Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mtihani ulivyo mgumu kuachana na dawa za kulevya

Bernard Morisson.jpeg Watumiaji wa Dawa za Kulevya

Mon, 4 Jul 2022 Chanzo: Mwananchi

Tanzania ikishuhudia wimbi la vijana kuingia bila kujua katika vihatarishi vya matumizi ya dawa za kulevya maarufu kama unga, waraibu wa mihadarati wanaohitaji usaidizi wa kuacha kutumia vilevi hivyo wanaongezeka.

Hali hiyo inadhihirika huku Serikali ikiendelea kuongeza nguvu kwenye mapambano dhidi ya dawa hizo nchini, huku ikiongeza idadi ya nyumba za upataji unafuu (sober houses) kwa waraibu wa dawa hizo kutoka 33 mwaka 2020 hadi nyumba 44 mwaka 2021.

Vilevile, mwamko wa kutaka kuachana na uraibu huo umeonekana kwa waathirika, kulingana na takwimu za Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).

Kwa mujibu wa takwimu hizo, mwaka 2017 kulikuwepo na waraibu 1,106 waliopata huduma ya dawa ya methadone (za kutibu utegemezi wa dawa nyingine za kulevya) na idadi imekuwa ikiongezeka hadi waraibu 9,188 kwa mwaka 2021.

Hata hospitali mbalimbali zimekuwa zikitoa bure tiba ya uraibu wa dawa za kulevya katika vitengo vya afya ya akili ambapo jumla ya waraibu 169,269 walipatiwa huduma mwaka 2020 na idadi hiyo imeongezeka hadi 891,117 mwaka 2021.

Wengi wakamatwa

Wakati ongezeko la wanaohitaji tiba linaweza kuashiria ari ya wengi kutaka kuachana na dawa hizo, kwa upande mwingine linaashiria kuadimika kwa dawa zenyewe, hivyo watumiaji wengi kulazimika kutafuta mbadala wake.

Kuadimika kwa dawa hizo, kwa mujibu wa DCEA, ni matokeo ya hatua zinazochukuliwa na mamkala hiyo kuwanasa wanaoingiza dawa hizo.

Takwimu za DCEA zinabainisha kwa mwaka 2020 watuhumiwa kupatikana na dawa aina ya heroine walikuwa 428 na cocaine 80 ikilinganishwa na watuhumiwa 588 wa heroine na 100 wa cocaine kwa mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 38 kwa heroine na asilimia 20 kwa cocaine.

Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, mamlaka hiyo ilifanikiwa kukamata kilo 5,051 za heroine na kilo 1,655 za cocaine.

Katika kipindi hicho ekari 11 za bangi na ekari 11 za mirungi ziliteketezwa, huku vifurushi 170 vya mirungi vikikamatwa wilayani Same Kilimanjaro kati ya Aprili na Oktoba 2021.

Ugumu kuacha

Baadhi ya watumiaji dawa za kulevya wanasema hulazimika kutumia dawa mbadala pale wanapokosa zile halali na pia kutokana na changamoto wanazozipitia wale walioamua kuacha kwa hiari.

Vijana hao waliopo eneo la Ubungo Darajani wanasema dawa za kulevya hawapati kama zamani na kuna nyakati wanaweza wasipate hata siku tatu, hivyo hununua dawa tiba kujitibu arosto (uraibu).

Hata hivyo, wanasema ingawa dawa mbadala zinawasaidia, bado mwili huzikataa mpaka pale watakapopata heroine.

“Kuna mwenzetu mmoja hapa kijiweni alitumia valium na baada ya muda, msela mwingine akaja na ‘kitu’, tukafurahi wana, tukasema acha tupone. Mwenzetu alipojidunga akasinzia tukajua mwana kawaida, ile kushtuka muda unaenda hachezi wala kutingishika, kumbe amekufa,” alisema kijana aliyejitambulisha kwa jina la Frank.

Licha ya kudhibitiwa kwa kiasi fulani, bado Frank anasema wamekuwa wakipata heroine, ingawa bei inazidi kuwa kubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo walinunua hata kwa Sh3,000 na Sh5,000.

Methadone na changamoto zake

Licha ya usaidizi uliopo, bado kuna changamoto, kwani wengi wanaohitaji kuacha dawa za kulevya hushindwa kuhimili hali ya ‘arosto’ kutokana na changamoto ya upatikanaji wa huduma.

“Natumia fedha nyingi kwa siku kwenda kunywa dawa Muhimbili, kutoka nyumbani mpaka Kibamba stendi natumia Sh2,000, nikitoka hapo nipande daladala mpaka Mbezi 500, pale nitapata mwendokasi mpaka Kimara 400 na Kimara mpaka Muhimbili 650, nikifika ninywe (dawa) nirudi, natakiwa kuwa na zaidi ya Sh7,000 kila siku,” alidai Asma Ally (25), mkazi wa Kibamba jijini Dar es Salaam.

Fadhili Ibrahim (34) ni mmoja wa vijana waliopitia changamoto hiyo, baada ya kuamua kuacha dawa za kulevya na kugeukia methadone.

“Kuna wakati nilijikuta nipo gerezani na huko nilipata changamoto kubwa kwa kukosa dawa ya methadone, arosto ilinitesa sana,” alisema Fadhili ambaye aliingia katika uraibu wa dawa za kulevya baada ya wazazi wake kutengana.

Alisema kusikia maumivu ya viungo, kukosa raha na amani, kusikia joto kali ni miongoni mwa vitu anavyosema alipambana navyo kwa kipindi chote alichoishi katika Gereza la Ruanda mkoani Mbeya.

Lakini mnufaika wa methadone ambaye alimsaidia Fadhili, Janeth Mwamtobe alisema ilikuwa changamoto kubwa kwa mahabusu na wafungwa kupata haki na huduma ya usaidizi wakiwa polisi, mahakamani na magerezani.

“Kwa sasa tunapata ushirikiano mkubwa, mfano mkuu wa Gereza la Ruanda anatusaidia, wafungwa wanatoka gerezani wanakuja kupata methadone wakiwa wameongozana na askari,” alisema.

Janeth ambaye aliathirika na dawa za kulevya miaka 20 iliyopita, ametumia miaka mitano tiba ya methadone, miwili Hospitali ya Mwananyamala na mitatu Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya.

Mkuu wa Gereza la Ruanda, Ahmad Lalikila Seleman alisema hapo awali waliwatafsiri watumiaji wa dawa za kulevya kama watu wasiofaa, lakini Februari mwaka huu utaratibu umebadilika katika gereza hilo.

Lalikila alisema hiyo iliyokana na wao kupewa elimu na taasisi za ndani na nje ya nchi.

“Wadau hawa kupitia mamlaka ya DCEA walitupatia mafunzo maalumu, kwa sasa tunawaangalia wafungwa wetu na kama tukipata mraibu tunamwangalia yupoje na msaada gani anahitaji ili kurudi katika hali yake ya zamani,” alisema.

Lalikila alisema kwa sasa wafungwa wote wanawaangalia na kuhakikisha wanapata tiba ya methadone kwenye vituo vyao husika, ingawa wanapendekeza waweze kuendelea kusaidiwa wakiwa gerezani.

Hata hivyo, Mrakibu msaidizi Gereza hilo, Bruno Ntangwa alishauri vifunguliwe vituo ambavyo vinaweza kusaidia magereza huduma ikawa karibu kwa wafungwa waathirika na dawa za kulevya.

Mkuu wa upelelezi makosa ya jinai mkoa wa Mbeya, Andrew Kantime alisema mkoa huo kwa sasa unatoa msaada kwa waathirika wanapokuwa mahabusu, lakini lazima nchi iendelee kupunguza upatikanaji wa dawa hizo kwa kutoa elimu.

Sally Chalamila, mkurugenzi mkuu wa HJFMRI, taasisi inayojishughulisha na huduma za afya, alisema wanashirikiana na vyombo vya dola katika kuhakikisha mahabusu na wafungwa waraibu wanapata fursa ya kupata huduma za kiafya wakiwa mikononi mwa vyombo hivyo.

Mamlaka na udhibiti

Kwa upande wake, Kamishna DCEA, Dk Peter Mfisi alisema wamekuwa wakidhibiti uzalishaji, usambazaji na uingizwaji wa dawa hizo kwa njia zote, hasa maji katika mikoa ya Tanga, Lindi, Dar es Salaam mpaka Mtwara.

Alisema wameweka nguvu kubwa kulinda kwenye vituo vya mabasi, viwanja vya ndege na sehemu nyingine ambazo zina muunganiko na nchi nyingine.

Zaidi ya hiyo, alisema wamekuwa wakitoa elimu kwa jamii madhara ya matumizi ya dawa za kulevya, uuzaji na usafirishaji.

“Wanaoathirika wanaamini walitumia dawa chafu, hawajui hata ukitumia safi unaathirika. Wengine wanapewa ahadi za kupata Dola 3,000 wakisafirisha, hawajui kuna kufa endapo zikipasukia tumboni au kufungwa kifungo cha maisha ukikamatwa.”

Kuhusu kupungua kwa mzunguko wa dawa hizo nchini, Dk Mfisi alisema biashara na matumizi ya dawa za kulevya ni kitu cha usiri, hivyo ni nadra kubaini iwapo mzunguko umepungua.

“Tunachoangalia ni kupungua kwa viashiria, ukiona bei inakuwa kubwa, ujue usambazaji ni mdogo. Bei ya Tanzania kwa sasa ni mara tatu zaidi ya nchi nyingine na watumiaji wengine wanatumia dawa tiba zenye asili za kulevya au mseto wa dawa nyingi kukidhi uraibu,” alisema.

Dk Mfisi alisema tayari watumiaji wengi wameanza kufika kwenye vituo vya matibabu wakisema dawa haipatikani kirahisi na ikipatikana ni bei ghali na hiyo inaashiria dawa kupungua kwenye soko.

“Mwaka jana tumekamata heroin na bangi kuliko mwaka wowote, kiwango kikubwa kuliko miaka 10 iliyopita. Hii inaonyesha nyingi zinazoingia zinakamatwa,” alisema.

Columnist: Mwananchi