Waswahili wana msemo wao kwamba; ‘Unaweza kuwaruhusu ndege kuruka juu ya kichwa chako lakini si vema kuwaruhusu kujenga kiota juu ya kichwa chako.’ Nimeukumbuka huu msemo kufuatia taarifa za kimtandao ambazo zimezagaa sehemu mbalimbali duniani na zaidi huku kwetu zikitoa takwimu za mpira wa miguu.
Uhuru wa habari na maendeleo ya kiteknolojia umefungua akili ya mwanadamu kuona au kupata taarifa mbalimbali za mambo yanayoendelea katika jamii yake. Lakini inahitaji maarifa binafsi kujua habari gani ya kukumbatia kichwani na kuamini na ipi ya kuachia, kama ndege warukao angani, habari zitazidi kutoka magazetini, redio, runinga, mitandao ya intaneti na kadhalika bila kujali ni za kweli au si za kweli, zinakuhusu au hazikuhusu maana ni jiwe linalotupwa gizani bila kujali litambonda mwenye nguvu au mnyonge, mtoto au mtu mzima.
Bahati mbaya sana, msambao wa habari si kama bidhaa zinazosambazwa madukani ambako utaambiwa na shirika la viwango (kama TBS hapa kwetu), kwamba bidhaa hii ni halali au ni haramu.
Mara nyingi katika michezo tumezoea kupata taarifa za matukio kuliko takwimu si wapenzi wengi wa michezo wanaopenda kufuatilia takwimu labda za mwanariadha mwenye kasi zaidi au bondia aliyeshinda mapambano mengi kwa knockout; watu wanapenda kujua nani kashinda marathoni au mita mia moja na nani kampiga nani.
Kama nilivyosema hapo awali, maendeleo ya nyenzo za upashanaji habari yamepanua pia wigo wa habari ambazo zinawafikia walaji kwa kuwa vyanzo vya habari vimeongezeka maradufu.
Kwenye mpira wa miguu tulizoea taarifa na takwimu zinatolewa na FIFA, UEFA, CAF, FAT/TFF na nyingine za namna hiyo.
Taarifa hizo, mfano za ubora wa mataifa (Fifa nations rankings), zilitunzwa na kutolewa na FIFA zikituonyesha kupanda na kushuka kwa mataifa kutegemea matokeo yao ya hivi karibuni.
Hata takwimu za CAF na vyama vya mabara viliendelea katika mstari wa FIFA, hata wakati huo kulikuwa na redio televisheni na majarida yakitoa taarifa na takwimu lakini mwisho wa siku neno la Fifa lilikuwa la mwisho.
Hivi karibuni mtandao unaoitwa Shirikisho la Takwimu na Historia ya Mpira wa Miguu (IFFHS), lilitoa takwimu la klabu na ligi duniani. Kuna klabu zilijulikana kwamba viko juu sana duniani, ghafla vikashushwa na takwimu hizi, kuna ligi zilionekana kuwa juu duniani, ghafla zikashushwa na kinyume chake.
Hili lilisababisha watu wengi kushtushwa na mafanikio au muanguko ambao hawakuutarajia, takwimu hizi zilikuja tofauti na tulizozoea za FIFA.
Mfano ni pale unapoambiwa ligi bora duniani iko nje ya Ulaya na klabu bora duniani iko nje ya Ulaya.
Si kwamba hili haliwezekani, linawezekana ila halijazoeleka na ukokotozi pia namna hizi takwimu zilivyopatikana haujaeleweka kwa wadau walio wengi. Hata wale walioelewa wanapata mkanganyiko kama ambavyo mtoto anaweza kusoma shule lakini matokeo yake yakatangazwa na asasi tofauti huku kila moja ikiwa na vigezo vyake.
Taasisi ya IFHSS ni taasisi binafsi isiyofungamana na mamlaka yoyote ya mpira wa miguu, ilianzishwa Leipzig Ujerumani na mtu aliyejulikana kama Alfred Poge mwaka 1984 na kuweka makao huko Abu Dhabi, kisha Bonn Ujerumani na sasa IFFHS ina makao yake Zurich, Switzerland. Taasisi hii ilianza kwa kutoa magazeti na majarida ya michezo kisha ikaingia kwenye takwimu mbalimbali na kutunza historia za mpira wa miguu.
Baadaye taasisi hii ilianza kutangaza tuzo mbalimbali kwa wachezaji na wadau wengine wa mpira wa miguu, wakati baadhi ya mamlaka hufanya rejea ya takwimu za IFFHS, mamlaka nyingine zimekuwa zikipuuza au kutochukua kwa uzito takwimu za asasi hiyo.
Moja ya sababu za kutochukuliwa kwa uzito kwa takwimu za asasi hii zinatokana na ukweli kwamba haina mafungamano na mataifa wanachama wa Fifa hivyo haina nafasi ya kupewa au kupata takwimu sahihi kutoka nchi wanachama wa Fifa. Pia wasomi na vyombo vikubwa vya habari vya Ujerumani kama idara kuu ya habari, DPA vimekuwa vikikwepa kuchapisha au kurejea takwimu za IFFHS, mwaka 2008, profesa wa historia wa chuo kikuu cha Cologne, Ujerumani aliita taasisi hiyo kama mchezo wa mtu mmoja kwa kuwa iliongozwa na mawazo ya mwanzilishi wake, Alfred Poge.
Ni sawa, mtu anaweza kusema Ligi ya Tanzania ni ya kwanza kwa ubora katika Afrika lakini ni muhimu kusema kwa mujibu wa asasi au chombo fulani cha habari, kidogo inaleta ukakasi pale vyombo vya mkondo mkuu kama redio, televisheni au magazeti ya kitaifa yanapofanya rejea ya takwimu za kimpira ambazo si za mamlaka kama Fifa, Caf na TFF bila kueleza ni kwa mujibu wa nani.
Tunaposema Brazil ni Taifa linaloongoza katika viwango vya soka duniani, basi moja kwa moja tunajua ni kwa mujibu wa Fifa lakini kama anayesema siyo Fifa ni muhimu basi kujiongeza na kujua hicho chanzo kingine kinapataje takwimu hizo.
Asasi huru kama magazeti, televisheni, redio na blogu zina nafasi kubwa katika kuelimisha umma kuhusu maendeleo ya mpira wa miguu na michezo kwa ujumla, hata hivyo, si jambo la afya pale watumiaji wanapoachwa wameduwaa kuhusu takwimu gani wachukue. Mfano, ni ngumu sana kwa mfuatiliaji wa kawaida kumwambia Al-Ahly ya Misri ni bora katika msimu wa 2022, kuliko Arsenal na Manchester United za Uingereza na hata Roma ya Italia kwamba Young Africans ya Tanzania iko juu ya Young Boys ya Uswisi. Kwamba Simba ya Tanzania iko juu ya Brighton na Wolverhampton.
Tunajitahidi kuuendeleza mchezo wetu ni jambo la kupendeza mdomoni na masikioni tunapohusishwa na takwimu chanya lakini ni muhimu kujua vigezo na kujipima kama kweli tuko hapo tunapoambiwa kuwa? Vinginevyo ni sawa na kukutana na zuzu mmoja akakwambia wewe ni tajiri kuliko Bakhressa, Dangote na MO Dewj kwa pamoja nawe ukapiga mluzi na kukimbia kumchinja ng’ombe wako wa pekee ukala na majirani zako katika kusherekea taarifa na takwimu za wewe kuwa milionea. Akili za kuambiwa changanya na zako.