Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NYUMA YA PAZIA: Coutinho, Rafiki ni bora kuliko mwanasesere

Cout Pic Data Coutinho, Rafiki ni bora kuliko mwanasesere

Mon, 24 Jan 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Tulisoma wakati tukiwa shule ya msingi kitabu kilichoitwa ‘Rafiki ni bora kuliko mwanasesere’. Unamjua mwanasesere? Ni mdoli. Afadhali uwe na rafiki kuliko kucheza na mwanasesere. Zipo nyakati ambazo mwanadamu anaamua kubaki kuwa mwanadamu.

Simu moja kutoka katika Jiji la Birmingham kwenda Barcelona ilitosha kumfanya mchezaji anayeitwa Philippe Coutinho kuamini kwamba rafiki ni bora kuliko mwanasesere. Kwa Coutinho wa sasa, kwa timu alizotembelea ilikuwa ni kama mtoto aliyekuwa amemshikilia mwanasesere.

Lakini mtu anayeitwa Steve Gerrard aliponyanyua simu yake ya kiganjani na kubonyeza namba za Coutinho ilikuwa wazi kwamba nyota huyo wa Brazili alikuwa na uhakika kwamba anaongea na rafiki yake. Ilikuwa afadhali kuliko kuukumbatia Mwanasesere.

Nani anamhitaji mwenzake? Aston Villa inamuhitaji sana Coutinho au Coutinho anaiihitaji sana Aston Villa? Ukweli ni kwamba Coutinho aliihitaji zaidi Aston Villa. Alimuhitaji zaidi Steven Gerrard katika nyakati. Anaweza kuwa aliwahi kuwa mchezaji mkubwa, inaweza kuwa timu zake tatu alizocheza mara ya mwisho zilikuwa zinampa nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa, lakini katika hali halisi kwa sasa Coutinho hastahili tena huko.

Usibishe sana. Uhamisho wake wa kwenda Barcelona ulitibua kila kitu katika maisha yake ya soka. Baadaye akaazimwa Ujerumani. Hata hivyo Bayern Munich walimbwaga na kumrudisha tena Catalunya. Kuanzia hapo nani alimtaka Coutinho?

Ukweli ni kwamba Coutinho alikuwa anapatikana lakini alimtaka? Tulikuwa tunasikia uvumi tu. Mara Arsenal, mara Spurs, mara Juve. Ukweli ni kwamba sidhani kama walikuwa wanamtaka. Kama kweli walikuwa wanamtaka wangemkosaje halafu Villa impate?

Villa haina mishahara mikubwa kuliko Arsenal, Juve wala PSG. Ukweli ni kwamba hizi timu hazikumtaka Coutinho. Na kitu kibaya zaidi ni kwamba Xavi Hernandez alikuwa hamtaki Coutinho. Nilishangaa kidogo. Nilidhani Coutinho angeweza kuwa aina ya mchezaji ambaye Xavi angemtaka kwa ajili ya kurudisha Tiktak pale Camp Nou. Haikuwa hivyo.

Umbo lake fupi, mnyumbulifu, lakini bado Xavi hamtaki. Hawa ni aina ya wachezaji wa kucheza pasi fupifupi maridhawa ambazo Xavi alikuwa anazifanya pale Nou Camp pamoja na timu ya taifa ya Hispania. Lakini bado hamtaki licha ya kwamba katika kikosi chake ana wachezajj wa kawaida tu.

Ni simu ya Gerrard ndio ambayo imebadilisha upepo wa Coutinho hata kama amehamia kwa uhamisho wa mkopo. Gerrard ni rafiki yake wa karibu. Lakini Coutinho kwa sasa alihitaji timu kama Villa kujaribu kurudisha makali yake. Na bahati nzuri pia alimhitaji kocha kama Gerrard amrudishie makali yake.

Ndani ya Villa, Coutinho atakuwa samaki mkubwa. Atacheza bila ya presha. Akikosea sawa, asipokosea sawa. Ndani ya Villa timu itamzunguka. Atarudisha kujiamini kwa sababu kwanza mashabiki na kila mtu atakuwa nyuma yake akiamini kwamba yeye ni shujaa na ataibeba timu.

Kila kitu kilikwenda sawa katika pambano lake la kwanza dhidi ya Manchester United. Aliondoka uwanjani akiwa shujaa. Aliingia dakika chache akafanya mabadiliko makubwa uwanjani na Villa ikaambulia sare. Swali la msingi ni kujiuliza kama alichokifanya kitaendelea.

Unapocheza Bayern Munich ni rahisi tu kuibuka shujaa wiki hii lakini ukaanzia benchi mechi ijayo. Kwa Villa ni wazi kwamba Gerrard atamuwekea mkono begani na kumwambia kwamba anamuamini. Ataanza tu. Jukumu litabakia juu yake. Juni atatimiza miaka 30. Ni wakati ambapo pia mkataba wake wa mkopo na Villa utakuwa unamalizika. Swali la kujiuliza ni kama atakuwa amezishawishi timu kubwa kumpa mkataba wa kudumu na hivyo kurudi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa.

Lakini kama sio timu kubwa, basi tunasubiri kuona kama atakuwa amemshawishi rafiki yake Gerrard kumpa mkataba wa kudumu. Mpira upo kwake. Tofauti yake na Wabrazili wengine ni kwamba hata wakati huu anapokuwa amekaribia miaka 30, Coutinho bado yupo katika umbo lile lile.

Kina Ronaldo, Ronaldinho, Adriano na wengine walianza kuwa tipwatipwa, yeye bado yupo katika shepu yake. Ataweza kurudi katika makali? Ni jambo gumu lakini mwanamuziki maarufu wa muziki wa kizazi kipya aliwahi kusema “ni kazi ngumu lakini lazima mtu aifanye”.

Ni wachezaji wachache ambao waliwahi kuzama kisha wakaibuka. Wapo ambapo wanaibuka katika Ligi nyingine za kawaida lakini kuibukia katika Ligi Kuu kubwa badala ya kuzama katika ligi kubwa huwa ni kitu kigumu. Waulize kina Fernando Torres.

Hata hivyo ninachowapendea rafiki zangu Wabrazili ni kwamba pamoja na yote haya maisha yakiwashinda pale Ulaya utasikia wapo kwao. Utasikia tu Coutinho yupo Palmeiras au Botafogo ama Corinthians. Hiki ni kitu cha mwisho wanachoweza kufanya. Bahati nzuri kwao kuna raha zaidi. Ni shida tu ndizo ambazo zinawapeleka Ulaya. Kwao kuna fukwe za kusisimua, kuna ngoma ya samba, kuna kila kitu cha kustarehe ambacho maisha ya mwanadamu yanahitaji.

Ukiona hii miezi sita imekwenda kombo kwa Coutinho pale Villa kiasi kwamba wao wasimhitaji, Barcelona wasimhitaji na klabu nyingine zisimhitaji, basi usishangae kusikia Coutinho yupo Sao Paulo kule kwao Brazil.

Vinginevyo kwa sasa tuone ataishi vipi na rafiki yake. Walituambia rafiki ni bora kuliko mwanasesere. Coutinho amehangaika sana miaka ya katikati hapa. Acha atulie kidogo kwa Gerrard. Huenda mambo yakabadilika. Dalili zimeanza kuonekana dhidi ya Manchester United.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz