Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NYUMA YA PAZIA: Iliandikwa mbinguni Messi atwae taji Doha

Messi Avunja Rekodi Ya Picha Iliyopendwa Zaidi Kwenye Instagram.png Nahodha wa Argentina, Lionel Messi

Mon, 26 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Ilikuwa kama hadithi tamu ya mapenzi ambayo mwandishi wake alimalizia vema. Mwandishi mahiri ambaye mstari wake wa mwisho ulisisimua na kila msomaji wa kitabu alikubali namna nukta ya mwisho ilivyomaliza kila kitu.

Hadithi ya Lionel Messi na Kombe la Dunia. Imeishia pazuri. Umekuwa ni mwisho uliosisimua. Messi ametwaa Kombe la Dunia. Baada ya filimbi ya mwisho kumalizika Jumapili iliyopita, sala za wengi zilishinda. Sala za kumuona Messi akitwaa Kombe la Dunia.

Ni kama hadithi nyingine zilizvyowahi kumalizika vema. Kwamba kuna wakati unamuona mtu shujaa na unaamini kwamba ushujaa wake utakamilika akishinda vita fulani. Wapo walioshinda mapema. Ndio hawa kina Kylian Mbape. Akiwa na miaka 19 tu alitwaa Kombe la Dunia pale Moscow.

Pele akiwa na miaka 17 tu alitwaa Kombe la Dunia pale Stockholm. Hawa kina Mbappe na Pele hadithi zao zilianzia mapema na waliendelea na kurasa nyingine. Waliofanya vema hapo katikati kina Zinedine Zidane, Ronaldo de Lima, Ronaldinho, Fabio Cannavaro na wengineo.

Halafu kuna huyu hapa, Lionel Andres Messi. Hadithi yake imekamilika patamu zaidi. Umri wa miaka 35 katika kile ambacho kinaonekana kwamba ni kombe lake la dunia la mwisho. Sijawahi kuona mashabiki wakisisimkwa na kutaka Messi achukue Kombe la Dunia kama hili hapa. Amecheza michuano mitano ya Kombe la Dunia, lakini hili mashabiki walitaka achukue.

Kwa nini? Ingekuwa zawadi yake kubwa zaidi ambayo angeweza kupata katika maisha yake ya soka baada ya kutuonyesha kila alichoweza kutuonyesha. Ingekuwa zawadi yake kubwa zaidi baada ya macho yetu kushuhudia kipaji kikubwa ambacho Mwenyezi Mungu ameshinda.

Unaweza kuwahesabu wachezaji ambao waliwahi kutwaa Kombe la Dunia wakiwa ni wachezaji wa kawaida tu. Wamejaa katika vikosi kibao vya nchi mbalimbali ambazo zimewahi kutwaa Kombe la Dunia. Kina Klebberson, Alain Boghosian, Thomas Lemar na wengineo. Kwa nini Messi asitunukiwe kombe hili? Hata kama angekuwa anaingia dakika tano za mwisho za kila mchezo lakini watu walitaka Messi atwae taji hili. Bahati nzuri ametwaa akiwa mhimili wa kikosi chenyewe. Kuna kila sababu tofauti ya kufurahi Messi kutwaa Kombe la Dunia.

Sababu kubwa na ya kwanza ni kwamba wakati mwingine wafahidhina walikuwa wanaamini Messi hawezi kulinganishwa na baadhi ya wakubwa waliopita kama Pele na Diego Maradona kwa sababu tu alikuwa hajatwaa Kombe la Dunia. Na sasa anaweza kuwekwa huko kwa sababu ametwaa taji hilo.

Kama watu wa Cristiano Ronaldo wangekuwa wanamkubali Messi wangeweza kujenga hoja kwamba Messi amewawakilisha vema watu wa kizazi hiki dhidi ya vizazi vilivyopita ambao waliamini Messi na Ronaldo hawawezi kuingia katika orodha ya wachezaji bora wa muda wote kwa sababu hawajatwaa Kombe la Dunia.

Kwa Messi binafsi kimekuwa kitu kizuri. Binafsi naamini Messi angeweza kuwa mchezaji bora wa muda wote mbele ya wale wanaotajwa. Kabla ya Jumapili usiku, alikuwa ametwaa kila kitu katika maisha yake ya soka. Alikuwa ametwaa mataji mengi binafsi na ya klabu alizocheza.

Endapo Messi asingetwaa Kombe la Dunia basi wale wote ambao wanaamini kwamba mchezaji bora wa muda wote lazima awe mchezaji aliyetwaa Kombe la Dunia wangeshikilia kwa nguvu hoja yao. Binafsi naiona hoja hafifu. Unaweza kudai kwamba Ronaldo sio mchezaji bora wa muda wote kwa sababu hajawahi kutwaa taji hilo?

Kuna wachezaji wengi mahiri ambao hawakupata bahati ya kuzaliwa katika mataifa makubwa kisoka lakini wamefanya mambo mengi makubwa katika ngazi ya klabu lakini pia walijaribu kila walivyoweza kuzisukuma timu zao za taifa lakini mambo yameshindikana kwa sababu walikuwa wamezungukwa na wachezaji wa kawaida tu.

Vipi kuhusu George Opong Weah na Liberia yake? Amewahi kuwa mwanasoka bora wa dunia lakini angefanya nini zaidi kulisukuma taifa kama Liberia kutwaa Kombe la Dunia achilia mbali tu kushiriki. Hata kushiriki Michuano ya Mataifa ya Afrika ilikuwa ngumu.

Ryan Giggs ndiye mwanasoka mwenye mataji mengi zaidi katika historia ya soka la Kiingereza lakini angefanya nini zaidi kulisukuma taifa la Wales kutwaa Kombe la Dunia? Ilikuwa ni ndoto ngumu. Kwa taarifa yako tu Giggs hajawahi kushiriki fainali hizo za Kombe la Dunia.

Hata hivyo, bahati kwa Messi amefanikiwa kuziba mdomo wale wote ambao walikuwa wanasubiri ashindwe kutwaa taji hilo ili wasimuingize katika orodha ya wachezaji bora wa muda wote katika kundi la kina Maradona na Pele.

Hata hivyo, pamoja na yote haya Messi ana bahati kubwa na michuano yenyewe. Ni kama vile Mungu aliamuandalia bahati yake. Jaribu kufikiria namna ambavyo alishindwa kuchukua Kombe la Dunia akiwa na wanasoka mahiri zaidi ya hawa.

Pale Maracana Brazil ilikuwa na kina Gonzalo Higuian, Sergio Aguero, Javier Mascherano, Ezequiel Lavezzi, Rodrigo Palacios na wengineo. Haikutwaa kitu. Na hawa walikuwa wanacheza katika timu mbalimbali kubwa barani Ulaya. Leo ametwaa kombe hili akiwa na wachezaji ambao ndio kwanza wanaanza kukuza majina yao. Ni wachache wana majina makubwa au wanacheza timu kubwa.

Wengi kwa sasa ndio wameanza kuhusishwa na timu kubwa zaidi. Bahati nyingine ambayo Mungu alipanga Messi atwae taji lenyewe ni mwenendo mzima wa Argentina katika michuano hii. Tazama walivyofungwa pambano la kwanza tu na vibonde Saudi Arabia. Tazama namna ambavyo Argentina ilivyopata penalti nyingi. Lakini tazama namna walivyokuwa wameshinda kwa mikwaju kuelekea katika pambano la fainali ambalo nalo lenyewe walishinda kwa penalti.

Lakini zaidi angalia ambavyo Kolo Randal Muani alivyokosa bao katika dakika za mwisho kabisa huku kipa Emilio Martinez akiucheza mpira ule. Kama Kolo angefunga, mpira ungeanzishwa na Waargentina na kumaliza hapo hapo. Kingekuwa kilio kikubwa kwa Messi. Iliandikwa iwe hadithi ya kusisimua ambayo ingeishinda kwa Messi kuchukua taji hilo mwishoni akiwa na umri wa miaka 35.

Argentina hii sidhani kama ilikuwa timu bora kuliko Wabrazili, Waingereza au Wafaransa. Lakini iliandikwa Messi lazima achukue Kombe la Dunia katika fainali yake ya mwisho pale Qatar na yametimia.

Columnist: Mwanaspoti