Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NIONAVYO: Kombe la Dunia ni ng'ombe wa maziwa wa FIFA

Ng'ombe Wa Maziwa Kombe la Dunia ni ng'ombe wa maziwa wa FIFA

Sat, 10 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Shirikisho la kimataifa la mpira wa miguu (FIFA) hivi karibuni lilitangaza kuingiza kiasi cha dola 7.5 bilioni kutokana na mapato yanayohusiana na Kombe la Dunia la Qatar 2022.

Mapato hayo yanahesabiwa kuanzia Julai 2018 hadi Novemba 2022. Mapato hayo ni zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 1 kulinganisha na mashindano ya 2018 yaliyofanyika nchini Urusi. Mashindano ya 2022 yamerigharimu taifa la Qatar kiasi kilichovunja rekodi, yaani zaidi ya dola 200 bilioni (Urusi 2018 walitumia dola 16 bilioni, Brazil 2014 walitumia dola 19.7 bilioni na Afrika Kusini 2010 walitumia dola 7.2 bilioni).

Vyanzo vya mapato ambavyo Fifa inavitegemea kupitia Kombe la Dunia ni pamoja na haki za televisheni, masoko na tiketi za mchezo.

Haki za televisheni ndiyo chanzo kikuu cha mapato yatokanayo na Kombe la Dunia.Kuelekea Kombe la Funia, Fifa huweka sokoni haki za kuonyesha Kombe la Dunia kwa televisheni mbalimbali katika maeneo tofauti. Kampuni nyingi hushindana na hivyo wanaotoa dau kubwa hushinda haki hizo.

Katika haki za televisheni za mwaka 2018, 2022 na 2026 Kampuni za Fox na Telemundo ziliishinda Kampuni ya ESPN na kupata haki hizo.Mshindi wa haki za matangazo huziuza haki mbalimbali kwa vituo vya televisheni, redio na mitandao ya kijamii iliyotawanyika sehemu mbalimbali duniani.

Udhamini na masoko

Kampuni nyingi kubwa duniani hutumia Kombe la Dunia kujitangaza na kutangaza bidhaa zao. Kundi hili lina kampuni nyingi kuanzia za vyakula, za utoaji huduma za vifaa vya elektroniki, magari n.k. Fifa huuza haki hizi kwa kampuni kwa njia ya makundi (category) na hivyo hawauzi haki kwa kampuni zilizo katika ushindani mfano hakuna kinywaji laini utakachokutana nacho katika maeneo na matangazo ya Kombe la Dunia zaidi ya Coca Cola na bidhaa zake.

Kwa sasa Fifa ina uhusiano wa udhamini na Adidas, Coca Cola, Hyundai-kia, Qatar Airways, Visa, Wanda Group, Anheuser-Busch InBev, Hisense, Mc Donalds, Mengniu Dairy na Vivo.

Tiketi na huduma za ukarimu

Wakati wa Kombe la Dunia Fifa huuza tiketi kupitia vyama vya kitaifa vya mpira wa miguu (FAs) na mawakala wengine.

Wakati tiketi katika mchezo wa makundi kama ule wa Saudia dhidi ya Argentina iliuzwa kwa shilingi laki tano, tiketi ya mchezo wa fainali inaweza kuwa kwenye shilingi milioni 5 na kuendelea. Fifa hushirikiana na taasisi za huduma (hospitality) kama hoteli mbalimbali kuuza tiketi za Kombe la Dunia zinazotoa huduma zaidi ya kuangalia mpira kama kukaa sehemu nzuri uwanjani, vinywaji, ukumbi na hata malazi na usafiri kwa mteja. Kupitia huduma hii Fifa hupata fedha nyingi na pia kujenga uhusiano na wadau.

Ni kutokana na mapato ya Kombe la Dunia Fifa inaweza kupata pesa za kujiendesha na kuuendesha mchezo na mipango yake mbalimbali kama miradi ya vijana, makocha, waamuzi, mafunzo ya utawala n.k.

Siri kubwa ya Fifa kupata faida kwenye karibu kila Kombe la Dunia ni kuacha mwenyeji ajishughulishe na uandaaji wa miundombinu ya mashindano kama ujenzi wa viwanja, barabara, mahoteli nk huku Fifa ikijikita katika mambo ya utawala kama kulipa posho za kamati ya maandalizi, waamuzi na gharama za zawadi za timu shiriki.

Columnist: Mwanaspoti