Klabu ya KMC haina mwenendo mzuri kwenye Ligi Kuu Bara ambapo inashika nafasi ya 12 ikiwa na pointi 23, imecheza mechi 22, ushindi tano, sare nane, imepoteza tisa matokeo ambayo yanaifanya iwe miongoni mwa timu zinazopambana kujinasua kushuka daraja au kucheza mtoano (play off).
Mwaka jana, klabu hiyo iliajiri mtendaji mkuu mpya, Daniel Mwakasungula akichukua mikoba ya Walter Harison ambaye alinyakuliwa na Yanga alikokwenda kuwa meneja wa mabingwa hao watetezi wa ligi.
Hivi karibuni, Mwakasungula alifanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti ambapo alieleza kinachompasua kichwa ndani ya timu hiyo kuwa ni matokeo mabaya wanayoyapata. Endelea naye
MATOKEO YA TIMU
Mwakasungula anaanza kwa kuvuta pumzi: “Aaah hakuna kitu kinachoninyima usingizi kwa sasa kama matokeo tunayoyapata. Aisee yananivuruga ingawa tulianza na msimu mzuri, ilikuja kivingine ila tulikutwa na majeruhi wengi.
“Wachezaji saba wa kikosi cha kwanza walipata majeraha. Tunasajili wengi lakini unakuta wale waliopo wanatoa mchango, lakini tofauti na wale wanaokuwa kikosi cha kwanza tayari.
Timu ilianza kupambana na kurejea taratibu maana wanapotoka kuuguza majeraha sio rahisi kuanza kwa kasi moja kwa moja, na wanaoingia nao wanaingia taratibu kwenye mfumo.
“Kwa sasa tunaangalia benchi la ufundi linafanya nini ili tuwape sapoti. Tupo pamoja na timu kuhakikisha hatushuki daraja. Ndani ya timu yetu hakuna tatizo lolote na ni miongoni mwa timu zinazolipa wachezaji wao kwa wakati. Sio wachezaji pekee hata wafanyakazi wote ili kuleta motisha ndani ya timu, hivyo pesa haichangii kupata matokeo haya.
“Tulitambua tangu mwanzo kwa kutengeneza plani kuwa tunaenda kwenye ligi ambako tutakutana na nyakati mbalimbali ambazo ndizo kama hizi, hivyo tunapaswa kushikamana kwa pamoja kuitoa KMC hapa ilipo.”
UWANJA
Kuhusu uwanja wao unaojengwa Mwenge, Kinondoni bosi huyo anasema: “Ni zaidi ya asilimia 80 umekamilika. Tunawashukuru viongozi wetu wa Manispaa ya Kinondoni akiwemo mkurugenzi na mstahiki meya. Ni viongozi ambao wamekuwa na maono mazuri, uwanja wetu unakwenda kuongeza thamani kwenye timu.
“Uwanja utaanza kutumika msimu ujao maana kuna vitu vichache tunamalizia. Ujenzi wa uwanja unahitaji vitu vingi sana na michakato, hivyo ni lazima ujengwe kwa awamu ili kuwa bora zaidi, vitu kama ‘pitch’, mageti, uzio, vyumba vipo tayari.
“Utakuwa uwanja wa kipekee sana na wa kisasa. Kuna eneo la biashara pia ndio maana kuna flemu za kisasa za ghorofa, ungekuwa uwanja pekee yake ungekuwa umekamilika lakini huu umejengwa kisasa zaidi kila mmoja atafurahia uwanja huo na utaongeza uchumi kwetu.
“Mchakato wa hosteli pia upo ambazo zitakuwa nje ya uwanja, ila zitakazokuwepo ndani ya uwanja zitakuwa kwa ajili ya timu zetu za vijana.”
NDANI YA UONGOZI
Akizungumzia suala la uongozi, anasema: “Ukiwa kiongozi lazima uwe na ngozi ngumu. Huwezi kumshushia mtu wala kumwachia mtu, likija jema na baya lazima uyapokee yote. Mabaya zaidi ndiyo yanayokufungua katika kufanya mapema, kuliko kupata mema zaidi tu utajisahau.
“Ukipata taarifa ambayo hukuitegemea lazima ikushitue kidogo. Hata mimi ilinipa wakati mgumu kuikubali nafasi hii kwani nilikuwa nimeshatoka kwenye mpira muda mrefu, lakini baadaye niliona ni sehemu ya kupiga hatua.
“Nilikutana na watu walionitangulia kwa muda mrefu na wamefanya mambo makubwa ndani ya hii timu, sasa hivi nimekuwa mzoefu, vitu vingi navifahamu, ukiwa nje unaviona vitu unatamani kufanya.
“Hata nilipokuwa Mbeya City nilikuwa msemaji msaidizi, nikakaimu pale kwenye benchi kama meneja ingawa napo huwezi kujua mambo mengi, nilikutana na wadau wengi katika soka ninaofahamiana nao na wamenipa ushirikiano mkubwa. Sasa hivi naona kazi ni nyepesi tu.”
Mwakasungula anasema timu yao inaendeshwa kwa ruzuku kutoka Manispaa ya Kinondoni ambao ndio wenye timu, wadhamini wao binafsi na wale kutoka kwenye ligi na magawio ya haki za matangazo ya televisheni kila mwezi.
TIMU ZA VIJANA
“Tuna timu za vijana za U-17 na U-20, wanafanya mazoezi uwanja wa Bora pale Kijitonyama na wana mpango mkakati wao ambao wameuweka.
“Tunakwenda kuongeza timu yetu ya wanawake, ni rahisi kupata kwasababu Halmashauri ya Kinondoni inamiliki shule nyingi hivyo hawa wachezaji wetu wanapatikana humo ndio maana hatuiti wachezaji kwenye majaribio, tunataka kuwafanya wananchi wa Kinondoni waione timu ni ya kwao.
“Vipaji vipo vingi na kazi kubwa ni kuhakikisha tunaviendelea ipasavyo, tumepeleka pendekezo kwenye bodi ya timu ili waangalie nao watupe mapendekezo ndipo tuanze mchakato.”
AMBULANCE vs MATOKEO
KMC wanalalamikia kuwepo kwa gari la wagonjwa (ambulance) kwenye mechi yao dhidi ya Ruvu Shooting iliyochezwa katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro kuwa haikukudhi vigezo.
“Kanuni ya 17 ya ligi iko wazi juu ya huduma ya kwanza. Matokeo hayahusiani na gari la wagonjwa ukiachilia mbali wachezaji kuumia lakini kuna mashabiki pale, maana lolote linaweza kutokea lakini linapokosekana inaweza kuleta maafa.
“Gari linatakiwa kukaguliwa, lakini siku ile halikukamilika maana hata kulikagua hawakuruhusu. Hii sio kwetu tu bali hata michezo mingine, kwenye soka ni uhuni, tulisema tucheze ili baadaye tupelekea malalamiko mahala husika.
“Ruvu si mara ya kwanza, waliwahi kufanya hivyo walipocheza na Prisons wakapokonywa pointi, ‘fair play’ sio kucheza tu bali hata mambo kama haya, hawatukomoi sisi bali hata wao wana wanachezaji, je wakiumia inakuwaje.
“Tumeiachia mamlaka ili waone, ukipeleka malalamiko na mlalamikaji anapaswa kuhojiwa kwa kupeleka vielelezo, majibu yatakayokuja ndiyo tutajua tunafanyaje. Gari halikuwa na chochote. Watu wanapambana kupandisha ligi kila siku lakini kuna wengine wanapambana kuirudisha nyuma, wachukuliwe hatua stahiki,” anasema Mwakasungula
RATIBA
Akizungumzia ratiba, Mwakasungula anasema: “Tunachagua uwanja wa kucheza ili kuwapa fursa mashabiki wengine kuona mechi za ligi, lakini huwa tunafuata taratibu za kikanuni na hadi wenye mpira wakubali kuihamisha hiyo mechi.
“Huwa tunaenda sana Mwanza kwa sababu wachezaji wetu wengi wanatoka huko hivyo tunataka watu wa kwao nao wawaone vijana wao.
“Ratiba ni ngumu lakini hakuna budi kuifuata, tuna mechi ngumu mbele yetu Yanga, Azam na Geita ambazo zitachezwa hapa hapa Dar es Salaam, ni ngumu ila tunajipanga namna ya kupata pointi.” anasema.