Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NDANI YA BOKSI: Kama sio Mbappe na Halaand, hawa wanatosha kabisa Madrid

Madrid Pic Data.png Kama sio Mbappe na Halaand, hawa wanatosha kabisa Madrid

Fri, 27 May 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Real Madrid imepata pigo kwenye mpango wake wa usajili katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya straika Mfaransa Kylian Mbappe kuamua kubaki zake Paris Saint-Germain.

Fowadi huyo supastaa, Mbappe, 23, alikuwa akihusishwa na mpango wa kuondoka PSG mwisho wa msimu huu kutokana na mkataba wake kufika tamati. Lakini, sasa amesaini dili jipya Parc des Princes la kubaki hapo hadi 2025.

Mara kibao, Mbappe alishindwa kuafikiana makubaliano juu ya ofa ya mkataba mpya huko PSG jambo lililowapa nguvu kubwa Real Madrid kuamini kwamba watanasa saini yake mwaka huu huku wakimsaka pia Erling Haaland.

Lakini, Los Blancos imepata pigo kubwa kwenye kuelekea msimu wa 2022-23 kwa sababu hakuna mchezaji yeyote watampata baina ya wawili hao, Mbappe na Haaland.

Mbappe amebaki PSG na Haaland ametimkia zake Manchester City. Dili jipya la Mbappe lina thamani ya Pauni 500 milioni. Real Madrid hawana ujanja, kutokana na straika wao Karim Benzema kuwa na umri wa miaka 34, hakuna namna zaidi ya kusajili mshambuliaji mwingine kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi mwaka huu.

Kutokana na kuwakosa Mbappe na Haaland, hii hapa orodha ya washambuliaji watano ambao Los Blancos inaweza kwenda kunasa huduma ya mmoja wao ili kufidia hasira za kuwakosa washambuliaji hao matata kabisa kwa sasa.

Mohamed Salah

Kama humpati Haaland au Mbappe, unaweza kuwa kwenye tatizo zaidi ukimkosa pia Salah. Mshambuliaji huyo ubora wake umekuwa bora siku hadi siku ukiendana na umri wake, ambapo kwa sasa ana miaka 29 na anacheza soka la kiwango cha juu. Mo Salah amekuwa na shida na Liverpool juu ya mkataba mpya na huenda akapigwa bei mwaka huu ili kuepuka kumpoteza bure mwakani. Liverpool wanatamani sana Mo Salah abaki, lakini kutokana na mkataba wake kubakiza mwaka mmoja tu, chochote kinaweza kutokea kwa wakali hao wa Anfield wakaamua kumpiga bei.

Kuhusu suala la kufunga mabao, Mo Salah amekuwa akifanya hivyo kwa kadri anavyotaka na ndio maana ameshinda Kiatu cha Dhahabu kwenye Ligi Kuu England msimu uliokwisha Jumapili iliyopita. Utakuwa usajili safi Madrid ikimnasa.

Baada ya kushinda kila kitu Liverpool, bila ya shaka Mo Salah atahitaji kwenda kukabiliana na changamoto mpya.

Sadio Mane

Si kitu kinachowezekana kwa Real Madrid kumsajili Mo Salah kwa wakati huo huo ikimsaka pia mchezaji mwenzake kwenye kikosi cha Liverpool, Sadio Mane. Lakini, supastaa huyo wa Senegal atakuwa ingizo bora kabisa kwenye timu yoyote itakayofanikiwa kupata saini yake. Mane amekuwa na kiwango bora kabisa huko Liverpool hasa kwa msimu wa 2021-22, ambapo miamba hiyo ya Anfield ilikuwa ikisaka mataji manne makubwa ndani ya msimu mmoja kabla ya Jumapili iliyopita kulikosa taji la Ligi Kuu England. Kama ilivyo kwa Mo Salah, naye mkataba wake utafika tamati mwishoni mwa msimu ujao. Akiwa na umri wa miaka 30, Mane ni moja ya mastaa ambao Liverpool inaweza kufikia kumpiga bei kama hatakuwa tayari kusaini mkataba mpya wa kuendelea kubaki huko Anfield. Barcelona nayo inamtaka.

Richarlison

Kubaki Merseyside kutawafanya Everton kuwa kwenye furaha kubwa baada ya kunusurika kushuka daraja msimu uliomalizika hivi karibuni na kushihuhudia Norwich City, Watford na Burnley zikishuka na kwenda Championship.

Hata hivyo, Everton itakuwa kwenye wakati mgumu wa kubakiza saini za wachezaji wao muhimu wakati dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi la mwaka huu litakapofunguliwa. Washambuliaji Dominic Calvert-Lewin na Richarlison ni muhimu kwenye kikosi cha Everton, lakini wachezaji hao wamekuwa kwenye rada za timu nyingi wakihitaji saini zao. Mbrazili, Richarlison mpango wake ni kwenda kujiunga na klabu kubwa ili kupata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na kama atakwenda Bernabeu, utakuwa usajili safi kwa miamba hiyo katika kumtafuta mtu wa kusaidiana na Benzema. Kuna wakati Richarlison alihusishwa na miamba ya soka ya Ufaransa, PSG ilipokuwa na wasiwasi wa kumpoteza Mbappe.

Ousmane Dembele

Ishu ya Mfaransa huyo huko Barcelona bado haijakaa vizuri. Kocha wa Barcelona, Xavi ni shabiki mkubwa wa mchezaji huyo na alikuwa kwenye kiwango bora kabisa msimu uliomalizika hivi karibuni baada ya kusumbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara tangu alipoondoka Borussia Dortmund mwaka 2017. Dembele mkataba wake unafika mwisho na atakuwa mchezaji huru kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka huu. Staa huyo na mawakala wake wamekuwa kwenye mazungumzo na mabosi wa Barcelona juu ya mkataba mpya, lakini bado hakuna kilichofikiwa. Na kutokana na mkataba kuelekea mwisho kabisa, Dembele naye anakaribia kabisa mlango ulioandikwa ‘exit’ huko Nou Camp. Timu kibao zimekuwa zikihusishwa na mchezaji huyo ikiwamo Chelsea, Manchester United, Bayern Munich, Juventus na PSG. Kwa kumkosa Mbappe na Haaland, Los Blancos inaweza kwenda kunasa saini ya Dembele na wakaendelea kufurahia maisha uwanjani.

Harry Kane

Kuna mastaa kibao wenye majina makubwa ambao Real Madrid inaweza kuwanasa. Moja ya majina hayo makubwa kwenye soka ni mshambuliaji wa Tottenham Hotspur, Harry Kane. Staa huyo Mwingereza mwenye umri wa miaka 28, mwaka jana alikaribia kabisa kusajiliwa na Manchester City, lakini badala yake kocha Pep Guardiola aliamua kufungua pochi, Pauni 100 milioni kumchukua Mwingereza mwingine, Jack Grealish. Kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi Man City imemsajili Haaland, hivyo Kane ataendelea kubaki Spurs. Na Real Madrid kitendo cha kumkosa Mbappe, mabosi wa timu hiyo wanaweza kuhamishia nguvu kwa Kane, hasa ukizingatia itampatia nafasi muhimu ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Sawa, Spurs nayo itacheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, lakini ni tofauti unapokuwa kwenye kikosi cha Los Blancos, huko uwazia kuhusu kulibeba taji hilo. Bei yake anayouzwa ni kati ya Pauni 100 na 150 milioni.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz