Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (19922-1999)

Mwl. Nyerere Fimbo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (19922-1999)

Wed, 12 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Watanzania wakiwa katika maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 23 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, ifikapo Ijumaa Oktoba 14, wanakumbushwa kuwa njia bora ya kumuenzi ni kudumisha uzalendo, upendo kwa taifa bila kujali kanda, mkoa wala kijiji kiongozi ulipozaliwa.

Mwalimu anasifika kwa uzalendo na mtu mwadilifu anabakia kuwafundisha Watanzania kuacha kujipendelea, ubinafsi  na kuwa wazalendo wa vitendo kwa taifa lao.

Mwanasiasa mkongwe Stephen Wasira, ndiye anayesema hayo katika mazungumzo yake na gazeti hili wiki hii kuzungumzia kumbukumbu ya maisha ya Mwalimu, huku akifafanua kuwa baadhi ya watu wakiwamo pia viongozi, hawafuati misingi alioiasisi, hasa ya kulitumikia taifa kwa uadilifu mkubwa.

"Baba wa Taifa alitaka maendeleo ya Watanzania, si kwa ajili yake  ndiyo maana alikataa barabara ya kutoka Makutano hadi Butiama ijengwe kwa kiwango cha lami licha ya kwamba alikuwa na uwezo ,"anakumbusha Wasira.

Anafafanua kuwa ilikuwa ni mwaka 1974 aliombwa kujengewa barabara ya kutoka eneo la Makutano, yenye urefi wa kilomita 24 hadi nyumbani kwake Butiama lakini akakataa, akiwa  na sababu moja kuwa yeye ni Rais wa Tanzania siyo wa Butiama.

Wasira anasema badala yake Baba wa Taifa alitaka barabara za lami kwa ajili ya kuunganisha mikoa, ili kuharakisha maendeleo, si sehemu moja ya mkoa kama kutoka eneo la Makutano kuishia nyumbani kwao Butiama pekee akieleza kuwa, ujenzi huo usingekuwa na tija kwa mamilioni ya wananchi waliokuwa hawana barabara katika mikoa hiyo.

"Baba wa Taifa alitamani hata yeye yupo au hayupo duniani, Watanzania wote waendelee kufurahia maendeleo ya nchi yao na si watu wa eneo moja la nchi ama Butiama na mkoa wa Mara kwa ujumla, kuwa na huduma mbalimbali kisa tu yeye amezaliwa huko.

Wasira anasema alitaka barabara ya lami isiishie Butiama, bali iende Nyamuswa, hadi Kijiji cha Sanzati na kisha iunganishwe na mji wa Mugumu wilayani Serengeti na kuwa kiungo kati ya mkoa wa Arusha.

Hata hivyo, anaongeza kuwa Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, sasa ni marehemu aliamua kujenga kilomita 24 za barabara lakini baada ya kifo cha Baba wa Taifa ili baadaye ujenzi zaidi uendelee hadi Mugumu, ili kuunganisha Mara na Arusha.

Katika moja ya mahojiano na wazee wa Butiama waliwahi kuieleza Nipashe kuwa wananchi wa Butiama waliwahi kumhoji kuwa akiwa mzaliwa wa mkoa wa Mara amewafanyia nini watu wa mkoa wake?

Wanasema kuwa Mwalimu aliwajibu kuwa yeye si Rais wa Wazanaki wala Butiama bali ni kiongozi wa Tanzania na kila mmoja anamtazama , akitaka amfanyie jambo, hivyo anawajibika kwa taifa zima siyo kijijini alipozaliwa.

KUKAMILISHA UJENZI

Mwanasiasa Wassira ambaye alifanyakazi wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, anasema, baadaye ujenzi wa barabara hiyo ili kutimiza lengo la Baba wa Taifa la kuunganisha mikoa ulianza, lakini anadai kuwa unasuasua na haijulikani utakamilika lini.

Ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kutoka Butiama kupitia Nyamuswa hadi Kijiji cha Sanzati, ulianza lakini  kwa kusuasua.

"Umbali kutoka eneo la Makutano hadi Kijiji cha Sanzati, ni kilomita 50, lakini zilipungua baada ya kujenga barabara hiyo hadi Butiama, hata hivyo hizo kilomita 36 zilizobaki imeshindikana kuzimaliza kwa miaka saba," anasema Wasira.

Anadai mbali na ujenzi huo kuchukua miaka mingi, hauko kwenye kiwango na kwamba ipo haja kwa viongozi wa serikali kufuatilia kwa karibuni kubaini ni kasoro gani na kuchukua hatua.

Wasira anasema ubinafsi huchangia kwa kiasi kikubwa kuwapo kwa mfarakano kwa wananchi kati ya aliyekuwa nacho na asiyekuwa nacho,  na kwamba Baba wa Taifa aliliona hilo na kulikemea kwa nguvu zake zote.

"Kama Baba wa Taifa angekuwa mbinafsi, Butiama isingekuwa kama ilivyo sasa, angelikuwa na sura nyingi kuanzia miundombinu bora, majengo, upendeleo wa kielimu, tiba na hata utajiri wa kutisha maana rasilimali zote za taifa  zilikuwa chini yake na maamuzi yake yasingepingwa.

“Hivyo basi tumheshimu Mwalimu hata barabara hii aliyotamani iunganishe Mara na mkoa wa Arusha ingejengwa kwa viwango na kwa wakati, ili kumuenzi Mwalimu," anasema Wassira.

Anaeleza kuwa kwa sasa kiwango cha uzalendo kinaendelea kushuka kwa  watu wengi na kwamba hali hiyo ni hatari, kwa kuwa raia wa aina hiyo kimsingi wanashindwa kumuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo hasa wanapokuwa viongozi.             

MAONO ZAIDI

Wasira anasema mbali na kuiunganisha Tanzania, anasema Baba wa Taifa alikuwa na maoni mengi na kwamba alipenda kuiona Afrika inaungana na kuwa moja. Lakini alipingana na Kwame Nkrumah wa Ghana katika suala hilo.

"Alitaka hatua ya kwanza iwe kuungana kwa nchi za Afrika Mashariki, Kusini, Kati na Magharibi  na kuunda jumuiya za kikanda.

Wakati akiwa na fikra hizo , Rais wa zamani wa Ghana Kwame Nkrumah alitofautiana naye akipendekeza kuungana kwa nchi zote za Afrika kwa wakati mmoja na kushirikiana kwa kila hali. 

Kwa kushirikiana wamekuwa viongozi wakuu wa Afrika kwani ndiyo  waliounda Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mwaka 1963.

Mwanasiasa huyo anafafanua kuwa katika harakati zake hizo, Baba wa Taifa alianzisha Ujamaa wa Afrika uliojaribu kujumuisha mfumo wa maisha wa Kiafrika wa kuishi kwa pamoja na siyo kila taifa lijiangalie lenyewe na kiubinafsi. Ni mfano wa mzalendo, asiyejali Butiama bali Tanzania kwa ujumla lakini pia akitazama pia maslahi ya Afrika nzima.

Wassira anakumbusha:"Alijadiliana na Jomo Kenyatta, na kuna wakati alikuwa tayari kumpa nafasi Kenyatta kuwa kiongozi wa Afrika Mashariki yote. Alikuwa tayari hata kuusogeza mbele uhuru wa Tanganyika, na kuzingojea nchi nyingine tatu za Afrika Mashariki kupata uhuru kwa matumaini ya kuungana pamoja baadaye kuwa na maendeleo makubwa wananchi wao waliyoyatamani."

Anaongeza kuwa juhudi zake hazikuungwa mkono na baadhi ya viongozi wenzake wa Afrika, akaelekeza nguvu katika kuyaunganisha makabila mbalimbali ya Tanzania kwa kutumia Kiswahili kama lugha ya taifa.

Maelezo ya Wasira yanazigusa Wakala wa Barabara wa Taifa (TANROADS) na Mijini na Vijijini (TANROADS) kuijenga na kuikamilisha barabara hiyo ambayo pamoja na kuunganisha Arusha, Mara na Manyara ni kazi aliyoianzisha na kuitamani Mwalimu Nyerere japo hakuweza kuijenga.

Columnist: www.tanzaniaweb.live