Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NYUMA YA PAZIA: Afadhali wiki ya mauzauza barani Afrika imepita

Soccer Afrikaa Afadhali wiki ya mauzauza barani Afrika imepita

Sun, 3 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Kama hautakusanya matukio unaweza kudhani ilikuwa wiki ya kawaida. Hapana. Ilikuwa wiki ya mauzauza kwa soka la Afrika. Hili soka lina safari ndefu. Ni kama mwanadamu aliyeambiwa atembee kilomita 5,908 kwa miguu.

Afrika walikuwa wanatafuta wawakilishi watano ambao watatupeleka katika Fainali za Kombe la Dunia pale Qatar baadaye mwaka huu. Nianzie wapi? Hata sifahamu vema. Labda nianzie suala la ubaguzi wa rangi. Bara limeendelea kuwa moja, lakini watu wake wana hisia tofauti.

Nani Mwafrika kamili? Nani hasa? Nilitaka timu imara za Afrika zipite ili twende Kombe la Dunia likiwa na wawakilishi watano. Hata hivyo baadaye nikagundua kwamba kuna wenzangu walikuwa wanataka wawakilishi halisi wa Bara la Afrika.

Baadaye nikagundua kwamba kuna wenzetu wanaamini kuna baadhi ya timu zingepita basi wangekuwa wanawakilisha Afrika. Kwamba Misri, Algeria, Morocco na Tunisia wakipita basi huenda wanawakilisha Asia kwa sababu ni Waarabu.

Sijui ubaguzi utakwisha lini. Mtu mweupe anambagua mtu mweusi, na mtu mweusi anajibu mapigo. Hata hivyo wakati mtu mweusi anapojibu mapigo huwa hajui kama anajibu mapigo. Ndicho kilichotokea wiki hii. Waarabu waliokuwa wanacheza na watu weusi waliombewa wafungwe.

Lakini ebu subiri kwanza. Sijawahi kuutazama mpira kwa jicho hilo. Sijawahi kuwa mbaguzi. Sipendi kuwa mbaguzi. Nilitaka Morocco aifunge DR Congo. Sababu? Morocco ni imara na anaweza kutuwakilisha vema Qatar.

Hivi kweli DR Congo licha ya kuwa majirani zetu ndio wakatuwakilishe Qatar? Kwa lipi hasa? Mpira hauchezwi chumbani. Nilichowaza ndicho kilichotokea. Kama DR Congo imelazimisha sare nyumbani ikapigwa ugenini na Morocco angeweza kuhimili vishindo vya kina Argentina, Ujerumani na Ufaransa? Sio kweli.

Nilitaka Algeria amfunge Cameroon kwa sababu miaka ya karibuni kina Riyad Mahrez wameonekana kuwa imara zaidi kuliko Cameroon ambayo imebaki jina tu. Hata hivyo mambo hayakwenda sawa kwangu kwa sababu kadri mechi ilivyokuwa inaendelea ndivyo ilivyokuwa inajidhihirisha kwamba nguvu ya Algeria imeanza kupungua kama tulivyoona Afcon.

Acha Cameroon aende. Sio kwa sababu ya rangi zao bali wameonekana kuimarika kuliko Afcon. Algeria inabidi wajipange upya. Baada ya ile fainali waliyotwaa ubingwa wa Afcon dhidi ya Senegal nadhani makali yao yamepungua. Acha wakajipange.

Nilipata wakati mgumu wa kujua nani aende kati ya Tunisia au Mali. Hata hivyo acha iwe kama ilivyokuwa. Mali ina wachezaji mmoja mmoja wanaofanya vizuri Ulaya lakini bado hawajakaa kitimu kama Tunisia, japo Tunisia yenyewe nayo siiamini sana.

Matarajio yangu ya kutamani Senegal apite dhidi ya Misri yalitokana na ukweli ambao hata wengine walitamani hivyo kwa sababu za kisoka. Senegal ipo juu kwa sasa, kitimu na kwa mchezaji mmoja mmoja. Hakukuwa na ubaguzi katika hili.

Tukiachana na mauzauza haya ya ubaguzi wa rangi kulikuwa na vioja vingi kando yake. Soka la Afrika bwana! Rafiki zangu Waghana waliwawekea Wanigeria ngazi za ajabu za kushukia katika ndege wakati walipofika uwanja wa ndege pale Ghana.

Ilikuwa aibu, lakini ndio mauzauza yetu. Hauwezi kuona mambo haya popote kwingineko. Ghana walipokwenda Nigeria katika mechi ya marudiano rafiki zangu Nigeria wakajibu mapigo kwa kuwazimia taa Ghana wakiwa mazoezini. Hauwezi kuona popote kwingine katika soka. Ni utalii wa ndani wa soka la Afrika.

Kilichotokea baadaye kimeniacha mdomo wazi. Nigeria walishindwa kufuzu baada ya kutoka sare ya 1-1 na Ghana. Mwisho wa mchezo mashabiki wa Nigeria waliingia uwanjani na kufanya vurugu kubwa ambazo zilisababisha kifo cha daktari mmoja kutoka Zambia ambaye aliyeuliwa na CAF kusimamia shughuli muhimu katika mechi hiyo.

Kuna maswali. Zilikuwa hasira dhidi ya mwamuzi? Timu yao Nigeria? Wageni Ghana au? Sikuona hasira zikiwa zimelenga popote pale. Yaani basi tu waliamua kufanya mauzauza kwa kuingia uwanjani na kufanya vurugu. Ujinga ulioje.

Lakini ni katika jambo hili la Ghana kufuzu dhidi ya Nigeria ndipo tunapopata maajabu mengine. Nilitamani Nigeria washinde na watuwakilishe mbele ya Ghana kwa sababu naamini Wanigeria wana wachezaji wakubwa kwa sasa. Kuliko Ghana.

Hata hivyo kwa jinsi ambavyo mpira wa Afrika ulivyokuwa hauna adabu basi amesonga mbele Ghana ambaye sidhani kama atakuwa na afya kubwa katika Kombe la Dunia kuliko kama Nigeria kama angekwenda. Huu ndio ukweli halisi.

Kule Dakar kuna hili jambo la Mohamed Salah kukosa kwenda Kombe la Dunia. Licha ya kwamba tulitamani Senegal asonge mbele, lakini tulitamani Salah aende katika fainali hizo. Mambo yote mawili yasingewezekana kwa wakati mmoja na sasa tupite athari zake.

Salah anaonekana kuwa mbele ya Sadio Mane katika soka la wazungu. Anapigiwa chapuo kuwania tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia. Kuna uwezekano mkubwa pia michuano ya Kombe la Dunia ikachangia kwa kiasi fulani kutuletea Mwanasoka Bora wa Dunia.

Salah atajikuta nje ya mbio. Bado ana nafasi ya kutwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya, ana nafasi ya kutwaa Ligi Kuu ya England na FA. Lakini kama akiibuka mwendawazimu ambaye atawaka vilivyo katika Kombe la Dunia pale Qatar basi huenda tukasahau mambo ambayo Salah ameyafanya Mei, mwaka huu.

Labda angeenda Qatar, hata kama Misri isingefika mbali kisha akafunga walau mabao manne huenda angezidi kushindilia nafasi yake katika udongo. Lakini sasa Salah hatakuwepo Qatar na kumbuka kwamba mwaka huu alishindwa kutwaa Afcon akiwa na Misri. Anaitegemea Liverpool tu.

Pia nataka kuona hatima ya Hakim Ziyech na timu ya Morocco. Haelewani na kocha wake. Hakuna mchezaji asiyependa kucheza Kombe la Dunia. Je Ziyech ataomba radhi na kurudi kikosini? Je Wamorocco watashinikiza Ziyech aitwe? Yote haya ni magumu kwa sababu kocha ana msimamo na anapendwa.

Pale Ghana kuna beki wao mahiri anaitwa Mohamed Salisu. Kwa sasa nadhani utakuwa unamuona katika kikosi cha timu ya Southampton pale Ligi Kuu ya England. Salisu ameigomea timu ya taifa ya Ghana mara kadhaa akidai kwamba anataka kujikita kwanza katika ngazi ya klabu.

Mpaka wakati huu Ghana inafuzu kwenda Qatar hajaichezea Ghana. Je ataitwa katika kikosi cha Ghana kwa ajili ya fainali hizo? Hatujui. Kesi ya Salisu inachekesha sana kwa sababu amezaliwa Ghana, amekulia Ghana, wazazi wote ni Waghana lakini ameidengulia Ghana tangu awe staa. Waghana watamkubali katika timu wakati huu wa neema? Wachezaji wenzake waliopambana kuipata tiketi watamkubali? Ndicho ninachosubiri kuona.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz