Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mynaco: Natamani kuolewa, nizae watoto watano

Mynaco: Natamani Kuolewa, Nizae Watoto Watano Mynaco: Natamani kuolewa, nizae watoto watano

Thu, 23 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Huyu Maimuna Hamis ‘Mynaco’ sio mtu wa mchezo mchezo hata kidogo. Yaani unamzungumzia fundi wa mpira ambaye ameshinda mataji matano mfululizo ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania.

Kiraka huyu ambaye anamudu kucheza nafasi zote za kiungo alianza safari yake ya soka mwaka 2016 na Mburahati Queens ambako alidumu kwa mwaka mmoja na 2017 kisha akajiunga na JKT Queens ambako ubabe wake wa kubeba mataji mfululizo ulianzia hapo.

Katika misimu yake miwili na JKT, Mynaco alishinda ubingwa Ligi Kuu ya Wanawake msimu wa 2017/2018 na 2018/2019.

Msimu uliofuata akajiunga na Simba Queens na mataji yakamfuata huko Msimbazi pia. Alishinda taji lake la tatu jumla na la kwanza kwa Simba msimu wa 2019/20, kisha 2020/21 wakabeba tena na akakamilisha taji lake la tatu Msimbazi na la tano kwake binafsi msimu wa 2021/22.

Msimu uliopita wa 2022/23, Yanga Princess ilifanya usajili mkubwa ikamchukua na Mynaco, mwenye nyota yake ya mataji, kwa matarajio ya kupata taji lao la kwanza ambalo lingekuwa la sita mfululizo kwa kiungo huyo.

Hata hivyo mambo yalikwenda ovyo. Ubingwa ulienda JKT Queens, Simba Queens ikawa ya pili huku Yanga Princess ikiishia kushika nafasi ya nne.

Baada ya kucheza msimu mmoja bila ya mafanikio akiwa na Yanga Princess, Mynaco akatimkia Zed FC inayoshiriki Ligi Kuu ya wanawake nchini Misri, ambako amekutana na nyota mwenzake wa zamani Yanga, Fiston Mayele anayekipiga katika klabu ya Pyramids ya huko.

Mynaco, ambaye jina hilo alipewa na wanafunzi wenzake akiwa darasa la saba kwa kuwa alikuwa mtukutu anayependa kucheza na wanaume mpira wa miguu, ameandika historia nyingine ya kuchezea timu zote tatu zenye ushindani za Simba Queens, JKT Queens na Yanga Princess.

MALENGO YAKE

Anasema lengo lake ni kufika mbali zaidi hivyo anataka kufanya makubwa hapo Misri ili iwe daraja la kutimiza ndoto zake.

“Kwangu kuichezea timu hiyo ni fursa ya kuonekana sehemu nyingine kwani kuna watu wananitamzama watahamasika wakiniona, nataka kufika mbali, kikubwa nazingatia nidhamu na juhudi,” anasema.

APATA NAMBA

Anasema tangu ajiunge na kikosi hicho amecheza mechi mbili na zote amemaliza dakika 90.

“Najua sio rahisi kupata namba ugenini, wengi walilalamika lakini mimi namshukuru Mungu nimefika tu nacheza tena dakika zote 90,” anasema.

Mbali na kupata namba lakini kiungo huyo tayari amepata rafiki wa kuongea naye na kubadilishana mambo mbalimbali ya mpira.

YANGA YAMPA UZOEFU

Kiraka huyo anasema Yanga imempa fursa nyingi ikiwemo kucheza nafasi tofauti kwani mwanzo alikuwa anamudu kucheza beki kiraka.

Anaeleza alipofika Yanga alibadilishwa nafasi tena akicheza kiungo namba 6, 8 na namba 10.

“Hii ni fursa mimi naweza hata siku ninapocheza ikatokea dharura nikamudu kucheza nafasi hizo kwa kuwa Yanga walinijenga na kunipa uzoefu mzuri,” anasema.

KWA NINI HAITWI STARS?

Kiungo huyo licha ya kuonekana kufanya vizuri eneo la kati lakini kwa miaka ya hivi karibuni hajaitwa timu ya taifa.

Mwenyewe anasema: “Tusiongee sana kuhusu kuitwa timu ya taifa ila jua kuwa labda muda wangu bado na sijahitajika kwasasa ila naamini timu ya taifa ni ya wote wakiona nahitajika nitaitwa tu.”

HAKUNA KAMBI

Anasema Misri kuna utaratibu wa tofauti kwani wachezaji kila mmoja anatokea kwake anakoishi na sio kukaa kambini.

“Kwa miezi kadhaa tumeambiwa tutakaa hotelini, baadaye kila mmoja atapangiwa nyumba hakuna kukaa kambini,” anasema.

YEYE ZANZIBAR

Mchezaji huyo anapendelea kutembelea maeneo ya Zanzibar kutokana na mandhari ya visiwa hivyo vilivyojaa historia.

Anasema akiwa Misri anavikumbuka vitu vingi vya Tanzania ikiwemo vyakula vya Zanzibar kama urojo na kachori.

LUGHA FRESHI

Kiungo huyo anaeleza kuwa kwa asilimia kubwa wachezaji wanatumia lugha ya Kiarabu na Kiingereza kidogo.

“Mimi nimesoma kidogo madrasa kwahiyo Kiarabu naelewa baadhi ya maneno wakiongea, pia ukiwa mtu wa mpira kuna lugha wanatumia unaelewa tu ila pia najua Kiingereza.” Anasema

FAMILIA

Anatamani kuwa na familia lakini anamini muda sahihi ni akimaliza soka.

“Natamani niolewe niwe na familia yangu, nipate watoto watano,” anasema mwanadada huyo.

Columnist: Mwanaspoti