Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mwisho wa zama unavyozidi kuukodolea macho CHADEMA

A0992fa2d5d3b2db0a73803130bd0baa.jpeg Mwisho wa zama unavyozidi kuukodolea macho CHADEMA

Wed, 2 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SAKATA la wabunge 19 wa Viti Maalumu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) limeendelea kuacha maswali kwa watu wengi, nikiwamo mimi kuhusu uhalali wa hatua zilizochukuliwa na uongozi wa chama hicho kuwafukuza uanachama.

Sakata hilo pia limeendelea kuonesha namna Watanzania tunavyopenda kuishi kwa dhana. Kwamba mtu akitoa uamuzi unaotofautiana na wenye chama chao, basi wamenunuliwa!

Nikianza na suala la hatua zilizochukuliwa na chama hicho dhidi ya akina Halima Mdee na wenzake 18 za kuwafukuza uanachama, nimesikia msingi wa hatua hiyo ni kupinga kwao kwamba uchaguzi mkuu uliopita haukuwa halali. Kwamba waliibiwa kura na demokrasia haikuzingatiwa.

Hii maana yake ni kwamba wameamua kutotambua uchaguzi uliofanyika na wao wakapata kura za wabunge zilizowawezesha kupata viti 19 vya ubunge wa viti maalumu pamoja na mbunge mmoja wa kuchaguliwa.

Ninavyoelewa mimi msimamo huo unalenga pia kuionesha dunia kwamba hakuna demokrasia Tanzania.

Mengine waliofanya kwa lengo hilo ni baadhi ya waliokuwa wagombea wao wa nafasi mbalimbali kudai kukimbia nchi kwamba wanatishwa.

Yaani wasitishwe wakati wanagombea hadi matokeo kutangazwa ndipo leo waje kutishwa baada ya kushindwa uchaguzi!

Maswali yanaanzia hapa: Usiku ule niliposikia kwamba Halima Mdee na wenzake wamefukuzwa uanachama kutokana na kitendo chao cha kuamua kuwakilisha chama chao bungeni, nijiuliza kwa nini yule mwingine wa 20, Aida Khenani, aliyeshinda uchaguzi hayumo?

Inawezekana wanafukuzwa kwa kitendo cha kwenda bungeni bila ruhusu ya wakubwa na hivyo suala la kwenda bungeni siyo hoja wanayopinga, lakini kama ndivyo, ni chombo gani chenye jukumu la kujua na mwanamke gani anafaa kuwakilisha Chadema bungeni kama sio wanawake wenyewe kupitia Bawacha?

Hapo pia ninapata swali lingine. Je, kama Chadema haina pingamizi ya kuwa na uwakilishi bungeni na ndio imemruhusu Aida aendele na ubunge wake, ilitaka akina Freeman Mbowe ambao wamekuwa wakituhumiwa kwa upendeleo wa kuchagua ‘watu wao’ ndiyo wachague wabunge wa viti maalumu kuwakilisha chama hicho?

Kama kumbukumbu zangu ni sahihi, mwaka 2015, Chadema pia ilidai kutotambua matokeo ya uchaguzi mkuu ingawa hatua ya mgombea urais wao wakati huo kurudi CCM inapingana na msimamo waliokuwa nao!

Lakini pamoja na msimamo huo huku wakitoka bungeni siku ambayo Rais John Magufuli alikuwa anazindua Bunge, lakini hatukuona wanagomea kuingia bungeni. Wale waliochaguliwa kwenye majimbo na wale wa viti maalumu waliingia bungeni licha ya madai yao ya kawaida ya kupinga ushindi wa CCM.

Tunaambiwa kwamba Mbowe akiwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika bunge lililopita, wakati Chadema wanatoka nje kuonesha kutokubaliana na matokeo yaliyomweka Rais Magufuli madarakani 2015 alikuwa tayari keshachukua marupurupu yote ya kiongozi wa kambi hiyo!

Halafu sikuelewa kwa nini suala hili waliliharakisha sana, wakianza kwa kusemasema kwenye vyombo vya habari badala ya kupata muda wa kutafakari na hata Halima alilisema hili jana kwamba suala zima lilihitaji subira badala ya kutoa uamuzi wa hasira na kukurupuka.

Ukiacha hili la sasa la kugomea viti maalumu huku wakiruhusu aliyechaguliwa kwenye jimbo kuingia bungeni wakilenga kuihadaa dunia kwamba Tanzania hakuna demokrasia, ni vyema tujiulize ni lini huku kususia kumewasaidia wapinzani kisiasa kwa maana ya kuimarisha chama chao?

Kuna mtu mmoja naye ameandika kwenye Jamii Forum kwamba vyama vyetu vya upinzani vimewahi kususia mambo mengi na kufanya migomo ya aina mbalimbali, ambayo matokeo yake sote tunajua yalikuwa ni hasara zaidi kuliko manufaa kwa upinzani!

Mtu huyo anatoa mfano wa hatua ya Maalim Seif kususia uchaguzi wa marudio wa Zanzibar wa mwaka 2015 akiamini kwamba kuna siku angepewa ushindi wa mezani na kuapishwa kuwa Rais wa Zanzibar, ilimsaidia nini?

Bila shaka alisubiri mpaka muda wa uchaguzi mwingine ukafika bila kupewa ushindi wa mezani huku baadhi ya wafuasi wake wakiwa wamezidi kukata tamaa.

Mwaka 2019, wapinzani walisusia uchaguzi wa Serikali za Mitaa hatua ambayo imeinufaisha sana CCM hata kwenye uchaguzi wa mwaka huu huku wapenzi wa chama hicho wakishindwa hata kujiandikisha kutokana na kukata tamaa.

Halima alisema jana alipozungumza na waandishi wa habari na mimi ninakubaliana naye kwamba kuchukua viti maalumu hakuzuii chama kuendelea na mapambano yake yoyote yale, kitu kinachoonesha kwamba akina Halima wana akili kubwa kuliko waliowafukuza pengine kinachowasumbua ni hasira za kukosa kuingia mjengoni! Hivi Mbowe angeshinda kule Hai, msimamo huo ungekuwepo?

Kudhani kwamba kugomea viti maalumu kutasaidia kuzishawishi jumuiya za kimataifa kuilazimisha Tanzania irudie uchaguzi mkuu ambao hata ukirudiwa watashindwa au kudhani hatua hiyo itasababisha jumuiya ya kumataifa kuiwekea nchi vikwazo ni fikra pia finyu sana.

Akina Halima wakifika mahakamani ninaona ushindi mkubwa kwao kuliko kamati kuu kutokana na kutoa uamuzi bila kusikiliza upande mwingine, jambo ambalo siyo la kidemokrasia. Akina Halima wanasema waliomba suala hilo lisogezwe mbele lakini Mbowe na Kamati yake hawakuwasikiliza.

Mimi si mwanasheria lakini kwa akili ya kawaida tu naona akina Halima watalindwa mahakamani na ukweli kwamba mazingira ya eneo waliloitiwa hayakuwa rafiki kwao, wangeweza hata kupigwa mawe na hasa baada ya kuwepo kwa kauli kali na chochezi za Katibu wa chama hicho, John Mnyika, ambaye sakata hilo limemwonesha kama mtu asiye na subira hata za kunywa maji!

Sakata hili pia limeendelea kuionesha Chadema ya Mbowe kama chama cha kibabe cha fukuza fukuza badala ya majadiliano na kuendelea kukiacha CCM kuwa chama kimbilio la wanaofukuzwa.

Kinazidi kudhihirisha kwamba ukitofautiana tu na mwenyekiti basi halali yako ni kufukuzwa. Tuliona kuanzia zama za Chacha Wangwe (sasa marehemu) alipoyataka madaraka ya Mbowe, tukaona kwa akina Zitto Kabwe walipoandika waraka wa kudai mabadiliko ndani ya Chadema na hivi karibuni tumeona kwa akina Silinde walipotofautiana na Mbowe na genge lake kuhusu suala la kushughulikia ugonjwa wa corona.

Lakini lingine ambalo tumeendelea kuliona kwenye sakata hili ni suala zima la dhana. Yaani chama hicho na wapambe wake wameendelea kuwa na dhana potofu kwamba kila anayetofautiana na msimamo wa akina Mbowe kanunuliwa na Chama Cha Mapinduzi au serikali yake.

Nimekuwa nikiona hatua ya akina Halima ambayo inaonesha kutokubaliana na akina Mbowe ikichukuliwa kama wamenunuliwa!

Mtu anakuwa kama Rais Donald Trump kudai aliibiwa kura bila kuwa na ushahidi wowote. Ndivyo pia kwa Chadema na wafuasi wao kwani ukifungua mitandao utaona wanataka kuuaminisha umma wa Watanzania kwamba hatua ya akina Halima inatokana na ushawishi wa pesa au kuahidiwa vyeo ukiwepo uwaziri.

Tatizo la dhana hizi mbovumbovu zilianza pale tulipokuwa tunaona wimbi la wanachama wa Chadema wakiwemo viongozi kuamua kwenda kinyume na mageuzi makubwa yaliyokuwa yanafanywa na Rais John Magufuli ambayo kila mwenye macho alikuwa akiyaona huku Chadema ikikalia kuyabeza! Hivi nani anaweza kumnunua Edward Lowasa, akamnunua Fredrick Sumaye kwa lipi?

Waswahili wanasema kwamba kamba hukatikia pembamba na pia wanasema la kuvunda halina ubani. Mimi kwa mtazamo wangu naona kama Chadema mwisho kabisa wa zama.

Kwamba chama hicho ambacho wakati fulani hata mimi mwandika makala haya nilikiamini na kukiheshimu kama kisipopata mabadiliko ambayo akina Zitto waliyataka basi mwisho wake ndiyo huu.

Kinavyoendelea kupoteza watu wake muhimu kama kilivyowapoteza akina Dk Wilbrod Slaa na wengineo, kinazidi kubaki na magarasa, vibaraka wa mabeberu na wachumia tumbo.

Columnist: habarileo.co.tz