Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mwamuzi England analipwa Sh118 milioni - 9

Anthony Taylor  Tt Mwamuzi England analipwa Sh118 milioni - 9

Fri, 13 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Katika mlolongo wa Ripoti Maalumu ya Waamuzi Bongo, jana tuliisha kwenye sehemu ya jinsi waamuzi wengi wa Ligi Kuu Bara walivyopea kwenye ramani ya soka, huku wengine wakieleza jinsi ambavyo walilazimika kupotea.

Awali tulishaeleza kuhusu rushwa, kuhusu malipo yao, fitina na jinsi ambavyo wanapata beji za Fifa kwa jasho kubwa lakini mwisho unakuwa mbovu kwao, leo tunakuletea jinsi ambavyo waamuzi wa nchi za wenzetu wanavyofanya kazi yao, hususani Ligi Kuu England.

LINAPOKUJA suala la kuutambua kuwa soka ni mchezo wa pesa, basi wote wanaohusika kwenye mchezo huo ikiwamo waamuzi basi wafanywe kuwa watu rasmi katika mustakabali wa maendeleo ya mchezo huo.

Kwa kulizingatia hilo ndiyo maana Ligi Kuu mbalimbali za kutoka nchi zilizoendelea, hususani ile ya England imelifanya suala la waamuzi kuwa ni ajira rasmi na kwamba waamuzi wote wanalipwa mishahara ukiweka kando pesa za posho wanazopewa kulingana na mechi wanazochezesha.

Waamuzi ni watu muhimu sana katika maendeleo ya mchezo wowote na kwa sababu soka imekuwa ikihusisha mambo mengi ya michezo ya kamari, kumlipa mwamuzi mshahara kutampunguzia ushawishi wa kuchukua rushwa ili kuwa na upendeleo kwa baadhi ya maamuzi ndani ya uwanja.

Huko kwenye nchi zilizoendelea, kama ilivyo kwa wanasoka kwamba wanatambulika kuwa ni mastaa basi waamuzi nao ni mastaa, wanatambulika na kuheshimika kutokana na kazi yao wanayofanya, kwa sababu nayo inawaingizia mishahara ya kila mwezi na si kulipwa posho tu.

Kwenye Ligi Kuu England, waamuzi wote wanaochezesha ligi hiyo ni waajiriwa wa kampuni inayofahamika kwa jila la Professional Game Match Officials Limited (PGMOL). Mwanzoni ilikuwa ikitambulika kama bodi, Professional Game Match Officials Board (PGMOB). Tangu mwaka 2001, urefa kwenye soka la England ulitambulika kama taaluma na hapo wakatambulika kwa kupewa maslahi muhimu ikiwamo mishahara ili kuwafanya kazi ya uamuzi isiwe kibarua cha siku tu (deiwaka).

Kwa kuwekwa kwenye ajira maalumu kunafanya waamuzi wengi kuwa makini ndani ya uwanja kwa sababu ni kazi kama ilivyo kazi nyingine. Na kundi la waamuzi ambao wapo kwenye ajira wamekuwa wakikutana mara mbili kwa mwezi kwa ajili ya kufanya mazoezini na kupitia video mbalimbali za mechi walizochezesha ili kutathmini viwango vyao.

PGMOL imekuwa na udhamini wa kampuni mbalimbali, ilianza na Air Asia kabla ya kubadili msimu wa 2010-11 na kudhamiwa na Tune Group. Msimu wa 2012-13 wadhamini wao walikuwa Expedia, lakini makubaliano yao yalifika ukingoni baada ya mwaka mmoja tu. tangu mwanzo wa msimu wa 2013-14, PGMOL imekuwa haina mdhamini, lakini wana makubaliano na EA Sports wakiweka logo yao mikononi kwenye jezi za waamuzi hao.

Kitendo cha kuwafanya waamuzi kuwa mastaa ndicho kitu kinachowafanya watu kama Michael Oliver huko kwenye Ligi Kuu England kutambulika zaidi, sambamba na wengine kama Anthony Taylor. Na kitu kizuri zaidi, waamuzi hao wanalipwa mishahara kila mwezi.

Kwenye Ligi Kuu England, ligi ambayo hutazamwa zaidi hapa nchini, waamuzi wake wanalipwa mishahara ya kila mwezi ukiweka kando posho za kila mechi wanazopangwa kuchezesha.

Ripoti zinafichua kwamba waamuzi wa soka wa Ligi Kuu England wanalipwa mishahara kati ya Pauni 38,500 na 42,000 – kulingana na uzoefu wao wa kuchezesha mechi. Pauni 38,500 ni zaidi Sh109 milioni kwenye pesa za Kitanzania. Kwa wale wanaolipwa Pauni 42,000 hiyo ina maana anapokea zaidi ya Sh118 milioni. huo ni mshahara wa mwamuzi England.

Na waamuzi hao, wanapewa Pauni 1,150 nyingine ya ziada kila anapochaguliwa kucheza mechi, jambo linalomfanya refa mmoja wa Ligi Kuu England kuvuna hadi Pauni 70,000 kwa mwaka, ambayo ni sawa na Sh 198 bilioni za Kitanzania.

Kwa waamuzi wanaochezesha kwenye Championship, mishahara yao inafanana na ile wanayolipwa waamuzi wa Ligi Kuu England, lakini hawa wa ligi hiyo ya Championship wanalipwa Pauni 600 kama posho wanapochezesha mechi.

Katika ligi cha chini kabisa kwenye soka la England, waamuzi wanalipwa posho za kila mechi ambazo ni Pauni 80 huku wakilipiwa gharama nyingi ikiwamo za usafiri na malazi. Pauni 80 ya posho anayolipwa mwaamuzi wa ligi za madaraja ya chini kabisa England ni sawa na Sh 226,374 za Kitanzania.

Na kula mchangani kabisa, kwenye ngazi za chini kabisa ikiwamo ligi za watoto, waamuzi wanalipwa kati ya Pauni 20 na Pauni 40 kwa mechi.

WAAMUZI WA LIGI NYINGINE ULAYA WANALIPWAJE?

Wakati waamuzi wa soka la England wakilipwa mishahara, ligi nyingine kubwa za Ulaya zimebuni utaratibu uliobora kabisa wa kulipa ujira marefa wake badala ya kuwalipa kutokana na mechi.

Huko Hispania, waamuzi wanalipwa Pauni 5,200 kwa kila mechi, hiyo ina maana kwa mwamuzi wa La Liga anaweza kulipwa zaidi ya Pauni 140,000 kwa mwaka. Pauni 140,000 ni sawa na Sh396 milioni.

Ujerumani kwenye ligi ya Budesliga waamuzi wanalipwa Pauni 3,150 kwa mechi (Sh8.9 milioni), wakati kwenye Serie A huko Italia, ambako waamuzi wake ni maarufu kwa kuvaa jezi za njano, wao wanalipwa Pauni 3,000 kutokana na kuchezesha mechi za ligi hiyo. Pauni 3,000 ni sawa na pesa ya Kitanzania, Sh8.5 milioni.

Waamuzi wa Ufaransa, ambako mastaa kama Lionel Messi, Kylian Mbappe na Neymar wanapiga mzigo katika Ligue 1, wao wanalipwa Pauni 2,400 kwa kila mechi, wakati Ureno mwamuzi analipwa Pauni 1,000 kwa kila mechi atakayochezesha.

LIGI YA MABINGWA ULAYA WAAMUZI WANALIPWA NINI?

Waamuzi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya wamegawanywa kwenye makundi kulingana na uzoefu wao na viwango. Waamuzi waliowekwa kwenye daraja la juu kabisa (Elite) wao wanalipwa zaidi ya Pauni 5,500 kwa kila mechi wanazochezesha kwenye michuano hiyo ya Ulaya na kundi hilo lina waamuzi makini kama Danny Makkelie na Felix Brych.

Waamuzi waliopo kwenye kundi la wanaofahamika kama Elite wao ni wale wenye uzoefu wa kuchezesha kati ya miaka mitano hadi saba katika ligi za nchi zao na wao wanapewa kuchezesha mechi kubwa za hatua ya makundi na mtoano.

Kundi la pili kwenye viwango hivyo vya waamuzi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, (Elite development) wao wanalipwa Pauni 3,800 kwa kila mechi wanazochezesha kwenye michuano hiyo ya Ulaya, wakati wale wa kundi la chini kabisa wanalipwa Pauni 700 kwa kila mechi na wao mara nyingi wanachezesha zile mechi za raundi ya awali kabisa.

Columnist: Mwanaspoti