Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Muungano unavyoboreka raia wataupenda zaidi

MUUNGANO Muungano unavyoboreka raia wataupenda zaidi

Wed, 6 May 2020 Chanzo:

MAADHIMISHO ya miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika mwaka 2017, yalikuwa na kiu ya kusikia kile serikali ya Rais John Magufuli, itakachosema kuhusu hatma ya Muungano.

Lakini Rais hakufanya ajizi aliweka bayana kuwa hakuna kitakachouteteresha Muungano na akazizika ndoto za kuunda serikali tatu na fikra za kuufanya uwe wa shirikisho ama wa kimkataba.

Alitangaza hayo katika hotuba yake aliyotoa Dodoma Aprili 2017 na kuweka wazi kuwa wenye nia za kuwa na sura nyingine ya Muungano hawatapewa nafasi hivyo, wauache ukae ulivyo na pia anawahakikishia Watanzania Bara na Zanzibar kuwa ataulinda kwa nguvu zake zote na iwapo atatokea mjanja kutaka kuuvunja ataanza kuvunjika yeye kwanza, kabla hajatimiza azma hiyo.

Kwa hiyo hatataka kusikia habari za kuuvunja, kuufanya wa mikataba, wa serikali tatu au shirikisho kama ambavyo wapo wanasiasa, wasomi na raia wanaotaka kuubadili.

Rais anaonyesha ni jinsi gani Muungano ni wa muhimu zama hizi na anaangalia jinsi ambavyo dunia ya leo inahitaji kuendeleza miungano na kuachana na hisia za kuuchukia ama kuulaumu mtangamano na ushirikiano wa kitaifa na kimataifa.

Hisia za kuwa na umoja si za Tanzania na Zanzibar pekee bali ziko miongoni mwa wananchi wa madola makubwa ambayo yamekomaa kiuchumi, kisiasa na kitekinolojia.

Hata hivyo dunia leo inajadili kuwa na mtangamano na ushirikiano wa kikanda kwa mfano , madola makubwa ya Ulaya kama Ujerumani, Ufaransa, Uholanzi na Hispania yanaendelea kujishikilia kwenye Umoja wa Ulaya (EU), licha ya kwamba yana uchumi mkubwa na yanaweza kujitegemea.

Madola ya EU yana sarafu ya Yuro iliyoanza kutumiwa tangu mwanzoni mwa mwaka 2000, wakati hayo yanatokea madola makubwa na yenye uchumi mkubwa ya Ujerumani na Ufaransa pamoja na Uholanzi yaliachia sarafu zake na kuingia kwenye Yuro ili kudumisha umoja na kuwa na fedha yenye nguvu duniani jambo ambalo linatokea sasa ni Yuro kuwa moja ya sarafu zenye nguvu ikichuana na Dola .

Pamoja na sarafu nchi hizo zina visa moja iitwayo Schengen Visa, inayotumiwa na nchi zote wanachama wa mataifa hayo.

Yuro moja ni zaidi ya Sh 2,400 za Tanzania wakati Dola nayo ni karibu sawa na kiwango hicho.

Kwa hiyo Afrika chini ya Umoja wa Afrika (AU) inasisitiza suala la mtangamano wa Afrika na kuwa na sarafu moja , soko la pamoja, pasi moja ya kusafiria, Afrika bila mipaka na shirikisho la kisiasa kupitia kile kinachoitwa The Africa We Want au Agenda 2063 ambayo ni suala la mtangamano uliokamilika.

Kwa hiyo si suala la Watanzania tena kupinga Muungano na kutaka kuwe na serikali tatu, mara uwe wa mikataba na wengine wakitaka iitishwe kura ya maoni kuamua uondoke ama ubakie.

Rais Magufuli anaona kuwa dunia ya zama hizi ni ya ushirikiano siyo ya kutaka kubomoa au kutengana, ndiyo maana katika jitihada za kushirikiana Tanzania ni mwanachama wa mtangamano wa Afrika Mashariki, kadhalika yupo kwenye ushirikiano wa Nchi za KUsini mwa Afrika (SADC).

KUUNGANISHWA KIHISTORIA

Ni wazi kuwa panapokuwa na muungano uwe wa EU au wa Tanganyika na Zanzibar kuna mambo ambayo historia inayaunganisha.

Kwa mfano Ulaya inaunganishwa na kumbukumbu za vita vikuu vya dunia hasa vita vya pili vilivyoangusha dola la Adolph Hitler wa Mjerumani na Uingereza kutwaa enzi.

Hayo yalibadilisha sura ya umiliki wa makoloni kwa Tanzania iliyokuwa chini ya Ujerumani ilichukuliwa na Umoja wa Mataifa na kuwekwa chini ya uangalizi wa Waingereza.

EU inaungana ili kulinda na kuepuka uhasama, ikitaka kudumisha amani na kuendeleza mshikamano miongoni mwa wanachama. Huo ni ukweli kwa vile tangu vita hivyo hakujawa na mapigano mengine wala uhasama miongoni mwa wana EU.

Umoja wa EU ni chipukizi linalokomaa zaidi kwa sababu ya kifo cha Jamhuri za Umoja wa Kisovieti zilizokuwa zinaongozwa na Urusi ambazo zilianguka kuanzia 1994. EU kihistoria inafahamu kilichoiua Urusi , hivyo madola haya yanajizatiti kuongeza dhamira ya kudumisha umoja wa Muungano wa Ulaya.

TANZANIA NA ZANZIBAR

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pia unaunganishwa na historia , utumwa , ukandamiza na unyonyaji wa mabeberu. Mbegu za ushirikiano zimepwanda kihistoria na Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume wanaunganishwa kwenye kitovu cha machungu ya ubeberu wa Kiarabu akiwamo Tip Tip mfanyabiashara mkubwa wa watumwa anaowatoa Tabora hadi Bagamoyo na kuwauza Zanzibar kama bidhaa nyingine.

Lakini hayo yalifanyika zamani kabla ya 1964, hivyo Karume na Nyerere wanateswa na machungu ya ukandamizaji, uliochagiza kuanzishwa chama cha ASP na TANU kutetea maslahi ya weusi ambao walidharauliwa, kunyanyaswa na kuipuuzwa.

Ikumbukwe Muungano ulilenga pia kuwa na nguvu ya kuendelea kuyalinda mapinduzi ya Zanzibar yaliyomng’oa Muarabu ya ambayo yalihitaji dola lenye msuli kijeshi na usalama wa taifa wenye nguvu ili kuyalinda dhidi ya chokochoko za wanaopinga Serikali ya Wazanzibari (Waafrika badala ya Waarabu).

KUBOMOA NI HISIA ZA SIASA

Wanachama wa EU wanafahamu umuhimu wa umoja tena wakiangalia Urusi ilivyoparaganyika. Ni wazi kuwa EU inadumu kwa sababu ya misimamo ya viongozi wanaotaka iendelee mmojawapo ni Kansela wa Ujerumani Angela Markel.

Kadhalika Rais Magufuli na Dk Ali Mohamed Shein,wakifuata nyayo za wastaafu Jakaya Kikwete, Benjamin Mkapa na Ali Hassani Mwinyi, kwa Tanzania Bara na Amani Abeid Karume, Dk. Salmin Amour, Idris Abdul Wakili, Ali Hassan Mwinyi na Abdu Jumbe Mwinyi, hawako tayari kuchezea Muungano. Wanayafahamu mazuri ya Muungano na utamu wa kuwa ndani ya ushirika wa dola lenye nguvu Bara na Visiwani.

Ni kazi ya wanasiasa kulinda na kupambana na fikra mchanganyiko zikiwamo za kisiasa, kiuchumi, kisaikolojia, kijiografia zinazoelekeza ama kuvunja Muungano kwa sababu wanafahamu kinasababisha watu kuukataa au kuukosoa.

KUVUNJA UMOJA NI LAANA?

Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuonyesha laana inayotokana na ubaguzi na kuvunja umoja , akitoa mfano wa sumu ya ubaguzi inayoambatana na kujitambulisha kwa ukabila na utaifa licha ya kuwa wote ni Watanzania.

Anaonya kuwa iwapo kuna hisia za kujiondoa kwenye Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zitaanza kusikika kelele za sisi Wazanzibari, Sisi Wazanzibara, Sisi Wapemba …. Na kauli nyingine za kujitenga. Yote haya hayajengi.

Ukingalia, Sudan ya Kusini ni taifa lililojiondoa kutoka Sudan ya Khartoum, lakini kinachotokea leo naweza kukifananisha na laana ya kujitenga, kuongezeka maafa kama vifo, vinavyotokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe, wakimbizi na umaskini miongoni mwa raia wa Sudan Kusini ndicho kinachojiri, bila kusahau vita visivyokwisha.

Ndiyo maana changamoto kama hizi zinawafanya marais wa Tanzania na Zanzibar kuamua kuulinda Muungano na sasa Rais Magufuli anasema atakayetaka kuuvunja anavunjika kwanza.

Wakati Rais anawaonya wenye kiu na ndoto za kuvuruga Muungano wasitamani kufanya hayo, ni wazi kuwa haiwezekani kuuacha ubaki kama msahafu. Watanzania wapewe jukwaa la kuujadili ili kuuboresha, kuukosoa, kuufanya wa wananchi zaidi badala ya viongozi waasisi au wanasiasa.

Zinahitajika juhudi za kuufuatilia mwenendo wa Muungano, kuibua changamoto, kushauri na kuleta mambo mapya yanayoleta tija kiuchumi, kisiasa na kiteknolojia.

MUHIMU

Kuimarisha Muungano ni jambo jema hivyo ni vyema kuwa na taasisi inayoshughulikia Muungano kikamilifu. Ianzishe utaratibu wa kutumia utaalamu na ubobezi kutoka kwa viongozi watangulizi kuanzia Marais wastaafu wa Bara na Zanzibar, mawaziri viongozi na wakuu, wanasheria wa serikali,wabunge, mgavana wa benki wasomi kushauri jinsi ya kuboresha taasisi hii.

Ofisi hii ya Makamu wa Rais itumie wataalamu na wana siasa kuratibu na kumaliza changamoto kubwa za Muungano, iitoe ufumbuzi na iwe ni jukwaa la kupokea maoni ushauri na miongozi ya kuboresha ushirikiano huu.

Muungano usiwe wa kisiasa zaidi ulinde maslahi ya pande zote, kiuchumi, uongeze furaha kwa Watanzania, waupende na kuuthamini kuwa ni mali yao na si kulazimishwa.

Columnist: