Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mwamuzi wa Mwanza ametukumbusha maswali yetu

Mwamuzi Utata Mwamuzi wa Mwanza ametukumbusha maswali yetu

Tue, 1 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kitu ambacho kimefurahisha baada ya pambano la juzi pale Uwanja wa CCM Kirumba ni kwamba mashabiki wote wa soka nchini wamekubaliana kwamba penalti ya Yanga waliyopewa katika kipindi cha kwanza haikuwa sahihi. Ndiyo, haikuwa sahihi.

Wakati mwingine huwa tunabishana kuhusu uhalali wa penalti, kadi nyekundu, mpira uliotoka, mpira uliovuka mstari na mengineyo. Ni mara chache huwa tunakubaliana jambo moja halafu kwa pamoja. Penalti ya Yanga dhidi ya Geita Gold kipindi cha kwanza cha pambano hilo haikuwa sahihi.

Kilichofuata jioni ya juzi kilikuwa kichekesho kidogo. Mashabiki wa Yanga walikuwa wanajibu mapigo kwa kutuma video za watani wao Simba wakati wakipendelewa hapo nyuma. Kwamba wanataka kuhalalisha kosa kwa kosa. Hii inampa unafuu mwamuzi wa pambano la juzi, Florentina Zablon.

Kabla ya kuanza kujibu mapigo kutoka kwa watu wa Yanga, kabla Simba hawajamshambulia sana mwamuzi tukumbuke haya maswali matatu ambayo niliwahi kuuliza kwenye ukurasa huu. Waamuzi wetu wana mapenzi binafsi na timu? Wanachukua hongo? Au hawajui kutafsiri kanuni za mchezo wenyewe? Tukiwa bize na maswali haya tunaweza kupata suluhisho la matatizo ya waamuzi wetu.

Turudi katika tukio. Zablon alipaswa kuwa hatua kumi kutoka katika tukio. Kama alikuwepo katika hatua hizo ni wazi angeona kwamba mchezaji wa Geita aliunawa mpira, lakini haikuwa ndani ya boksi. Nadhani kamera za Azam TV nazo zinapaswa kututendea haki tuwe na kona tofauti za kuonyesha ni wapi mwamuzi alikuwepo na mpira ulikuwa wapi.

Lakini hata kama mwamuzi alikuwa mbali au alizibwa bado inampa nafasi mwamuzi msaidizi kumsaidia kutoa uamuzi. Zamani waamuzi wasaidizi tulikuwa tunawaita washika vibendera, lakini siku hizi wanaitwa waamuzi wasaidizi. Tunawaita hivyo kwa sababu kazi yao sio kutoa uamuzi unaohusu mistari tu, bali hata yanayotokea ndani ya uwanja. Sawa, Zablon hakuona, je mwamuzi msaidizi hakuona?

Tunakuja katika swali jingine. Waamuzi wetu huwa wanahongwa? Inawezekana. Sina uhakika kama Zablon alihongwa ili aitoe ile penalti. Sina ushahidi wa kutoa mahakamani kama akinishtaki. Lakini nina hisia kadhaa za kujiuliza.

Ingekuwa dakika za mwisho mwisho basi tungeweza kusema kwamba mwamuzi alihongwa. Inawezekana kwamba alikosa visingizio vya kutoa penalti kwa dakika nyingi za mchezo halafu akakutana na kisingizio hiki katika dakika mwisho. Lakini hii ilikuwa penalti ya kipindi cha kwanza. Alikuwa na muda wa kusubiri kuinyonga Geita katika kipindi cha pili. Kwanini aliharakisha?

Achana na hilo ukweli ni kwamba licha ya Yanga kuwatumia wachezaji wengi ambao hawachezi kila wiki katika kikosi cha kwanza, lakini walicheza vema kuliko Geita. Kwanini mwamuzi aharakishe kuinyonga Geita katika tukio la kijinga na asisubiri wakati tukio linalokaribia uhalisia litakapokijitokeza?

Sina jibu lolote katika haya, lakini kama mwamuzi alikuwa amehongwa basi nadhani hana hata akili ya kujua ni wakati gani wa kupendelea na hajui ni katika tukio gani linalokaribiana na uhalisia ambalo anapaswa kupendelea. Mtu mmoja aliwahi kusema ‘Hata matapeli walioishia darasa la saba wanatumia akili nyingi kuliko maprofesa’.

Swali hili la pili kwa waamuzi linafanana na swali la tatu. Je waamuzi wetu wana mapenzi na timu zao? Sawa, tufanye kwamba Zablon ni Yanga na ana mapenzi na Yanga katika mechi ambazo anachezesha, lakini unaweza kuhalalisha mapenzi yako kwa kitendo alichofanya? Inabakia akili ile ile kwamba kwanini hakusubiri tukio ambalo linafanana na uhalisia?

Tukifanikiwa kujibu maswali haya matatu huku tukimtumia Zablon kama mfano wa waamuzi wetu ambao wanaendelea kutuletea uamuzi mbovu katika soka letu nadhani tunaweza kupata suluhisho la msingi kuhusu utata wa uamuzi ambao umeendelea kuzingira katika soka letu. Tukileta ushabiki nadhani hata sisi tulio nje tutakuwa wajinga tu katika kuwajadili waamuzi wetu.

Tutafute suluhisho la uamuzi wao wanaofanya lakini kwanza tupata majibu ya uhakika kwamba waamuzi wetu wanahongwa? Wana mapenzi binafsi na timu, au hawaelewi kanuni? Baada ya hapo tuanze kuchukua hatua kwa kila jibu letu. Kama wanahongwa basi vyombo vya usalama vifanye kazi zao. Kama wana mapenzi binafsi basi wafungiwe maisha. Kama hawajui kanuni basi tuandae waamuzi wajao katika usasa zaidi.

Kwa mfano, kwa sasa imefikia mahali ambapo inatabirika kuwa mechi za Simba, Yanga na Azam zitachezeshwa na waamuzi fulani. Hii ni kwa sababu eti waamuzi wengine hawafikii ubora wao. Kwamba mechi hizo zitachezeshwa na Ramadhan Kayoko, Ahmed Aragija au Elly Sasii. Hii ni kwa sababu waamuzi wengine hawaaminiki kuchezesha mechi za timu hizi kubwa.

Hapo hapo unajiuliza kwamba kama waamuzi wengine hawawezi kuchezesha mechi hizi ina maana wakatibue mechi nyingine za Namungo dhidi ya Coastal Union? Hakuna mpira wa hivi duniani. Waamuzi wa Ligi Kuu wanapaswa kuwa na viwango sawa vya uchezeshaji.

Kinachosikitisha pia ni kwamba hata hao watatu wakati mwingine viwango vyao vinakuwa katika shaka. Mwamuzi bora wa msimu uliopita ni Aragija, lakini tayari ameshafungiwa kwa kuvurunda hivi majuzi. Kama hao tunaowana bora wana matatizo, vipi kwa kina Zablon?

Mwisho wa siku, mwisho wa kila kitu nadhani tusipopata majibu ya maswali haya matatu basi hatutapata majibu ya kwanini waaamuzi wetu huwa hawateuliwi kuchezesha michuano mikubwa kama ya Afcon au Kombe la Dunia. Sio tu kwa timu za wakubwa bali katika michuano ya wanawake na watoto.

Orodha zinapotoka kwa waamuzi wanaochezesha michuano mikubwa kama hii halafu hatuwaoni Watanzania huwa tunashindwa kukumbuka kujiuliza maswali matatu ambao nimeuliza. Hadi siku tutakapochukua hatua na kujibu maswali haya huku tukifanya utekelezaji wa upungufu wetu ndipo waamuzi wetu watakapoitendea haki ligi yetu na kuitwa katika michuano mikubwa.

Watu wanawekeza pesa zao lakini hali halisi ni kama hii tuliyoiona Kirumba katika pambano la juzi. Tuanze kujibu maswali.

Columnist: Mwanaspoti