Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mwili mkakamavu unajengwa hivi

IMG 4269.jpeg Mwanasoka Cristiano Ronaldo

Sun, 11 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kila kijana wa kisasa anapenda kuvaa mavazi ya kisasa ambayo yanaendana vyema na mwili wake kwa lengo la kuwa na mwonekano nadhivu wenye kuvutia.

Lakini mwili huo wenye kuendana na mavazi hayo hauji ukiwa umekaa tu bali ni kwa mazoezi mchanganyiko ikiwamo yale mazoezi ya gym na mazoezi mepesi.

Wapo ambao wanapenda kuwa na umbile la kikomavu kama ilivyo kwa Christiano Ronaldo au la Ibrahimovic ambaye wiki iliyopita ametangaza kustaafu soka akiwa na miaka 41.

Mara nyingi maumbile yaliojengeka vyema kimazoezi yanaonekana zaidi kwa wachezaji wa soka hii ni kutokana na ukweli kuwa mchezo huu unahitaji utimamu wa mwili ili kuweza kucheza kwa kiwango.

Hata hapa Tanzania miili kama ya Clatous Chama, Mudathir Yahya au Mzamiru Yassin ni miili ambayo ina ukakamavu wa kiwango cha juu hii ni kutokana eneo wanalochezea ni moja ya nafasi ngumu katika soka.

Wapo vijana ambao si wanasoka ila wanatamani kuwa na mapaja makakamavu kama ya kiungo wa Yanga Azizi Kii au Wapo ambao wanatamani kuwa na “six pack” kama ya kiungo wa Simba, Chama.

Kiujumla kizazi kipya chenye mihemko ni kawaida kupenda kuwa na miili ambayo imejenga vizuri kuanzia chini mpaka juu lakini wengi hawajui siri ya kujenga mwili uliojengeka kirahisi.

Mwanaume kuwa na mwili wenye muonekano mzuri ulio na misuli imara na iliyojengeka ni jambo ambalo linapendwa lakini si kila zoezi linaweza kuujenga mwili wote.

Kwa wanasoka walio wengi huwa wanafanyishwa mazoezi mchanganyiko ikiwamo yale maalum ya gym pamoja na mazoezi ya kuogelea ndio maana utimamu na ukakamavu wao huwa ni mwili mzima.

Wapo vijana wengi ambao hubeba vyuma vizito kiholela ili kuujenga mwili pasipo kufahamu ni aina gani ya mazoezi yanayoweza kujenga mwili wenye mvuto.

Yapo mazoezi ambayo yanakubalika na wataalam wa tiba za michezo na mazoezi ya viungo kuwa ndio yanakufanya kujenga mwili wote kutokana na uwezo wa kushughulisha misuli mingi ya mwili.

Mazoezi haya endapo mwanadamu atayafanya mara kwa mara humfanya kuwa na mwili imara uliojijenga kama vile walivyo wanasoka.

Yapo mazoezi bora ambayo yakifanywa kwa umakini huweza kutengeneza mwili uliojengeka pasipo kwenda gym wala kutumia virutubisho vya kutunisha misuli vinavyouzwa kiholela mitandaoni.

SIRI YA MAZOEZI HAYO

Zoezi linaloshika namba moja kwa kujenga mwili huwa ni kuogelea, zoezi hili linaujenga mwili kwani kuogelea kunahusisha misuli mingi zaidi kuanzia miguu, kiwili wili, mikono na kichwa.

Jaribu kuwatazama wavuvi, wapiga mbizi, wanamichezo waogeleaji utagundua wamejengea mwili mzima. Zoezi hili ndilo ambalo limekuwa ni sehemu ya maisha ya wanasoka wwakulipwa ndio maana klabu kubwa za kisasa zimeweka mabwawa ya kuogelea katika kambi zao.

Zoezi la pili ambalo linashika nafasi ya pili kwa kujenga mwili huwa ni kucheza mziki, lakini sio mziki laini kama ilivyo bluzi au taarabu asilia.

Mziki kama wa dansi, afro, house, hot fanky, pop na ngoma za kitamaduni inahusisha kuchezesha misuli mingi mwilini hivyo kumfanya mcheza dansi kuwa na misuli imara.

Miaka ya nyuma mwanamziki wa zamani wa Rap Mc Hammer au Michael Jackson alikuwa akipungua uzito kila baada ya kutoka katika tamasha alililotumbuiza hii ni kutokana na mwili wake kutumia misuli mwingi wakati wa kucheza mitindo yake.

Zoezi linaloshika namba tatu huwa ni kukimbia, mwanadamu anapokimbia huweza kuhusisha misuli ya mwili mzima. Ukiwatizama wanariadha wengi duniani wana miili imara yenye misuli iliyojijenga vema.

Upo ushahidi wa kitafiti unaonyesha ufanyaji wa zoezi hili kuchangia mamilioni ya wakimbiaji kuwa na miili iliyojengeka huku wakiishi maisha marefu zaidi.

Ukitizama maisha ya mwanasoka yoyote yule kila mara zoezi hili atalifanya na pia katika kucheza soka kukimbia ni sehemu ya maisha ya mchezo huo.

Michezo kama sarakasi, michezo ya karate, mpira wa miguu, mpira wa kikapu, mchezo wa rugby yenyewe ndio inashika namba nne kwa kujenga misuli na kumfanya mwanadamu kuwa imara kimwili na kiafya.

Zoezi namba tano huwa ni kutembea nako ni mojawapo ya zoezi ambalo linahusisha misuli mingi ya mwilini, kutembea umbali mrefu ndiko haswa kunakojenga mwili.Mtindo huu ndio unaowafaa watu wenye umri mkubwa wanaohitaji kujenga mwili wenye afya njema.

Utahitajika kutembea umbali wa wastani angalau kilometa mbili kwa siku katika siku tano za wiki huku ukitembea na kutupa mwili na mikono ili kuishughulisha misuli mingi ya mwili.

Mazoezi ndio chanzo cha kuwa na mwili imara wenye afya njema hivyo kuepukana na maradhi yasiyoambukiza ikiwamo kisukari cha aina ya pili, maradhi ya moyo, kiharusi na unene uliokithiri.

Hii ndio sababu inayochangia mamilioni ya wanamichezo duniani pamoja na wafanya mazoezi mepesi ya mara kwa mara kuishi kwa muda mrefu zaidi ukilinganisha na wasiofanya mazoezi.

Lakini swali la msingi zaidi je mazoezi haya yafanyike kwa muda gani ili kupata matokeo chanya? Kwa kifupi inashauriwa kufanya mazoezi haya yafanyike kwa siku dakika 30-60 katika siku 5 za wiki.

Vile vile inashauriwa kufuata mwenendo na mitindo bora wa kimaisha ikiwamo mlo kamili uliozingatia kanuni za lishe.

Mwenendo na mitindo mibaya ya kimaisha inayoweza kuchangia kutoweza kujenga mwili hata kama unafanya mazoezi haya ni pamoja ulaji holela wa vyakula vyenye mafuta mengi, wanga na sukari nyingi, unywaji pombe kupita kiasi na utumiaji tumbaku.

Vyakula hivi ambavyo hupatikana zaidi mitaani, katika migahawa ya kisasa hasa ya kimagharibi, vyakula vya kusindika hasa vile vinavyuouzwa katika maduka makubwa (supermarkets).

Vyakula hivi huchangia watu kunenepa na kuwa na uzito au unene uliokithiri hivyo kuharibu ule mwonekano wa ukakamavu wa mwili kutokana na mrundikano wa mafuta mengi.

CHUKUA HII

Kama unapenda kuwa na mwili uliojengeka zingatia mojawapo ya mazoezi haya au fika katika vituo vya mazoezi kwa ushauri zaidi.

Jipangie ratiba ya kufanya mazoezi haya mara kwa na kuwa sehemu ya maisha yako kwani si tu yanaujenga mwili kimazoezi bali pia kukufanya kuwa na afya njema.

Unaweza kuitumia simu janja yako kupakua zile apps zenye muongozo mzima wa mazoezi ya kujenga mwili.

Fika katika vituo vyenye wataalam wa lishe na mazoezi ya mwili kwa ajili ya ushauri zaidi na jenga utamaduni wa kusoma majarida ya Afya ili kujiongezea ufahamu zaidi.

Columnist: Mwanaspoti