Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NYUMA YA PAZIA: Bamidele Alli ameumaliza mwendo mapema

Skysports Dele Alli Everton 5670370 Dele Alli

Mon, 22 Aug 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Julai ndani ya mwaka 2017, mtalii mmoja aliyefika katika visiwa vya kifahari Myknos pale Ugiriki aliondolewa akiwa ‘amezimika’. Alipelekwa chumbani kwake. Mpenzi wake alimbebea viatu vyake. Sijui aliamka lini. Labda kesho au keshokutwa.

Huwa inatokea. Maisha yanataka nini zaidi? Kijana mdogo. Una pesa. Una kipaji una kila kitu. Bamidele Alli. Huyu ndiye mtalii mwenyewe ambaye alizimika siku hiyo. Wakati huo alikuwa ameishika Tottenham Spurs mkononi. Wakati huo alikuwa anahusishwa na Real Madrid, mara Manchester United, mara Liverpool.

Kando yake walikuwepo kina Christian Erikssen, Son Heung-Min na Harry Kane. Dele alikuwa moto mno. Leo zile hadithi za kwenda Real Madrid zimekufa. Ana miaka 26 tu anakwenda zake kwa mkopo Uturuki. Jinsi ambavyo maisha yanakwenda kasi. Erikssen yupo Manchester United, Son na Kane wapo Tottenham.

Dele anaondoka zake. Nadhani anaondoka katika soka mdogo mdogo. Safari yake ya kuondoka haikuanzia Tottenham moja kwa moja. Alipitia Everton. Timu ambayo imechoka na ipo hoi. Ameshindwa kujihakikishia nafasi katika kikosi cha Everton ambacho kwa sasa kinaweza kuwa kibovu kuliko vikosi vyote vya klabu hiyo tangu kuanzishwa kwa Ligi Kuu.

Awali ilidhaniwa kwamba Dele angeweza kuibuka Everton. Labda angerudisha uwezo wake wa kujiamini. Hata hivyo amezidi kudidimia. Inatia huzuni. Na sasa anakwenda katika Ligi ambayo haipo hata katika tano bora za Ligi Kuu barani Ulaya.

Nini kimemtokea? Sijui. Naishia kuwa mtabiri tu. Natabiri tu kwa namna ambavyo maisha ya vijana wa Kiingereza yalivyo basi huenda Dele akaangukia kuwa mhanga wa tabia zao. Mambo kama yale ya Myknos ndio maisha yao ya kila siku, hasa wanapopata pesa nyingi na umaarufu mkubwa.

Kina Jack Wilshere, Wayne Rooney, Steven Gerrard na wengineo haya ndio maisha yao. Jack mara kadhaa alijikuta akipigana katika klabu za usiku. Arsene Wenger alikuwa ana wakati mgumu. Gerrard alijikuta akitolewa selo mara kadhaa na mkewe Alex kutokana na vurugu zake klabu za usiku.

Rooney ndio balaa. Mara ngapi tumesikia amelewa na kupigana au amekutwa katika vyumba vya wanawake akiwa amelewa chakari. Katika eneo hilo hilo la Myknos Ugiriki, Harry Maguire ameacha kesi ya ugomvi. Alikwenda likizo mwaka jana akalewa akaanzisha vurugu.

Vipi kuhusu Rio Ferdinand. Vipi kuhusu John Terry. Wote walikuwa na matatizo makubwa ya kilevi nje ya uwanja. Rafiki yangu Rio aliwahi kukwepa kufanyiwa vipimo vya kutumia dawa za kuongeza nguvu michezoni. Alifungiwa miezi kadhaa. Inasemekana kuna kitu alitumia.

Ni wachezaji wachache wa Kiingereza ambao hawapo hivyo. Mfano ni kama David Beckham. Lakini pia Harry Kane anaonekana sio msela. Hawa wengine usiwaamini sana. Maisha yao yanakuwa ya ajabu ajabu kweli kweli.

Katika maisha haya kuna wachache ambao wanamudu kuendelea kuishi kwa uweledi baada ya kinywaji. Lakini hawa kina Dele ndio ambao huwa wanajikuta wamezidisha. Sio kwa bahati mbaya kwa mchezaji aliyekuwa na kipaji kikubwa kukwama akiwa na miaka 26 huku akiwa hasumbuliwi na majeraha.

Dele wa leo anashindwa hata kutuliza mpira. Sio kitu cha kawaida. Hata ukimtazama nuru yake anaonekana hayupo sawa. Ingekuwa Afrika tungeweza kusema amerogwa, lakini kwa wenzetu maisha yao hayapo hivyo. Inabidi ujiheshimu zaidi hata kama una maisha mengine.

Nadhani tumeuona mwisho wake. Nadhani ameumaliza mwendo. Ni wachezaji wachache wanaoweza kwenda katika nchi kama Uturuki halafu wakarudi salama. Sikumbuki mchezaji ambaye alikwenda Uturuki akitokea England ambaye alirudi tena kukiwasha. Labda Nicolas Anelka.

Vinginevyo mtu kama Mesut Ozil anazidi kuzama. Mtoto wetu wa nyumbani, Mbwana Samatta alipokwenda Uturuki mambo yakawa mabaya zaidi na sasa amerudi Genk, klabu ambayo ilimpokea Ulaya. Vipi kuhusu kipa wa Liverpool, Karius? Alipofanya uzembe katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akapelekwa Uturuki. Hajawahi kuibuka tena.

Na sasa ni zamu ya Dele. Sidhani kama ataibuka. Sehemu ambayo alipaswa kuibuka ni Everton. Kama Everton hii inakushinda sijui ni wapi angeweza kuibuka. Mwisho wa siku hawa vijana baadae huwa wanakuja kuandika vitabu na kuandika mambo mengi ya nyuma ya pazia.

Hapo ndipo Dele atakapojitokeza hadharani na kukiri kwamba katika nyakati hizi alikuwa anasumbuliwa na ulevi, kucheza kamari na mengineyo. Bahati mbaya tu ni kwamba katika nyakati hizi hawawezi kujitokeza hadharani kwa sababu bado wanacheza.

Vinginevyo stori ya Dele Alli inasikitisha. Nyakati hizi alipaswa kuwa juu ya watu kama kina Kelvin De Bruyne lakini ndio hivyo tena. Maisha yake ya soka yanakwenda chini wakati wenzake wanakwenda juu na wapo katika vilele vya ubora wao. Leo angekuwa anachukua nafasi ya Luka Modric pale Santiago Bernabeu lakini haikuwezekana. Angekuwa ni mchezaji kutoka Afrika tungeweza kudai kwamba umri umemuumbua, lakini Dele amezaliwa London. Ni mtoto wa kiswahili kwa maana ya kwamba Baba yake ni Mnigeria huku Mama yake akiwa mzungu lakini ukweli ni amejiangusha mwenyewe. Sio umri.

Columnist: Mwanaspoti