Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NIONAVYO: Mafanikio ya Morocco ni ya Waafrika

Morocco To Quarter Final Kikosi cha timu ya Morocco

Sat, 24 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Timu ya taifa ya Morocco ‘Simba wa Atlas’ imeweka rekodi ya kutinga nusu fainali na kumaliza kama mshindi wa nne katika fainali za Kombe la Dunia 2022 zilizomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita nchini Qatar.

Morocco ilifungwa mabao 2-1 na Croatia kaika mechi ya kusaka mshindi wa tatu, huku ikiwa imeweka heshima kubwa kwa timu za Afrika, kwani ilikuwa haijawahi kutokea kwa timu ya bara hilo kufika hatua hiyo.

Mafanikio ya Morocco yamewashangaza wengi si katika Afrika tu, bali pia dunia nzima. Kabla ya mafanikio hayo, nafasi ya juu kufikiwa na timu kutoka Afrika katika Kombe la Dunia ilikuwa ni robo fainali ambayo ilifikiwa na Cameroon (1990), Senegal (2002) na Ghana (2010).

Wafuatiliaji na wabashiri wa soka hawakuipa nafasi kubwa Morocco miongoni mwa wawakilishi wa Afrika.Matumaini zaidi yalionekana kuwa kwa Senegal, Cameroon na Ghana labda kwa sababu hao walikuwa na rekodi ya kufika robo fainali.

Kufika nusu fainali mwaka huu huko Qatar, Morocco iliziondoa timu vigogo kama Hispania, Ubelgiji na Ureno.

Huku dunia ikistaajabu na kusifia mafanikio waliyopata Morocco, nyumbani Afrika na hata hapa Tanzania kulikuwa na baadhi ya maoni ya kubeza na hata kubagua kwamba ushindi wa Morocco si ushindi wa Afrika.

Kwa kweli maoni ya hawa wabaguzi wachache ni ya kushangaza hasa wakati huu wa zama za utandawazi ambapo unategemea watu kuipata kwa urahisi historia na mwenendo wa mpira wa Afrika. Kwa kiasi kikubwa inaonekana ubaguzi huo unatokana na uelewa mdogo wa historia utamaduni na jiografia ya Morocco.

Kwa wanaofuatilia mpira wa Afrika watathibitisha kwamba katika baadhi ya mataifa ambayo huwezi kuacha kuyataja unapoongelea maendeleo ya mpira wa Afrika ni Morocco. Morocco imecheza katika mashindano ya mataifa ya Afrika mara 18 na ilitwaa ubingwa wa Afcon mwaka 1976. Imewakilisha Afrika kwenye Kombe la Dunia mara 6 tangu ilipowakilisha mara ya kwanza mwaka 1970.Mwaka 1986 Morocco ilikuwa timu ya kwanza ya Kiafrika kuongoza kundi la Kombe la Dunia na timu ya kwanza ya Kiafrika kuingia raundi ya 16 Bora.

Morocco ni nchi iliyo kaskazini mwa Afrika huku kaskazini ikipakana na bara la Ulaya na bahari ya Mediterranean. Utamaduni wa Morocco kwa kiasi kikubwa una mchanganyiko wa Ulaya -Arabuni na Afrika.

Kwa maana nyingine, utamaduni wa Morocco na hata mtazamo wao unawakilisha Afrika na zaidi, jambo ambalo hawakulichagua bali ndiyo ukweli wa kihistoria, kijiografia na kiutamaduni.

Kama tulivyoona hapo awali, Morocco ni Waafrika na wameshiriki mashindano mengi ya shirikisho la mpira wa miguu Afrika (CAF) katika ngazi mbalimbali za timu za taifa na klabu. Haishangazi kwamba ubingwa wa Afrika kwa klabu za wanawake na wanaume unashikiliwa na klabu za AS FAR na Wydad Cassablanca kutoka Morocco.

Pamoja na kuwa mwanachama wa CAF na kucheza mashindano ya Afrika, Morocco pia ni mwanachama wa michezo ya mataifa ya Kiarabu (Pan Arab Games)ambako wamechukua ubingwa mwaka 1961 na 1976.

Morocco wanashiriki pia michezo ya ukanda wa Mediterranean ambayo hushirikisha pia timu za Ulaya Kusini na wameshinda mwaka 1983 na 2013.Morocco ni mwanachama wa umoja wa mshikamano wa Kiislam (Islamic Solidarity Games) ambayo wameshinda mwaka 2013.Hizo zote zimekuwa ni fursa kwa Morocco kujiendeleza kimpira na kulitangaza taifa lao pia.

Morocco imekuwa nchi ya msaada kwa mataifa mengi ya Kiafrika katika juhudi zao za kuendeleza soka. Hii ni pamoja na kutoa wataalam wakiwemo makocha na madaktari.Morocco pia imekuwa ikitoa nafasi kwa klabu na mataifa ya Kiafrika, ikiwemo Tanzania, kuweka kambi na kufaidika na miundombinu ya kisasa iliyoko Morocco .Morocco imekuwa mwenyeji wa shughuli nyingi za kimpira za vyama tofauti duniani ikiwemo FIFA. Morocco imewahi kuandaa mashindano ya klabu bingwa ya dunia na inategemewa kuandaa tena mashindano haya mwakani.

Tutake tusitake, mafanikio ya Morocco yana wadau wengi wa kujivunia. Ni mafanikio ya Wamorocco, ni fahari ya Waafrika, ni fahari ya Waarabu, fahari ya Waislam na fahari ya ukanda wa Mediterania.Ni fahari ya ulimwengu wa soka.

Columnist: Mwanaspoti