Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mtoko wa Mastaa kipindi hiki cha likizo

IMG 4558 Messi Na Wanae.jpeg Lionel Messi na wanae

Sat, 8 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hapa Bongo ni hekaheka za klabu kubwa nchini ikiwamo Yanga, Simba na Azam kuingia chimbo kusaka nyota wakali wataocheza msimu ujao na kuwapa mafanikio.

Hata kule kimataifa mwendo ni huohuo kila kukicha ni habari za klabu fulani kusaka saini ya mchezaji fulani, mfano ni kule katika Ligi Kuu England (EPL) na Ligi Kuu Hispania (La Liga) ambapo tayari klabu kubwa zimesainisha mastaa wapya.

Kipindi hiki huwa ni muda wa mastaa kuwa katika hali ya utulivu, huku wakisikilizia dili kutoka kwa mawakala ambao ndio wapika dili la wakubwa katika usajili.

Wakiwa wanasubiri mambo hayo, mastaa wa kulipwa ambao wako timamu kiafya huwa wako sehemu za burudani wakijiachia katika maeneo ya kujipa utulivu wa kimwili na kiakili ikiwamo yale ya fukwe kama vile za Zanzibar, Dubai na Miami.

Vilevile na wale ambao wako katika majeraha hujipa utulivu katika maeneo kama hayo na huku pia wakijiuguza na kuhakikisha kuwa wanapona na kuwa timamu kiafya. Mastaa wa kulipwa wanaolipwa pesa nyingi ambao pengine walimaliza ligi wakiwa majeruhi huwa wanatambua vyema ule msemo wa “afya mtaji”.

Wengi huwa wamejituliza kwenye mazingira mazuri ya raha na burudani wakiwa katika maeneo ambayo pia huwa na gym za kueleweka, hivyo wale walio majeruhi huweza kupasha pasha kwa kuzingatia programu za mazoezi mepesi kwa mchezaji mwenye majeraha yanayoelekea kupona.

Ukitembelea katika kuta za mitandao ya kijamii za mastaa wa EPL, La Liga na Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga) utakuta wametupia picha wakiwa mapumziko, lakini haimaanishi kuwa wanakula raha pekee, bali pia hufanya mazoezi binafsi.

Hata yule staa majeruhi kipindi hiki anahakikisha kuwa katika mapumziko hayo anakula burudani za kawaida ambazo haziingilii uponaji wake ikiwamo kutojihusisha na unywaji pombe na ulaji holela.

Ni kweli pia kipindi hiki huwa karibu na familia, lakini wanahakikisha kuwa wanatenga muda wa kufanya mazoezi binafsi ili kulinda utimamu wa afya. Vilevile hawajiachii moja kwa moja kula burudani, bali huwa na mpango kazi maalumu wa mazoezi ili kurudisha akili na mwili katika mpira.

Uchaguzi wa mastaa kwenda maeneo mazuri ya burudani huwa ni uamuzi sahihi kwani wanahitaji mazingira rafiki zaidi kuwapa utulivu wa akili na mwili. Kupata hali hiyo katika mazingira mazuri ni faida kubwa hasa kwa mchezaji ambaye alimaliza ligi akiwa majeruhi au yule ambaye anauguza jeraha la muda mrefu.

VITU 10 MAZINGIRA RAFIKI

Moja ya vitu ambavyo ni rafiki kwa mwili wa binadamu ni mazingira ya safi yenye jua kwani mwanga unauwezesha mwili kuwa na ngozi na mifupa imara na hii ni kutokana na mwili kujitengenezea vitamin D.

Miili hutengeneza vitamini D kwa kukaa katika jua dakika 15 kwa siku. Vitamini D inauwezesha mwili kulinda madini ya kalisiamu na kuzuia mifupa kuwa dhaifu.

Jua kwa sasa lipo la kutosha nchini, katika maeneo ya Ulaya na nchi za Uarabuni ikiwamo kule Falme za Kiarabu kama vile Dubai sambamba fukwe za Amerika kama vile Miami.

Pili ni unywaji majisafi na salama katika mazingira ya joto hukupa kiu ya kunywa maji mengi ukilinganisha na aliyepo katika mazingira ya baridi.

Ikumbukwe kuwa ili jeraha kupona haraka au kuboresha utimamu wa mwili wa mchezaji inahitajika kunywa maji ya kutosha angalau lita tatu kwa siku kwa wanamichezo.

jambo la tatu ni kupumzika na kulala katika mazingira ya kuvutia hasa ya sehemu za fukwe ambayo husaidia kupeperusha matatizo ya akili ikiwamo msongo wa mawazo na shinikizo la akili.

Uboreshaji wa afya ya akili husaidia utulivu wa mwili na hatimaye kupona haraka jeraha au kulinda na kuboresha utimamu kwa yule mchezaji asiye majeruhi.

Ikumbukwe matatizo ya akili yanachangia kinga ya mwili kushuka na kuwa dhaifu, hivyo ni hasara kwa jeraha kupona na kudhoofisha utimamu wa mwili kwa mchezaji asiye na majeraha.

Nne kupata hewa safi. Katika maeneo mengi ya kitalii ya kuvutia huwa ni ya wazi yakiwa na hewa safi ya kutosha, jambo ambalo ni faida kwa mwili kwani hupata oksijeni nyingi na hatimaye kuchangia jeraha kupona vizuri.

Tano ni uwepo wa mazoezi rafiki na mazoezi mepesi ambayo ni aina ya mazoezi yanayouwezesha mwili kuvuna utimamu pasipo kujijeruhi. Kumbuka sio kila zoezi ni rafiki wakati wa uuguzi wa jeraha.

Na kwa wale wasio na majeruhi huhakikisha kuwa wanafanya mazoezi binafsi yasiyouchosha mwili wala kuupa uchovu au majeraha.

Sita ni usingaji na mazoezi tiba. Ni kawaida kwa mchezaji majeruhi na asiye na majeraha kipindi hiki kuongeza saa za kufanya usingaji kwa lengo la kuipa misuli ya mwili utulivu na akili.

Vilevile huweza kufanya mazoezi tiba kwa wale ambao wana majeraha ya viungo kwa lengo la kuponesha kiungo na kurudisha utendaji kama awali. Wakati kwa yule asiye na jeraha anaweza kuwa anafanya mazoezi kuboresha utimamu wa mwili na kuondoa uchovu wa mwili au mkazo wa misuli ya mwili.

Saba ni mlo bora uliosheni vyakula vya makundi yote ikiwamo kula zaidi mazao ya baharini kama vile minofu ya samaki ili kupata protini rafiki ambayo ndio malighafi ya misuli kufanya kazi.

Nane, mastaa hukwepa kutumia vilevi na uvutaji tumbaku. Muda mwingi mastaa kama Cristiao Ronaldo na Lionel Messi hupendelea kutumia “snacks” kama juisi za matunda asili, sambusa na kababu za minofu ya samaki.

Njia hii ni danganyishi kwa mwili ili kumfanya asitamani vitu hatari kama vile tumbaku na pombe. Ikumbukwe kuwa vitu kama hivi hudhoofisha mwili na kuchelewesha jeraha kupona kwa wakati.

Vilevile wakati wa ulaji wa vyakula katikati ya mlo mkuu yaani snacks husaidia mwili kuja kumeng’enya mlo mkuu kwa ufanisi na pia kulifanya tumbo lisiwe tupu.

Tisa ni kusikiliza burudani ya muziki. Hiki ni moja ya kiburudisho kinachompa binadamu utulivu wa kiakili na kimwili. Maeneo wanayokula raha huwa na utulivu huku wakipata burudani ya muziki laini. Muziki ni tiba ya matatizo ya akili ikiwamo shinikizo la akili na msongo wa mawazo.

Jambo la kumi na la mwisho mastaa kipindi hiki huhakikisha wanakuwa na uhusiano mzuri na klabu walizonazo pamoja na wakala kwani wanafahamu fika kuwa uhusiano bora ndio msingi wa mafanikio.

CHUKUA HII

Kumbuka vitu hivi sio tu kwamba vipo Ulaya, Amerika au Uarabuni, bali hata Bongo vipo vya kumwaga tena vya kiasili kwa bei chee. Hivyo ni muhimu mastaa wa Kibongo nao wakafanya haya katika mazingira yetu.

Columnist: Mwanaspoti