Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mwamuzi mlokole mchukia rushwa - 8

FF6C7339 0E10 4BB5 8332 DCD5CFB684D5.jpeg Mwamuzi mlokole mchukia rushwa - 8

Thu, 12 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Tunaendelea na Ripoti Maalumu ya Waamuzi wa Ligi Kuu Bara pamoja na ligi nyingine za hapa nchini na tumekuwa tukipata maoni mengi ya wasomaji wetu kuhusu ripoti hii. Hili ni jambo zuri na linaonyesha kuna wasomaji wengi walitaka kufahamu kuhusu yale tuliyoripoti.

Jana tuliishia kwenye kipengele kinachoonyesha jinsi kuna waamuzi walikuwa bora kwenye ligi lakini ghafla wakapotea moja kwa moja na siku hizi hawaonekana tena sehemu ambayo tunaendelea nayo tena leo. Kipengele ambacho tuliishia nacho jana ni kile kinachomzungumzia mwamuzi Alex Mahagi kupewa taarifa ya uongo na Hassan Dilunga wa Yanga, huku mechi ikiwa inaendelea.

Neto alidai kiungo wa wakati huo wa Yanga, Dilunga alimpa mwamuzi taarifa za uongo dhidi yake, alikuwa ameficha kitu kinachodhaniwa ni hirizi kwenye sehemu zake za siri kitu ambacho si kweli.

“Refa alitaka kuingiza mkono kwenye sehemu zangu za siri ili kuthibitisha kama ni kweli, mimi nikagoma, aliendelea kusisitiza nikagoma kwani pale palikuwa ni uwanjani hivyo kwa hasira nikamfunulia ili aangalie, yeye aligoma na kunipa kadi ya pili ya njano ambayo ilizaa nyekundu,” alisema Neto. Hata hivyo, mwamuzi Mahagi alijitetea madai ya mchezaji huyo si ya kweli na alikuwa na kitu chenye ncha kali.

“Haikuwa kama ambavyo watu wanavyosema ni vitu vya kishirikina na wala sikutaka kuingiza mkono katika sehemu zake za siri, nilimlazimisha kutoa alichonacho ili niweze kujiridhisha juu ya alichoweka ndani ya bukta ambacho ukiacha wachezaji wa Yanga hata mimi kilinichoma.”

Baadaye Mahagi alisamehewa na kurejeshwa kuchezesha, hata hivyo hakudumu muda mrefu na akapotea lakini kwa sasa anaonekana kwenye mashindano ya ndondo.

MATHEW AKRAMA

Mmoja ya waamuzi waliokuwa vizuri uwanjani na moja ya sifa yake kubwa ambayo waliokuwa wakimfahamu walisema ni kuchukia rushwa huku wakimpachika jina la 'mwamuzi mlokole'.

Mwenyewe ameliambia gazeti hili tangu aokoke mwaka 2003 na kuanza kuchezesha Ligi Kuu Bara mwaka 2005 hajawahi kuchukua rushwa kwa timu yoyote ile ili kuisaidia uwanjani kupata ushindi.

Mechi yake ya mwisho kuchezesha kabla ya kuamua kustaafu ni mechi kati ya Simba na Azam iliyofanyika mwaka 2017 kipindi hicho Wallace Karia akiwa kaimu rais.

"Nimepumzika uamuzi kwa sababu ya umri. Kuna umri ukifika (miaka 45) unatakiwa kustaafu ila kama ukiona unaweza kuendelea pia sawa lakini mimi 2017 niliamua kustaafu tu maana niliona mambo yamekuwa mengi.

Akizungumzia kuhusu rushwa michezoni, Akrama anasema ni janga hasa kwenye Ligi Kuu Bara. "Matukio ya rushwa yamezoeleka na kuwa hali ya kawaida kwa mpira wetu tena, cha kushangaza timu kubwa zilizofanya usajili mkubwa ndio zinaongoza kwa matukio ya rushwa.

"Tangu niokoke mwaka 2003, sijawahi kukubali rushwa na hadi naanza kuchezesha ligi mwaka 2005 nilikuwa sipendi kabisa timu zinazotoa rushwa ili zishinde na nafikiri walikuwa wananijua vizuri na waliniita mwamuzi mlokole," anasema Akrama.

ODEN MBAGA

Mwaka 2018, Mwamuzi huyu ambaye aliwika kipindi cha Tenga na Malinzi alijikuta akifungiwa kifungo cha maisha na Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) kwa kujihusisha na masuala ya rushwa ya upangaji matokeo.

Baada ya uchunguzi uliofanyika kuanzia Julai 11,2018 Mbaga alikutwa na hatia ya kuhusika kwenye upangaji wa matokeo ikiwa ni kinyume na kanuni za Maadili za FIFA.

Mwamuzi huyo alifungiwa maisha kujihusisha na shughuli zozote za mpira wa miguu katika ngazi ya kitaifa na kimataifa kwa mujibu wa Ibara ya 7j ya Kanuni za Maadili za FIFA za mwaka 2018 pamoja na Ibara ya 22 ya Kanuni ya nidhamu ya FIFA.

Adhabu hiyo ilikuja baada ya Mbaga na wenzake Jesse Erasmo, Hamis Chang’walu walisimamishwa tangu mwaka 2014 kwa upangaji wa matokoeo.

Julai 24, 2014, rais wa wakati huo, Jamal Malinzi alitangaza kuwasimamisha waamuzi hao kwa tuhuma za kupanga matokeo, ambazo hakuziweka wazi. Huo ndiyo ukawa mwisho wa mwamuzi Oden Mbaga ambaye pia ana taaluma ya kuchezesha mchezo wa mpira wa kikapu.

JUDITH GAMBA

Mwamuzi huyu naye alitikisa kipindi cha utawala wa Tenga na hata Malinzi kwani alikuwa mwamuzi pekee wa kati wa kike kabla ya baadae kuja, Jonesia Rukyaa na sasa pia kaongezeka Frolentina Zabroni.

Hata hivyo, Judith hakuendelea tena kuchezesha ulipoingia madarakani uongozi wa Karia na taarifa zinasema hivi sasa ni kamishina wa mechi za Ligi Kuu.

TATIZO NINI?

Mmoja ya waamuzi ambaye hakutaka kutajwa jina lake anasema siasa ipo kila mahali hata katika uongozi wa soka kwani kila mtu anakuwa na watu wake wa kufanya nao kazi.

"Sasa swali ni je watu wake ni bora au anakuwa nao ili mradi wabebane?

“Kwa upande wangu mimi nilikuwepo tangu enzi za Tenga hadi sasa bado nipo, ni kazi ambayo naipenda, kuna wanaokata tamaa na kuamua kuachana na kazi ya urefa na kutafuta maisha mengine.”

“Kina Saanya, Jonesia, Eli Sasii na mimi bado tunapambana kujituma kwa kuamini katika wakati na ndio kitu pekee ambacho kimetufanya tufikie hapa lakini wengine walioamua kuishia njiani utakuta walikatishwa tamaa na utendaji wa viongozi na wengine waliona hawakui wanaishia kuwa chini, hivyo kuamua kukaa pembeni,” anasema mwamuzi huyo.

Anasema pia kuna changamoto ya wadada kuingia kwenye mahusiano ili waweze kupata nafasi lakini ambao hawawezi mambo hayo wanajiengua ili kutunza utu wao.

"Unakuta pia mwamuzi anapangiwa mechi zile zile siku zote na wakati anatamani kuchezesha mechi kubwa lakini anakosa nafasi hiyo, hivyo anajiona hawezi kukua anaamua kuchagua maisha mengine," anasema mwamuzi huyo.

NINI KIFANYIKE

Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Ally Mayay anasema ili kuiboresha sekta ya waamuzi nchini, inapaswa wawe na programu ambazo zitasimamiwa na chama.

"Chama cha waamuzi kinaongozwa na waamuzi ambao wengi wao wamestaafu, wanakuwa na uzoefu wa kutosha na kuwa na ufuatiliaji.

"Tunaona kwenye Chan, tumekosa waamuzi wetu kule, sio kama hatuwezi, la hasha! lakini hatujatengeneza programu nzuri ya kufika huko," anasema.

Anasema bajeti ya kufanya semina za mara kwa mara za waamuzi haikwepeki, pia lazima chama kiwe na mkakati, kila kitu cha waamuzi kitokee kwenye chama.

"Hata kama ikiwa ni TFF, lakini kupitia kwenye chama, wawe na mikakati, ikiwezekana waanze kutengeneza waamuzi vijana kuanzia miaka 18, hadi wakifikisha miaka 20, wanakuwa wameiva.

"Plani za muda mrefu lazima zitokee kwenye chama chao, huko ndiko kwenye msingi na walioko pale wamepitia kwenye fani wana uzoefu wa kutosha," alisema Mayay.

Omary Abdulkadir, mwamuzi aliyewahi kuchezesha fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), anasema ili kuondoa changamoto ya waamuzi nchini, kwanza ni wengi wao kukubali kuongeza elimu.

"Wengi hawana elimu kubwa, wanapaswa kujiendeleza zaidi katika fani yao, hiyo itawasaidia si tu kupata 'exposure', pia kujipambanua kwenye utendaji wao," alisema.

Columnist: Mwanaspoti