Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mvutano CWT, Chakumwata *Walimu hawa wakimbilie wapi?

13757 Pic+cwt Mvutano CWT, Chakumwata *Walimu hawa wakimbilie wapi?

Tue, 23 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WALIMU wana malalamiko kadhaa ambayo yanawafanya wasiridhike na asasi zinazosimamia maslahi yao, wakiamini kwamba hayapatiwi ufumbuzi na kusababisha wengine kufikiria kujitoa uanachama wa taasisi hizo au kufuata utaratibu mwingine.

Ndiyo maana hivi karibuni changamoto za kutorodhika na makato ya michango yao zimesababisha baadhi ya walimu kuibuka na chama kingine kwa ajili ya kutetea maslahi yao.

Malalamiko ya makato ya asilimia mbili ya mshahara kwa kila mwanachama na mchango wa rambirambi wa Sh. 200,000 zinazotolewa na Chama cha Walimu (CWT) mwanachama akifariki na kuzawadiwa mabati 20 akistaafu wanaamini kwamba, kiasi hicho hakitoshi ikilinganishwa na michango ambayo wamekuwa wakitoa katika chama hicho, pia mabati 20 ambayo mwanachama hupewa kama zawadi anapostaafu nayo hayatoshi.

Mbali na hayo, walimu wamekuwa wakidai kwamba, wakati mwingine hata hayo mabati 20 hayatolewi kabisa na kusababisha kuwapo kwa malalamiko yasiyoisha ndani ya CWT.

Ndiyo maana wapo baadhi ya walimu waliamua kuanzisha chama kingine kiitwacho Chama cha Kutetea Haki na Maslahi ya walimu Tanzania (Chakamwata), ambacho kinapingana na CWT.

KUWAPO KIZUNGUMKUTI

Katibu Mkuu wa Chakamwata, Meshack Kapange, anadai kwamba walimu wengi siyo wanachama wa CWT na hawajawahi kuwa wanachama wa kisheria hivyo kuwakata mishahara yao kunazua jambo.

"CWT ilitumia nafasi ya kuwa chama pekee cha walimu kwa kuagiza makato ya asilimia mbili kwenye mishahara ya walimu wote nchini, siyo kama ada ya uanachama," anasema Kapange.

Anaongeza kuwa wengi na hususan walimu, wamekuwa wakihoji na kutafuta ukweli kuhusu mazingira na matukio yaliyosababisha kuanzishwa kwa CWT na madai mengine muhimu kwa maslahi ya wanachama.

"Hiyo ndiyo iliyosababishwa kuanzishwa kwa Chakamwata kwa ajili ya walimu wote wanaopenda kuona malalamiko yao yanapatiwa ufumbuzi wa kudumu ingawa safari yetu ina vikwazo vingi," anasema.

Anasema, chama hicho kinajulikana na kinaendelea kufanya taratibu za kujitambulisha mikoani na kusajili wanachama.

Wanachama hao wanasajiliwa kwa mujibu wa taratibu za sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini namba 6 ya mwaka 2004 na kanuni zake za mwaka 2007.

Katibu mkuu huyo anasema, Chakamwata kilipata usajili rasmi Machi 18 mwaka 2015, kwa lengo la kuwa mbadala wa CWT katika kutetea maslahi ya walimu nchini.

Baadhi ya wanachama (majina tunayo), wanazungumzia ubadhirifu na matumizi ya kufuru ya pesa za chama wakitaja kufanya burudani nje ya nchi na madai ya kuwapo kiburi na dharau kwa walimu.

Aidha, bungeni wabunge walihoji taarifa za jengo la Mwalimu House mali ya CWT na kueleza kuwa kuna benki imepangisha na wapangaji wengine lakini haijulikani pesa za mapato zinaratibiwa na nani.

Kadhalika walimu hao wanalazimishwa kuingizwa kwenye chama cha kuweka na kukopa (Saccos ya Walimu) bila utaratibu wa kisheria na unaoelweka.

MTAZAMO CHAKAMWATA

Anasema, pamoja na CWT kufanya uchaguzi wapya, bado malalamiko ya walimu yatakuwa pale pale na kwamba yanaweza kuisha iwapo chama mbadala na serikali vitashirikiana kuyatatua.

"Chama chetu kimeanzishwa kwa ajili ya kutetea maslahi ya walimu, hivyo bila chama hiki, ninaamini kwamba malalamiko kuhusu maslahi ya walimu yataendelea kuwapo," anasema.

Kapange anadai kwamba, hiyo ni kwa sababu haoni kama CWT inaweza kuwavusha walimu na kuwafikisha katika hali bora na kufanya kazi yao bila manung’uniko.

"Serikali inapofikia kuitaka CWT kuchagua viongozi bora na waadilifu, maana yake ni kwamba imeiona kuna jambo haliko sawa na ndiyo maana sisi tukaainisha chama hiki baada ya kuona kero za walimu hazitatuliwi," anasema.

Anasema, malalamiko ya walimu hayawezi kutatuliwa na CWT kwa madai kwamba chama hicho ni sehemu ya matatizo ya kuendelea kuwapo kwa malalamiko hayo yasiyo na mwisho.

Kauli hiyo inaonyesha kuwa viongozi wapya wa CWT wana kazi kubwa ya kuunganisha walimu na kusimamia maslahi yao, ingawa Chakamwata haiamini kwamba hilo litawezekana.

CWT WANASEMAJE?

Kwa upande wa CWT imepata viongozi watakaoiongoza kwa miaka mitano ijayo, wakiwamo wale waliotetea nafasi zao baada ya uchaguzi uliofanyika hivi karibuni.

Katika mazungumzo yake na gazeti hili, Katibu Mkuu wa CWT, Deus Seif, anasema, chama kitaendelea kusimamia katiba, kanuni, taratibu na sheria zake kwa maslahi ya wanachama kama ambavyo imekuwa ikifanya.

Hata hivyo, akijibu malalamiko ya kutoa Sh. 200,000 za rambirambi ya mwanachama akifariki dunia, kuchelewesha au kutotoa bati 20 za kiinua mgongo na malalamiko ya kukata asilimia mbili ya mshahara, hakuwa tayari kuzungumzia kero hizo.

Licha ya kwamba kuna malalamiko mengi na maswali kwa CWT, Seif anaahidi kuwa wataongoza chama kulingana na katiba yao.

Anaongeza:"Kwanza kabisa sihitaji kuzungumzia Chakamwata, bali sisi ni viongozi tuliochaguliwa tutaendelea kusimamia wajibu wetu bila kutoka nje ya katiba, kanuni,taratibu na sheria."

Anasema, walimu wote ni wamoja na wanatakiwa kuungana na kufanya kazi inavyotakiwa huku wakitambua kuwa lengo ni kuinua kiwango cha elimu nchini, lakini pia wakipata maslahi yao inavyotakiwa.

Anasema, hakuna haja walimu kutengana wakati wanajenga nyumba moja ambayo ni maendeleo ya elimu nchini, hivyo ni vyema wadau wote ambao kimsingi ni walimu, wakalitambua hilo.

"Sisi walimu tuna jukumu kubwa la kuhakikisha Tanzania inakuwa na wasomi kuanzia ngazi ya chini hadi taifa, hivyo suala la kuwa wamoja ni la muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu," anasema Seif.

Columnist: www.tanzaniaweb.live