Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mtihani, waamuzi Bongo pasua kichwa

Waamuzi Waula Mtihani, waamuzi Bongo pasua kichwa

Thu, 5 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Waamuzi ni kati ya wadau muhimu katika mchezo wa soka na ndio maana haikuwa ajabu katika Sheria 17 za mchezo huo nao wamejumuishwa sambamba na wasaidizi wao.

Ndio. Mwamuzi kati ndiye mkuu wa mchezo wa soka akiwa ni sheria namba 5 na ana jukumu na mamlaka ya mwisho ya kusimamia sheria za mchezo huo na uamuzi anaoutoa uwanjani huwa ni wa mwisho.

Moja ya kazi za mwamuzi wa kati ni kudhibiti mchezo kwa ujumla akishirikiana na wasaidizi wawili na kama itabidi, msaidizi wa nne anayekaa mezani naye anabeba jukumu hilo na baadhi ya majukumu ya mwamuzi ni kuhakikisha kuwa mpira na vifaa vya wachezaji vinakidhi mahitaji ya mchezo husika.

Pia huangalia muda na kusimamisha mchezo pindi sheria za mchezo zinapovunjwa wakati waamuzi wasaidizi wamepangwa kama sheria namba 6 ya soka, ambapo huwa wawili wakimsaidia mwamuzi wa kati.

Kazi ya waamuzi hao wasaidizi ambao zamani walizoeleka kuwa kama washika vibendera ni kuamua endapo mchezaji amezidi upande wa timu pinzani, mipira ya kurusha na kumsaidia mwamuzi wa kati kufanya uamuzi sahihi kulingana na mchezo.

Wanatakiwa kushika vibendera muda wote kwa ajili ya kutoa ishara ya uamuzi wao na wanatakiwa muda wote kuangalia mistari ya pembeni ya uwanja na langoni na kuinua vibendera iwapo mpira utavuka mistari hiyo ili kuashiria kama mpira unatakiwa kurushwa au kupigwa kutokea langoni.

Kwa hapa Tanzania waamuzi wamekuwa muhimu katika mechi mbalimbali kuanzia zile za Ligi Kuu Bara hadi za madaraja ya chini na michuano mingine, lakini wakati mwingine wamekuwa wakijikuta kwenye lawama kutokana na uamuzi wao wakati mwingine kuwa na utata.

Hata hivyo, uliwahi kujiuliza hao waamuzi wa soka nchini wanapatikana vipi? Ni mali ya nani au wanawajibika kwa nani kati ya Shirikisho la Soka (TFF), Kamati ya Waamuzi au Chama cha Waamuzi (Frat)? Wanalipwaje na malipo yao mgawanyo wake ukoje na nje ya fani hizo wanafanya nini?

Mwanaspoti linakuletea ripoti maalumu inayojibu maswali hayo na kuweka bayana namna waamuzi hao wanavyokabiliana na changamoto mbalimbali ambazo wakati mwingine huwapa wakati mgumu kutekeleza majukumu yao viwanjani. Endelea nayo...!

WANAVYOPATIKANA NA MADARAJA YAO

Waamuzi wanapatikana kutokana na kujiunga na mafunzo ya awali (preliminary) ya uamuzi wa soka kisha hupanda madaraja kwa jinsi wanavyoshiriki kozi zinazotolewa na mamlaka inayosimamia soka na Chama cha Waamuzi (Frat) kuanzia ngazi za wilaya, mkoa hadi taifa.

Mgawanyo huo wa madaraja hadi wale wanaopata beji za Fifa huwa na ngazi tofauti za uchezeshaji na kusaidia kazi iwe rahisi kwa wasimamizi wa soka nchini.

Mmoja ya wakufunzi wa waamuzi nchini (jina tunalo) anasema kwa waamuzi wanaotoka darasani 3P, yaani daraja ambao wengi ni kwa ajili ya Ligi Daraja la Tatu Ngazi za mikoa, Daraja la Pili kwa ajili ya First League na Daraja la Kwanza. Hivyo waamuzi wote wa Ligi Kuu ni wale wa Daraja la Kwanza.

“Sasa hawa Daraja la Kwanza kuna wale wanaochezesha Championship na wale wa Ligi Kuu ambao wanachanganywa na wale wa Fifa (Shirikisho la Soka la Kimataifa) kwa ajili ya Ligi Kuu, hivyo kutokana na wingi wao utakuta wengine wapo hadi First League lakini wana sifa sawa na yule wa Ligi Kuu,” anasema mkufunzi huyo mwandamizi ambaye anafafanua pia juu ya maswali ya wadau wengi kutaka kujua kuna tofauti ya mafunzo baina ya waamuzi wa kati na wale wa pembeni (linesmen au line one na line two).

“Hakuna tofauti yoyote, kwani wote wanasoma masomo sawa lakini mwamuzi mwenyewe anajiangalia wapi anapamudu zaidi kama ilivyo kwa mwandishi wa habari mwingine anaandika habari za michezo mwingine habari za kijamii, uchumi na afya,” anasema na kuongeza:

“Kozi ni moja, lakini unapomaliza mtu mwenyewe anaamua kujikita sehemu moja yaani katika ‘practical’ ndio utaona utofauti wa mtu hivyo hadi mtu anakuwa promoted (kupandishwa) na wakufunzi kufikia levo ya Fifa, lakini huwezi kufika Fifa bila kupita ‘elite’ yaani ni ‘crime’ ya Daraja la Kwanza.”

MALI YA NANI?

Mmoja wa waamuzi anasema Chama cha Waamuzi (Frat) ndio wanaostahili kuwamiliki waamuzi, lakini kwa sasa ni kama wamepokwa nguvu kwani TFF kupitia

Kamati ya Waamuzi ndio imekuwa na nguvu zaidi, tofauti na zamani chama hicho kilikuwa kinawapangia mechi na kuhusika nao zaidi.

“Frat ndio wanaowapangia waamuzi ratiba za michezo au kutoa pendekezo flani dhidi yao kutokana na uwezo wa kila mmoja. Hata hivyo, Frat kwa sasa chama hicho ni kama kivuli tu maana hawana nguvu yoyote kwenye uamuzi, hivyo waamuzi kwa tafsiri ya haraka ni mali ya TFF,” anasema mmoja wa waamuzi na kufafanua.

“Mfano mwamuzi Michael Jojo (sio jina halisi) amepangwa kuchezesha mchezo kati ya Ihefu na Azam yale majina yakifika TFF wanayachakata upya na TFF ina uwezo wa kubadilisha jina la mwamuzi na kupewa mwingine.”

“Leo Frat wanaweza kuona, Jojo anastahili kupewa beji ya Fifa na jina lake likapelekwa, lakini TFF ikigoma na hakuna kitachofanyika na TFF wanaweza wakapendekeza majina mengine bila Frat kuhusishwa na likapita, hapo ndio ujue hiyo Frat ni kama kikundi tu pale TFF ambacho hakina kazi yoyote sababu Fifa wanaisikiliza zaidi TFF,” anazidi kufafanua

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Frat, Omary Abdulkadir anasema waamuzi ni mali ya Chama na wamesajiliwa chini ya mwamvuli wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Anafafanua kwamba Frat ni chama ambacho kimesajiliwa hakihusiani na Bodi ya Ligi wala TFF wanajitegemea wenyewe na kujiendesha kwa kutegemea wanachama.

“Wanachama wanalipia ada kila mwaka pesa inayopatikana huko ndio inayosaidia kuendesha chama na awali tulikuwa tunasaidiwa na TFF kupitia mapato ya kila mchezo wa ligi kuu kutuingizia elfu kumi kwenye akaunti ya chama na ikichezwa mechi ya ligi daraja la kwanza Championship elfu tano ingawa sasa mchakato huo umesitishwa na hatufahamu shida imetoka wapi?” anasema.

Hata hivyo, mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Nassoro Hamduni anasema jukumu lao kubwa ni kupendekeza majina tu ya waamuzi watakaochezesha mchezo husika na kisha wanaiachia TFF na Bodi ya Ligi (TPLB).

“Sisi baada ya kufanya mapendekezo tunapeleka majina yao kwenye kamati za TFF, TPLB na wao ndio wanaowapigia simu kuwajulisha na kuhusu mengine yanayoendelea kuhusu wao wanajua wenyewe.”

OFISI ZAO NI ZIPI?

Chama cha Waamuzi Taifa (Frat), kimesema pamoja na kuwa na ofisi yao waliyopewa na Shirikisho la Soka nchini, (TFF), lakini wapo katika hatua za mwisho kuhakikisha wanarejesha ofisi yao iliyouzwa.

Mwenyekiti wa Chama hicho, Omary Abdulkadri anasema kabla ya kuingia madarakani, Frat ilikuwa na ofisi yake yenye hadhi lakini mmoja wa viongozi wa juu aliyekuwapo aliuza katika moja ya kampuni (jina tunalo).

Alisema kwa sasa anapambana kadri ya uwezo wake kuhakikisha anarejesha mali hiyo na yupo tayari kuuza kila kitu chake ili kufanikisha suala hilo.

“Tunaishukuru sana TFF kwa kutupa ofisi nzuri ambayo inatusaidia kutimiza wajibu wetu, lakini tunatafuta njia ya kumkamata aliyeuza ofisi ya chama na kuirejesha.

“Kama niko hai nitapambana ofisi hiyo inarejea, nitauza hata kila kitu changu kwa maslahi ya Chama, tunajua ofisi hiyo ilipokuwa sambamba na Baraza la michezo Taifa (BMT)‚“ anasema Abdulkadri.

Anaongeza kuwa kabla ya kuwa na mpango wa kujenga ofisi nyingine mpya za chama, anahitaji kuona anakamilisha kwanza kurejesha ofisi hiyo ya zamani na mhusika kuchukuliwa hatua.

“Mawazo ya kujenga ofisi mpya tunayo kwa sababu tulishapewa eneo hapa Dar es Salaam na mipango ni kutafuta wadau kwa sababu sisi kama chama hatuna pesa,” anasema Kigogo huyo.

FA ZINAKABA NA KUACHIA

Katika kutimiza majukumu yao kwenye mechi za Ligi Kuu, Championship, First League, Ligi Kuu ya Wanawake na Kombe la Shirikisho kundi hilo hujitegemea katika usafiri na malazi hivyo kujikuta kwenye mazingira magumu ugenini, licha ya baadhi yao kulipwa posho kabla ya safari na wengine kuisubiri baada ya kazi.

Baadhi ya waamuzi wanasema, wanapofika kituo cha mechi, wanapaswa kuripoti kwenye FA ya mkoa husika kwa kuwapa taarifa ya uwepo wao pale, lakini je? ni upi mchango wa vyama vya soka vya mikoa husika kwa waamuzi hao?

“Kwa kawaida FA za mikoa ndiyo huwa ‘wenyeji’ wa waamuzi pale wanapotua kwenye mkoa wao kwa kuwaandalia mazingira rafiki kabla na baada ya mchezo ikiwemo usalama wao na malazi kwani vyama hivyo ndiyo huwa mwenyeji wa mchezo husika lakini si kuwalipia,” anasema mmoja wa viongozi wa FA.

WASIKIE HAWA

Ingawa kwa Dar es Salaam, (DRFA), Daudi Kanuti ‘Injinia’ ambaye ni mjumbe wa kamati ya mashindano anasema mwamuzi anapokuwa kwenye kituo cha mechi wao hawawajibiki nao kwa kuwa wanajitegemea.

“Umekujaje, umefikia wapi, usalama wake na vitu vingine sisi havituhusu, kazi yetu ni kuhakikisha wale wa Dar es Salaam wanapata mafuzo na kazi nyinginezo.

Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Dodoma (Dorefa), Mweri Hamsini anasema FA wamekuwa wakiwatafutia mechi nyingi za kuchezesha za madaraja ya chini ili kuwapa ufiti.

Anasema pia wamekuwa wakihakikisha viwango vya waamuzi wa Mkoa wa Dodoma vinaendelea kuboreka kwa kukutana mara kwa mara na kuzungumza na wakufunzi wa waamuzi.

Anaongeza kwa wale wanaochezesha madaraja ya juu Championship na Ligi Kuu wamekuwa wakikutana nao mara kwa mara na kujadiliana nao changamoto wanazokutana nazo.

“Kile kinachopatikana kama chama huwa tunawapa ili kuwasapoti na ndio maana mashindano yetu yanaenda vizuri. Ndani ya chama chetu hatuna madeni ndio maana hujawahi kusikia kashfa yoyote wamekuja kulalamika

“Kubwa zaidi ni kuendelea kuwapa sapoti na ndio maana wapo Jamhuri kila siku wanafanya mazoezi,” anasema Hamsini ambaye anakaimu nafasi hiyo mara baada ya Hamis Kissoy kusimamishwa.

Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mbeya, (Mrefa) Jumbe Sadick anasema baada ya kuwasili waamuzi huwa wanaripoti kwa mwenyeji wao, katibu mkuu wa chama, ambaye ni msimamizi wa kituo.

Anasema baada ya kupokelewa na msimamizi wa kituo wanaweza kumjurisha pia mwamuzi wa akiba ‘fourth official’ ambaye watakuwa wote kwenye mchezo ili kuweza kupanga maandalizi ya mchezo.

“Sisi Chama cha Soka huwa hatuhusiki zaidi, kwa sababu wanakuwa na msimamizi wa kituo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Mrefa, lakini pia wanakuwa na mwenzao mwamuzi wa akiba ambaye anakuwa ni wa hapahapa.

“Mrefa tunaweza kusaidia pale inapohitaji jambo lolote kutoka kwetu japokuwa kuna pia kamati ya waamuzi Mkoa, ambapo na wao wana umoja wao wana-vyowasiliana,” anasema Sadick ambaye ni mwamuzi mstaafu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi mkoani humo, Ahadi Nyondo anasema wao huwa hawahusiki moja kwa moja kwa waamuzi wanaofika kuchezesha mechi, isipokuwa mwenyeji zaidi huwa ni mwamuzi wa akiba.

“Sisi tunachoweza kusaidia ni pale ikitokea dharula mfano mwamuzi kapata tatizo tutamsaidia ila wanakuwa wanaratibiwa na kamati ya waamuzi Taifa,” anasema Nyondo.

WASIMAMIZI WA VITUO

Kwa upande wake msimamizi wa kituo na katibu mkuu wa chama cha soka mkoani humo, Lucas Kubaja anasema jukumu lake ni kuhakikisha usalama kwa waamuzi wanapofika eneo la kazi.

Anasema tangu kuanza majukumu hajapokea tatizo kubwa lolote hadi kufikia hatua ya kuahirisha au kusimamisha mchezo, isipokuwa changamoto ni za kawaida kama mwamuzi kuchelewa kutokana na usafiri. “Mimi ndio nakuwa mwenyeji wa waamuzi nikiwakilisha Bodi ya Ligi, kazi yangu ni kuhakikisha mchezo unaanza na kumalizika salama, ikiwamo hao waamuzi wanafanya majukumu yao vizuri.

“Kama kutakuwa na tatizo kubwa ambalo siwezi kulimaliza nawasilisha ripoti ngazi za juu wao wanaamua kwa sababu miongoni mwa sheria za mpira refa ni namba mbili,” anasema Kubaja.

MENGI ZAIDI

Katibu Msaidizi wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), Khalid Bitebo anasema mchango wao kwa waamuzi ni kuwapa usaidizi wa mahali salama pa kufikia, kuwapa muongozo na mazingira yote yaliyouzunguka mchezo husika.

Anasema mara nyingi waamuzi wanapotaka kuja mkoani kwao kuchezesha mchezo huwasiliana na chama hicho kwa ajili ya mapokezi, kuandaliwa eneo la kufikia na usaidizi mwingine utakaowapa usalama kabla na baada ya mchezo.

Anaongeza kwa kueleza kuwa wakati mwingine waamuzi hawawasiliani na vyama hivyo (FA), bali humalizana kwa juu na baadhi ya timu ambazo huwapokea na kuwaandalia mazingira ya sehemu za kufikia kwa ajili ya malazi hivyo ikitokea hali kama hiyo huwa hawaingilii uamuzi huo.

“Sisi ndiyo huwa mwenyeji wa mchezo na msimamizi wa kituo kwahiyo huwa tunawapokea wanapowasiliana nasi ama kuhitaji msaada wetu wowote ikiwamo eneo la kufikia, usalama wao na usaidizi mwingine, japo siyo lazima wengine hufikia wanapopajua ama huwasiliana na timu mwenyeji.

“Kwenye Kombe la Shirikisho (ASFC) waamuzi huwekewa fedha kabla ya kuanza safari hivyo mambo mengi wanamaliza wenyewe hakuna usumbufu mkubwa, hali ni tofauti kwenye ligi waamuzi hujitegemea kila kitu na hufidiwa baadaye kwahiyo huwasiliana na chama cha soka cha eneo husika na kuomba usaidizi,” anasema.

Mwamuzi wa zamani wa Ligi Kuu, Joseph Masija anaamini vyama vya soka vya mikoa havina mchango kwa waamuzi kwani mara nyingi hukutana tu kwenye kikao cha mchezo husika (PM) na wakati mwingine hawafahamu kabisa mazingira wanayokuwemo waamuzi hao. “Unajitegemea nauli ya kwenda na kurudi, malazi na chakula ambayo unapaswa kurudishiwa baada ya mchezo, pia posho ya kujikimu na hela ya mchezo kwahiyo ukiwa navyo unajisimamia mwenyewe,” anasema

Kwa upande wake mmoja wa makimishna wa mechi za Championship na Ligi ya wanawake (jina tunalo) anasema vyama vingi vya mikoa hutoa msaada kwa waamuzi kwa kuwa wanafahamu changamoto nyingi zilizopo kwenye kada ya marefarii nchini.

“FA nyingi wanasaidia sana kwa sababu wanalijua hili. Wanatupokea na kusaidia huduma ndogondogo, ‘sometimes’ hata nauli ya kugeuza huwa wanasaidia. Yote haya mfano najichukulia mimi mwenyewe sijui lakini kama wote huwa hivi, ila nina imani huwa hivi kwa wote, na wakati mwingine kwa kushirikiana na timu mwenyeji,” anasema kamishna huyo.

Columnist: Mwanaspoti