Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mzize wa Annaba na Kigali na fursa zake tatu mkononi

Mzize Wa Annaba Na Kigali Na Fursa Zake Tatu Mkononi Mzize wa Annaba na Kigali na fursa zake tatu mkononi

Wed, 20 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hotelini Park Inn Radisson pale eneo la Kiyovu, Kigali, Rwanda nilimwambia Clement Mzize, mshambuliaji aliyeanza kuongoza mashambulizi ya Yanga dhidi ya El Marreikh kwamba kuna kitu nataka kuongea naye. Sikupata nafasi hiyo na miadi yetu ipo pale pale.

Hakuna siri sana. Nitakachomwambia ndio hiki hiki ambacho nataka kukiandika leo. Labda nitaweza kuongeza maneno machache wakati huo tukiongea kwa sababu itakuwa tunatazamana sura kwa sura. Mengineyo yanaweza kuandikwa hapa.

Katika fainali za Kombe la Dunia pale Ufaransa mwaka 1998 Wabrazil walikwenda na mchezaji aliyeitwa Ze Carlos. Miaka michache kabla ya michuano hiyo Ze Carlos alikuwa anauza matikiti nchini kwao Brazil. Hakuwa miongoni kwa maelfu ya wachezaji wengi wa Kibrazil ambao wanapitia ngazi mbalimbali za soka la vijana hadi kufika juu.

Ze Carlos alichomokea kitaani akafanya mambo makubwa katika soka la ndani kiasi cha kustahili kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Brazil kilichokwenda Ufaransa kutetea Kombe la Dunia pale Ufaransa. Kumbuka kwamba miaka minne iliyopita Wabrazil walikuwa wametwaa Kombe la Dunia pale Marekani.

Na kuna hii hadithi ya Clement. Naambiwa kwamba miaka michache iliyopita alikuwa akizurura na bodaboda pale Iringa. Dereva mzuri tu anayepambana kuhakikisha siku inamalizika salama kwa kujipatia riziki ya kawaida. Jumamosi hii alikuwa anaongoza safu ya ushambuliaji ya miongoni mwa timu kubwa nchini pale Kigali. Yanga.

Wikiendi ile nyingine alikuwa anaongoza safu ya ushambuliaji ya timu yake ya taifa pale Annaba nchini Algeria. Kando ya Simon Msuva na Kibu Dennis. Nadhani akiwa anaendesha bodaboda alikuwa anawasikia watu hawa katika vyombo vya habari. Sidhani kama alijua kwamba mapema baadaye atakuwa nao anaongoza safu ya ushambuliaji ya Stars.

Hivi ndivyo maisha yanavyokwenda kasi. Kuna wanadamu maisha yanakwenda kasi namna hii. Sio katika soka tu, bali katika maisha kwa ujumla. Katika fani mbalimbali. Ni kama kifo tu. Leo unaweza kuwa na afya njema lakini usiweze kuiona kesho.

Kwa Clement, habari kubwa katika kichwa chake sio kuitazama jana yake, bali kuitazama kesho yake. Wakati mwingine Watanzania tuna tabia ya kujifariji kwa kuilinganisha jana yetu na leo yetu. Hatutaki kuilinganisha leo yetu na kesho yetu. Kama leo yetu ni salama kuliko jana yetu huwa hatutaki kuitamani kesho yetu.

Miongoni mwa watu ambao wamefanikiwa kuitazamani kesho yao kuliko jana yao au leo yao ni Diamond Platinumz. Kila siku anaitamani kesho yake. Nazungumzia kuhusu wasanii na wanamichezo. Wengine wengi wanatanua makwapa wakiona leo yao ni nzuri kuliko jana yao.

Kwa mfano, Mzize ana mambo yanayovutia usoni kwake. Kwanza kabisa Fiston Mayele hayupo tena Yanga. Haishangazi kuona kwamba alianza pambano la Jumamosi dhidi ya El Marreikh. Kocha wa Yanga, Miguel Gamond aliamua kumuanzisha mshambuliaji mmoja Jumamosi. Akamchagua Mzize badala ya Musonda.

Kama Mayele angekuwepo basi Mzize angeanzia nje. Labda angeanzia baadaye. Hii ni fursa ya kwanza ambayo Mzize aliipata. Na kama tunataka kusema ukweli ni kwamba ile ni fursa ambayo aliitendea haki. Aliondoka uwanjani na bao moja huku akionyesha kiwango kizuri.

Lakini ukiachana na fursa hiyo moja, Mzize ana fursa mbili zaidi. Zote mbili zipo mikononi mwake. Fursa ambazo zinaweza kumtoa kutoka katika bodaboda aliyokuwa anaendesha na kisha kuendesha Range Rover. Labda kwa sasa anaendesha gari ya Kijapani na anadhani amefanikiwa kimaisha. Kuna fursa ya kuendesha Range Rover na kuishi katika apartment binafsi Masaki.

Ya kwanza kabisa ni kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa akiwa na Yanga. Na bahati nzuri kwake ni kwamba Yanga ina asilimia tisini za kwenda kucheza hatua ya makundi. Kama Yanga wakifuzu watakuwa na mechi sita kwa kuanzia. Tatu za nyumbani na tatu za ugenini. Hili ni jukwaa bora katika kuonyesha uwezo wake katika ngazi ambayo itamchukua kutoka katika gari alilonalo sasa hivi kwenda katika Range Rover.

Mayele ameondoka akitokea katika jukwaa hili. Wote tunafahamu kwamba Mayele ni hatari. Ametutisha sana ndani ya nchi hii lakini alipopewa jukwaa la michuano ya Shirikisho ndipo alipochomokea. Mabao saba katika michuano ya Shirikisho ilikuwa lazima yamuondoe Yanga.

Katika dunia ambayo ina uhaba wa washambuliaji, mabao saba yalitosha kumuondoa Mayele na kumpa mshahara ambao naamini unaweza kuwa mara tatu ya ule mshahara mzuri aliokuwa analipwa Yanga. Huu ndio ukweli. Lazima atakuwa anapokea mshahara wa kumiliki Range Rover.

Mabao matano tu au sita ya Mzize yanaweza kumtoa hapa alipo na kwenda mbali zaidi. Dunia ina uhaba wa washambuliaji na makipa. Mabeki sio tatizo, viungo sio tatizo, hata mawinga sio tatizo. Tunabakiwa na tatizo la washambuliaji au wafungaji.

Fursa ya pili ambayo imemuangukia Mzize ni michuano ya Afcon ambayo itafanyika pale Ivory Coast mwakani. Nilikuwepo Annaba na niliona imani ya kocha Adel Amrouche kwake. Nadhani anaweza kuwa miongoni mwa washambuliajj wetu wa kutegemewa pale Ivory Coast. Katika nyakati hizi anbazo zama za Mbwana Samatta zinaelekea ukingoni huku soka la kisasa likiwa na mahitaji makubwa ya nguvu, Mzize atahitajika.

Mawakala wataunganisha tu kuanzia kwa Mzize wa michuano ya Ligi ya Mabingwa na wa michuano ya Afcon. Na watakapoona kuwa pasipoti yake ni nzuri na inaonyesha ana miaka 19 nadhani atakuwa katika nafasi nzuri ya kwenda mbali zaidi. Narudia. Dunia ina uhaba wa washambuliaji.

Hata hivyo, itategemea zaidi na kile ambacho atakifanya kuanzia sasa hadi wakati huo. Kama angekuwa mchezaji wa Nigeria angejua kama hii ni fursa ya kutazama mbele zaidi na sio kuridhika kutoka kule alikotoka. Ni mida hii angeweza kuwa Diamond Platinumz au Mbwana Samatta. Watu waliosahau zaidi walikotoka na kujali zaidi wanakokwenda.

Na kama akifanya kila kitu katika uwezo wake basi atailazimisha Yanga kufanya kile ambacho walifanya kwa Mayele. Kumuuza. Sio kwamba Yanga walipenda kumuuza Mayele. Walilazimishwa. Kama Mzize akifanya vizuri na Yanga wakapokea ofa nono basi hawatakuwa na jinsi.

Najua kwamba klabu zetu hazipendi kuuza mastaa wake nyota mpaka pale zitakapolazimishwa. Mzize ana fursa tatu mkononi ambazo anaweza kuilazimisha Yanga wamuuze ili aendelee na simulizi yake ya kusisimua ya kutoka kuendesha bodaboda hadi kwenda Yanga. Kisha wapi kwingine? Inaweza kuwa Marseille au Anderlecht. Nani anajua?

Columnist: www.tanzaniaweb.live