaji bora wa muda wote katika Ligi Kuu ya England. Mpaka sasa inashikiliwa na Alan Shearer aliyefunga mabao 261. Kane amefunga mabao 201. Kama akicheza kwa misimu mitatu tu katika ligi kuu ya England nina uhakika ataivunja rekodi ya Shearer. Ni kitu ambacho kinawezekana kama asipohama kwenda Hispania au Ufaransa.

Tunaishi katika zama ambazo Neymar amevunja rekodi ya Pele. Rekodi ya mfungaji wa muda wote ya Brazil. Hapa katikati kina Ronaldo de Lima na Romario walishindwa. Tunaishi katika zama ambazo Lionel Messi alivunja rekodi ya Diego Maradona na kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Argentina.

Wayne Rooney amevunja rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote Manchester United akivunja rekodi ya Sir Bobby Charlton. Jaribu kufikiria Charlton aliacha lini soka. Jaribu kufikiria hapo katikati wamepita wakongwe wangapi Manchester United. Kijana mdogo kutoka jiji la Liverpool akaja kuwavunjia rekodi yao.

Na katika timu ya taifa ya England, Kane na Rooney wote kwa pamoja ni wafungaji bora wa muda wote wakiwa na mabao 53. Walivunja rekodi ya Gary Lineker. Tunaishi katika kizazi ambacho rekodi nyingi za klabu na zile za timu ya taifa zimevunjwa. Wengi waliovunja ama wanaendelea kucheza soka au wameacha kucheza soka miaka michache iliyopita. Ni wachezaji wa kizazi hiki hiki.

Kwanini hapo katikati kulikuwa na wachezaji wengi mahiri lakini hawakufanikiwa kuvunja? Zimebaki rekodi chache ambazo hazijavunjwa lakini nyingi zimevunjwa na wachezaji wa kizazi hiki. Kuanzia Kombe la Dunia, Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, ligi mbalimbali pamoja na timu za Taifa katika mabara mbalimbali.

Kuna mawazo mengi. Kwamba mchezo wenyewe umekuwa dhaifu kuliko ilivyokuwa zamani. Kwamba ushindani umepungua tofauti na ilivyokuwa zamani. Wapinzani wamekuwa dhaifu tofauti na ilivyokuwa zamani. Kwamba wakati ule ilikuwa ngumu kwa kina Pele kufunga mabao mengi zaidi kutokana na kukwatuliwa mara kwa mara.

Kwamba kina Cristiano Ronaldo wamekuwa wafungaji bora wa muda wote katika nchi zao kutokana na udhaifu wa mataifa kama Malta, San Marino na wengineo ambao mara kwa mara utasikia wamebugizwa mabao 12-1. Ni kitu cha kawaida tu katika miaka ya hivi karibuni.

Lakini inadaiwa kwamba mchezo wenyewe umekuwa wenye kasi kuliko zamani. Mwanasoka wa zamani alikuwa anakimbia kilomita saba tu lakini leo kuna wanasoka ambao wanakimbia kilomita hadi 12. Eneo ambalo leo Casemiro anakimbia uwanjani ni tofauti na eneo ambalo zamani Nicky Butt alikuwa anakimbia.

Wachezaji wa kisasa wapo fiti mara mbili ya wachezaji wa zamani. Teknolojia imewafanya pia wawe fiti zaidi. Kuna vifaa vya kisasa vya kuwawezesha kutambua kasi yao uwanjani. Wakiwa mazoezini tu unajua kwamba fulani amekimbia kilomita ngapi na kwa kasi gani.

Zamani mchezo ulitegemea zaidi kipaji lakini leo tuna wachezaji wengi ambao wamekuwa wakitamba kwa sababu wapo fiti zaidi na wala hawana vipaji vikubwa. Hawa ndio wanaweza kuupeleka mpira kwa kasi zaidi tofauti na ilivyokuwa zamani. Zamani watu walikuwa wanatembea zaidi lakini siku hizi mchezo unatembea zaidi.

Kasi ya mchezo imekuwa ikiwanufaisha wachezaji. Lakini pia mchezo wenyewe umebadilika na umekwenda katika mifumo zaidi. Zamani mfumo ulikuwa mmoja tu 4-4-2 lakini leo kumekuwa na mifumo mingi tofauti ambayo inawawezesha washambuliaji wa kisasa kufunga mabao mengi zaidi. Inatajwa kwamba wachezaji wa zamani walikuwa wanacheza kibinafsi tu.

Inatajwa kwamba hata NBA mchezo umekuwa wa kasi zaidi tofauti na zamani. Inawawezesha wachezaji wa kisasa kufunga zaidi tofauti na zamani. Haishangazi kuona LeBron amefanya kile ambacho amefanya. Sidhani kama rekodi yake na ile ya Kane zinaweza kudumu kwa muda mrefu kama hizi ambazo wamezivunja.

Jaribu kutazama rekodi za Olimpiki za miaka ya sabini halafu tazama sasa hivi. Mtu aliyevunja rekodi ya dunia kwa dakika 18 leo rekodi yake inavunjwa kwa dakika tisa tu. Inakudhihirishia namna gani mwanadamu wa leo yupo fiti zaidi kuliko mwanadamu wa zamani. Hii ni katika soka na michezo tu sio katika masuala mengine.

Columnist: Mwanaspoti