Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NYUMA YA PAZIA: Hatimaye tumeona mwisho wa Jacky Wheelchair

Jack Wilshereeee Kiungo wa zamani wa Gunners, Jack Wilshere

Mon, 18 Jul 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna muda hauwezi kupata kila unachokitamani maishani. Lakini pia kuna wakati hamuwezi kupeana kila mnachokitamani maishani. Ni kama hadithi ya Jack Wilshere. Lakini pia ni hadithi ya mimi na Jack Wilshere. Waingereza wanapenda kumuita Jack Wheelchair.

Mapema wiki hii Jack alituandikia ujumbe kwamba anastaafu soka. Nilijisikia vibaya. Katika umri wa miaka 30 tu. Jack ni miongoni mwa wanadamu waliobahatika kuzaliwa siku ya mwaka mpya. Alizaliwa Januari Mosi, 2002.

Akiwa na kipaji maridhawa miguuni, akili kichwani, dhamira moyoni, Jack alianza kupotea akiwa na miaka 24 tu. Labda tuseme miaka sita iliyopita. Kwa mimi shabiki wa Arsenal Jack anaingia katika kundi la mastaa ambao hawakuwahi kufika mwisho. Sijui kama nitaeleweka.

Namaanisha kwamba leo ghafla Kelvin De Bruyne akipotea tunaweza kujisemesha kwamba tuliuona mwisho wake. Hatutazamii kuona Kelvin akituonyesha kitu zaidi ya kile ambacho aliwahi kutuonyesha. Sawa anaweza kwamba hakuwahi kuwa kama Zinedine Zidane lakini amewahi kutuonyesha anapoweza kufika.

Jack ni kama kina Phillipe Coutinho. Amekatika ghafla. Yaani ni aina ya wachezaji ambao unajua kwamba bado walikuwa wanatarajiwa kufika katika safari ya mbali lakini wakashuka kituo kinachofuata. Kisa? Kulikuwa na mambo mengi nyuma ya pazia.

Wakati akitangaza kustaafu hii majuzi, Jack amekiri kwamba anaondoka huku akiamini kwamba alikuwa na mambo mengi ya kuufanyia mpira lakini haikuwezekana. Aliongea lugha ile ile ambayo ninaizungumza hapa

Jack aliandamwa na majeraha. Lakini hapo hapo alikuwa mchezaji msela kama ilivyokuwa kwa Wayne Rooney na baadhi mastaa wa Kiingereza. Kupigana disco huku akiwa amelewa chakari kwake halikuwa jambo la ajabu. Kukutwa anavuta sigara halikuwa jambo la ajabu.

Katika ubora wake, ulikuwa unamuona kabisa Jack akienda mbali. Kwa nyakati hizi angeweza asiwe Arsenal kwa sababu labda angeweza kuwa bora kuliko klabu yenyewe. Labda angekuwa Real Madrid au Barcelona au Manchester City. Katika ubora wao Barcelona, Jack aliwahi kucheza dhidi ya Xavi Hernandez na Andres Iniesta na bado akajitawala katika dimba.

Ilitajwa kama vile Pep Guardiola baadaye aliamua kumtaka lakini sikujua hadithi hii iliishia wapi.

Hata hivyo ilikuwa ni alama za nyakati kwamba alikuwa katika ubora wake. Ukiondoa Bukayo Saka nadhani Jack ndio mchezaji wa mwisho kutoka kutoka katika shule ya soka ya Arsenal kuelekea kuwa mchezaji wa kiwango cha dunia.

Kuanzia hapo Jack amejaribu kuzurura West Ham na Bournemouth bila ya mafanikio. Aibu ya mwisho ya majuzi ni pale alipokwenda klabu ya AGF ya Ligi Kuu ya Denmark. Wakati ule alipoanza hatukutazamia kwamba katika miaka 29 angekuwa akicheza katika Ligi Kuu ya Denmark. Sio Ufaransa, wala Italia, Ujerumani. Denmark!.

Lakini kama hatukutazamia hilo, basi sasa tuna mshangao zaidi. Katika umri wa miaka 30, Jack ni kocha wa Arsenal chini ya umri wa miaka 18. Inachekesha kidogo. Ukocha wake unaniachia maswali mawili ya msingi.

Swali la kwanza ni kama Jack atafuata nyayo za makocha wa kisasa. Siku hizi wachezaji wengi wa zamani wanatamani kuwa makocha pengine kuliko wakati mwingine wowote ule. Soka umekuwa mchezo unaovutia zaidi. Sayansi yake imekuwa na mvuto zaidi ikiongozwa na Pep Guardiola na Jurgen Klopp.

Halafu siku hizi ni kama vile kuna njia ya mkato kama ukiwa kocha mzuri. Kwa mfano, Pep alikuwa kocha wa vijana Barcelona. Alifanya mambo makubwa kiasi kwamba Barcelona walipoachana na Franck Rijkaard wakaamua kwenda kwa Pep. Sijui walimuamini nini lakini kilichofuata kilibakia kuwa historia. Mpaka leo. Lakini mtazame Mikel Arteta. Alipoachana na soka akaenda kukaa katika benchi la Pep kama msaidizi. Akasifika kuwa na akili nyingi. Arsenal wamempa timu na inaonekana anaifanyia mapinduzi makubwa. Walikosa kuingia Top Four katika siku ya mwisho ya msimu uliopita.

Labda Jack anataka kufuata njia hii. Inaweza isiwe kwa kuelekea katika timu yake Arsenal lakini akaibukia timu nyingine akafanya makubwa. Lakini kwanza itategemea atafanya mapinduzi katika kikosi cha chini ya umri wa miaka 18 pale Arsenal.

Kule makocha huwa wanapimwa vipi? Huwa kuna michuano mbalimbali ndani na nje ya England. Katika michuano kama hii ndipo ambapo Pep aliwaonyesha Barcelona kwamba anaweza kwenda katika timu ya wakubwa. Wengine huwa hawapitii njia hii.

Lakini kuna jambo la pili la kuchekesha kidogo kuhusu ukocha wa Jack. Kuna wachezaji ambao walikuwa wakorofi na masela wakati wanacheza soka. Unajaribu kujiuliza watakuwa makocha wa namna gani wakati wanafundisha soka. Wao ndio walikuwa sehemu ya matatizo katika timu lilipokuja suala la nidhamu.

Ni kama ambavyo Arsene Wenger alivyolazimika mara kadhaa kuitisha vikao wakati alipogombana Disko.

Ni kama ambavyo Sir Alex Ferguson alivyolazimika kupambana na nidhamu ya Wayne Rooney. Lakini leo hawa watovu wa nidhamu ndio wamekuwa makocha. Watakuwa makocha wa namna gani? Ni jambo linaloshangaza kidogo.

Ni kama kwa mtu anayeitwa Joe Barton. Alikuwa mkorofi kweli kweli wakati akiwa mchezaji. Leo ni kocha mahala fulani hivi. Sijui anashughulika vipi na wachezaji wakorofi katika kikosi chake. Ndivyo tunavyomsubiri Jack na ukocha wake kwa sasa.Vyovyote ilivyo kila la kheri kwa Jack. Sijali sana kuhusu ukocha wake kwa sababu ni kazi mpya. Kinachoniumiza jinsi alivyoniaga huku katika kazi ya uchezaji. Ni mchezaji ambaye sikuchoka kumsubiri.

labda siku moja angerudi lakini haikuwezekana. Nilisubiri halafu nikasubiri, kisha nikasubiri tena lakini hakuna kilichowezekana. Hatimaye tumeuona mwisho wake.

Columnist: Mwanaspoti