Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NYUMA YA PAZIA: Hakim Ziyech, shujaa wa udongo anayeyuka Morocco

Hakim Ziyech 22 Hakim Ziyech, shujaa wa udongo anayeyuka Morocco

Sun, 13 Feb 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Nyumbani ni wapi? Watu wamewahi kuulizana swali hili. Yalikuja majibu mengi lakini jibu ambalo lilitamba zaidi ni lile la Mwafalsafa maarufu wa zamani wa Warumi, Pliny the Elder aliyetuambia ‘Nyumbani ni pale ambapo moyo wako upo’.

Ndio, pale moyo wako ulipo. Unaweza kuwa katikati ya jiji la New York, lakini moyo wako ukawa unawaza Nzega Tabora. Hapa ina maana Nzega ndio nyumbani. New York ni makazi tu. Sidhani kama Pliny the Elder alitudanganya.

Lakini wakati mwingine unapata shaka kidogo. Mastaa wakubwa wa soka Ulaya huwa wanaelewa nyumbani ni wapi? Mastaa wa Kiafrika waliozaliwa Ulaya inawezekana wana hisia mbili. Kuna wale wenye hisia kwamba Ulaya ni kwao na kuna wale ambao wanaamini Afrika ni kwao.

Wote ambao huwa wanaamua kurudi na kuchezea timu za taifa za Afrika tunaamini kwamba wamechagua kuwa nyumbani ni Afrika. orodha ni ndefu lakini kwa sasa tuna mtu kama Achraf Hakimi. Amezaliwa Madrid lakini anaichezea Morocco.

Pierre-Emerick Aubamayeng, amezaliwa Laval, Ufaransa, lakini anacheza Gabon. Riyad Mahrez amezaliwa Sarcelles, Ufaransa ila anacheza Algeria. Kuna huyu hapa, Hakim Ziyech, amezaliwa Dronten, Uholanzi lakini anacheza Morocco.

Wote hao wangeweza kucheza katika timu za taifa ambazo wamezaliwa. Napata shaka kwamba huenda baadhi yao hawakukadiria kwamba wangeweza kuingia katika vikosi vya nchi walizozaliwa na ndio maana wakaamua kucheza timu za Afrika.

Majuzi Ziyech amenifikirisha sana. Kweli Morocco ni nyumbani? Sina uhakika sana. Nina uhakika kwamba amezaliwa na wazazi wa Morocco na hata Uholanzi amezungukwa na jamii ya Wamorocco. Lakini kweli Morocco ni kwao? Majibu anayo kocha wa timu ya taifa ya Morocco, Vahid Halilhodzic.

Mapema wiki hii Ziyech aliamua kustaafu soka la kimataifa. Kifupi ni kwamba amestaafu kuichezea timu ya taifa ya Morocco. Ziyech ana bifu kali na kocha huyu raia wa Bosnia. Kocha anadai kwamba Ziyech hajitumi katika kikosi cha Morocco na anajiona staa.

“Hataki kufanya mazoezi, hataki kucheza. Hayupo serious. Siwezi kumuomba arudi. Baada ya michuano ya Afcon miaka mitatu iliyopita yeye ndiye alikuwa mchezaji aliyekosolewa sana. Alikuwa anazomewa, msisahau hilo,” anasema Halilhodzic akimuelezea Ziyech.

“Kwa mara ya kwanza katika kazi yangu ya ukocha nimemuona mchezaji wa timu ya taifa ambaye hataki kucheza na anadanganya kuwa ameumia, huku vipimo vikionyesha kwamba yuko sawa. Sitavumilia,” alisema kocha huyu kwa hasira.

Hayo ni maelezo mafupi kati ya mechi ambayo kocha huyu mwenye miaka 69 alikuwa akimuelezea Ziyech. Ziyech mwenyewe anadai kwamba kila ambacho kocha alikuwa akisema ni uongo. Unajiuliza nani mkweli kati yao. Nani ana matatizo baina yao?

Kuna kocha ambaye hataki kufanya kazi na wachezaji wake walio bora? Sidhani. Huyu kocha amefanya kazi na Morocco tangu mwaka 2019. Kwa makocha wa timu ya taifa ni miaka mingi. Inaonekana Wamorocco wanamuamini.

Kitu kizuri kwake ni kwamba hata katika sakata hili dhidi ya Ziyech inaonekana kama vile Wamorocco wameamua kumuamini. Alipoamua kutomuita Ziyech katika kikosi ambacho kilikuwa kinakwenda Cameroon Wamorocco hawakusimama upande wa Ziyech.

Morocco walifika robo fainali na inaone-kana kama vile hawakuwa na matatizo na kocha na uamuzi wake wa kuachana na Ziyech. Lakini sasa Ziyech ameamua kustaafu soka huku akidai kwamba hatarudi tena katika kikosi cha timu ya taifa na uamuzi wake ni wa mwisho.

Alishindwa nini kumalizana na kocha wakati Machi 23 na Machi 29 watakuwa wakicheza na Congo katika mechi muhimu za mtoano za kufuzu Kombe la Dunia? Ina maana Ziyech hatamani kucheza Fainali za Kombe la Dunia?

Kinachoonekana hapa ni kwamba kujikisia kwake (ego) kupo juu kuliko hamu yake ya kucheza Kombe la Dunia. Au anaona kuwa kuichezea Morocco katika michuano hiyo ni kupoteza muda kwa sababu haiwezi kutwaa ubingwa wa michuano hiyo?

Lakini labda huenda Ziyech hachezi kwa moyo akiwa na Morocco kwa sababu mbili. Sababu ya kwanza ni ile ile ambayo tumeizoea kutoka kwa wachezaji wa Afrika ambao hawajitumi sana wakija Afrika kwa sababu wanalipwa mishahara mikubwa Ulaya na hawawezi kujiumiza huku kwetu.

Lakini hapo hapo inawezekana labda Ziyech anajuta kwa kuichezea Morocco. Labda alidhani kwamba angekosa nafasi kama angeamua kuichezea Uholanzi. Kumbuka kwamba tayari alishaichezea Uholanzi katika ngazi za soka la vijana na alianza kuichezea Morocco akiwa na miaka 20 mwaka 2015. Labda anajuta.

Vyovyote ilivyo ni kwamba Ziyech anajivua ushujaa. Kuna rafiki zangu Wamorocco huwa nawatembelea pale Ubelgiji. Mara zote walikuwa wanajivunia kuona Ziyech akiwa amechagua kuichezea Morocco na sio Ubelgiji. Mpaka sasa najiuliza wamesimama upande gani lakini kwa hiki kinachoendelea nadhani Ziyech atakuwa amewaangusha.

Mwaka 2008 nilikwenda Ghana kuhudhuria michuano kama hii ya Afcon na Marcel Dessaily alikuwa mmoja kati ya mastaa waliohudhuria michuano ile. Hata hivyo mara zote ambapo jina lake lilikuwa likitajwa mashabiki wa Ghana walionekana kuzomea.

Nilipouliza sababu walidai kwamba Desailly hakuwa na sababu ya kucheza Ufaransa na badala yake angecheza Ghana ambako amezaliwa. Hizi ndizo hisia ambazo wenzetu wanazo. Na hapana shaka ni hisia ambazo zilimfanya Ziyech awe shujaa alipoamua kuichezea Morocco badala ya Uholanzi.

Lakini kwa hiki ambacho kinaendelea hapana shaka kinamfanya ageuke kuwa shujaa wa udongo. Ameloa na sasa ameanza kumomonyoka. Unawezaje kulikacha Kombe la Dunia kwa sababu ya ugomvi na kocha? Lakini mbaya zaidi ishara ni mbaya kwake kwa sababu hata baada ya Morocco kutolewa hatua ya robo fainali na Misri pale Cameroon bado Wamorocco wamemkumbatia kocha wao.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz