Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NYUMA YA PAZIA: Arteta, naandika nafuta halafu naandika tena

Nyuma Pic Data Arteta, naandika nafuta halafu naandika tena

Sun, 20 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Kwamba Arsenal imerudi. Kwamba Mikel Arteta anajua anachokifanya. Kwamba Thomas Partey ni Patrick Vieira mpya. Kwamba Arsenal ni Manchester City mpya. Kwamba Arsenal ni Liverpool mpya. Kwamba inawezekana haya yote niliyoandika ni ujinga. Wakati utatuambia.

Chukua msimamo wa ligi tazama nafasi ya Arsenal. Inashika nafasi ya nne. Ilianza ligi kwa kufungwa mechi tatu mfululizo. Dhidi ya Chelsea - dhidi ya Manchester City na dhidi ya Brentford. Ikaonekana Arteta hafai katika nafasi yake.

Baada ya kufungwa kijinga mechi hizi tatu na kisha hapo katikati timu ikayumbayumba hatimaye timu ikapata mwelekeo ambao wamedumu nao hadi leo. Imedumu nao hadi Jumatano usiku licha ya kufungwa na Liverpool.

Na hata tukiweka kiwango cha kupima mechi zao tatu za mwanzo ilizofungwa na jinsi ilivyocheza marudiano ya mechi hizi. Mechi za marudiano Manchester City ikafukuza vivuli vya wachezaji wa Arsenal. Bahati mbaya Gabriel alipewa kadi nyekundu na ikabadilisha mechi. Haijawahi kuonekana mechi ambayo Man City ilikimbizwa chini ya Pep Guardiola kama ile.

Ikaja mechi ya Brentford na ilitamani mpira uishe. Ilikimbizwa dakika zote. Mechi ya Chelsea haijafika, lakini itasisimua mashabiki. Kinachoonekana ni kama vile Mikel Arteta ameanza kututia katika majaribu. Ameibadili Arsenal kwa kiasi kikubwa.

Kuanzia pale ambapo tulitamani afukuzwe na timu iende ama kwa Antonio Conte au kocha mwingine yeyote mwenye uwezo hadi leo ambapo Arsenal inaonekana kama vile imekaribia kuingia Top Four kwa mara ya kwanza baada ya miaka sita hivi, inaonekana kama vile Arteta anajua anachokifanya.

Hapo katikati Pep Guardiola alipotuambia kwamba Arteta ndiye alikuwa mtu pekee anayeweza kuirudishia heshima yake hatukuamini sana. Tuliamini kwamba labda kwa sababu alikuwa kijana wake, rafiki yake na pia mshkaji wake kutoka Hispania.

Lakini sasa Arteta anatuweka majaribuni. Amefanya kazi nzuri isiyotarajiwa mpaka wakati huu tukikaribia kufika Aprili. Kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi Arsenal inacheza kama timu yenye mamlaka kamili uwanjani.

Inakaa na mpira, inapasiana kwa haraka, inashambulia, lakini zaidi ni kwamba inafanya kile ambacho soka la kisasa linahitaji. Inakaba kwa nidhamu na kwa pamoja. Timu zote bora katika soka la England kwa sasa, Man City na Liverpool hii ndio nguvu yao kubwa. Kuonyesha uwezo mkubwa wakati hawana mpira.

Arsenal wa leo inaonekana kuwa bora wakati haina mpira. Wachezaji wengi wanajua wawe wapi na kwa wakati gani wakati hawana mpira. Ni tofauti na enzi za rafiki yangu, Per Metersacker. Ni tofauti na zama za Arsene Wenger ambaye isingekuwa ajabu kwa Arsenal kufungwa na timu kubwa mabao sita, nane au matano.

Katika hili inaonekana Arteta ametumia akili zaidi. Amepunguza umri wa wachezaji kikosini. Staili hii ya soka inahitaji vijana wenye nguvu. Mastaa wa leo wa Arsenal wana miaka 19, 20, 22, 24. Kaka zao wakubwa ni Alexandre Lacazette na Granit Xhaka. Labda na Partey kama amedanganya umri zaidi.

Ameondokana na Pierre-Emerick Aubameyang. Tatizo halikuwa nidhamu pekee, lakini staa huyu wa Gabon alikuwa haingii vyema katika mfumo wake. Achilia mbali mabao, lakini Aubameyang alikuwa haipi Arsenal mchango mwingine. Sio mkabaji, lakini pia sio muunganishaji timu kama ambavyo Lacazette anafanya.

Unaweza kuona namna gani Arsenal imezidi kuimarika zaidi baada ya Auba kuondoka. Imeimarika kimfumo na wakati mwingine unajiuliza ni namna gani Arsenal imeweza kusonga mbele bila ya kuwa na mshambuliaji mwingine hatari kama yeye. Wanatengeneza mabao mengi kutoka katika nafasi tofauti.

Kuna maswali mawili ya msingi. Unaweza kujikuta unaandika kumsifu Arteta, lakini ghafla unafuta. Muda ni jambo zuri kabla haujaandika sana kumsifu. Arsenal ipo fomu au imerudisha hadhi yao? Hivi ni vitu viwili tofauti.

Liverpool na Man City hazipo katika fomu, bali zipo katika ubora wao. Zinaweza kufungwa leo, lakini huku zikitawala mechi au zikitegemewa kutamba mechi ijayo na ijayo. Hii ndio maana ya ubora uliokamilika.

Arteta anahitajika kujua hili. Kwamba anaweza kumaliza Top Four - sawa. Lakini anaweza kuifanya timu yake icheze kama hivi kila wikiendi kwa kipindi cha miaka minne au mitano kama ambavyo Manchester City na Liverpool zinafanya.

Suala la fomu hata kina Wolves huwa wanakuwa fomu. Suala la ubora wa kudumu ndilo suala gumu. Hata kina Ole Gunnar Solskjaer walikuwa wanamfunga Manchester City katika zama hizi za Pep Guardiola lakini leo Man City wako wapi na Solskjaer yuko wapi?

Arteta akitaka tuandike jina lake aendeleze kiwango hiki hiki msimu ujao. Hapo ndipo tutakapoamini kwamba ameirudisha Arsenal inapostahili baada ya vilio vingi tangu Wenger aipoteze dira ya timu kisha akaja Unai Emery.

Mchakato wake unakwenda poa, ingawa wengi hatukumiani hapo mwanzoni. Labda kwa sasa tunaweza kumsikiliza kile ambacho Pep alisema. Pia tutampima zaidi pale ambapo atapewa pesa za kununua wachezaji wa maana.

Auba ameondoka na hakuna mchezaji aliyechukua nafasi yake. Lacazette anamaliza mkataba wake na ni ngumu kwa mchezaji wa aina yake kuondoka wakati anaweza kwenda kuchukua pesa nyingi kama mchezaji huru kwingineko.

Eddie Nketiah naye anamaliza mkataba wake. Ni kinda mzuri, lakini sio wa hadhi ya Arsenal. Anaweza kuondoka mwishoni mwa msimu kwa sababu ana kila sababu ya kufanya hivyo. Kwanza hapati nafasi mara nyingi.

Arteta atakuwa katika nafasi ya kununua washambuliaji wawili na kuimarisha maeneo mengine. Alexander Isak wa Real Sociedad? Mzuri na atawasaidia. Patrick Schick wa Bayer Leverkusen? Naye mzuri. Najua hawawezi kumpata Erling Haaland.

Baada ya hapo, na katika msimu wa tatu wa Arteta tunaweza kujua mwelekeo sahihi zaidi wa Arsenal na Arteta. Tutapaswa kutambua kwamba gari limewaka au ilikuwa katika fomu tu msimu huu. Binafsi naamini kwamba gari lao litakuwa limewaka.

Wanaomfahamu Arteta wanadai kwamba alibaki katika mbinu zake anazoziamini hata kama timu ilikuwa haifanyi vizuri.

Ndicho hikihiki wanachofanya kina Pep na Jurgen Klopp. Huenda wachezaji wakawa wamemuelewa Arteta na labda watakaokuja nao pia watakuwa wamemuelewa vyema.

Kwa sasa tunaandika na kufuta halafu tunaandika tena. Nusu ya moyo unaamini, nusu ya moyo bado hauamini sawa sawa kama inavyotakiwa.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz