Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Msiba wa JPM uwe somo kwa viongozi

634a8551792194d64329f2ace1762fcc Msiba wa JPM uwe somo kwa viongozi

Thu, 25 Mar 2021 Chanzo: ippmedia.com

Sote tumeshuhudia jinsi ambavyo umati umekuwa ukijitokeza kwenye shughuli za kuaga mwili huo, kuanzia jijini Dar es Salaam kwa siku mbili Jumamosi na Jumapili. Jumatatu (Dodoma) na jana Zanzibar, kabla ya leo jijini Mwanza na kesho (Chato) na kufuatiwa na Ijumaa ambayo itakuwa siku ya kumpumzisha rasmi Hayati Dk. Magufuli kwenye nyumba yake ya milele kijijini kwake Chato.

Kila Mtanzania amejionea kwa macho yake ama kusikia jinsi umati hususan wa wananchi wanyonge walivyofurika mitaani kwenye barabara ambazo mwili huo ulikuwa ukipitishwa, huku walilia na kutoa kauli za kuonyesha kwamba wamempoteza kiongozi waliyempenda, kumwamini na kumtumainia kuwatatulia matatizo na kero zao.

Waombolezaji wamemuita Hayati Magufuli kwa majina mengi yakiwamo ‘chuma’, jeshi, ‘jembe’, ‘tingatinga’, ‘jasiri’, ‘mtetezi wa wanyonge’, ‘mkombozi’ na mengine mengi. Makundi ya wafanyabiashara wadogo (wamachinga) na bodaboda yalijitosa barabarani kuusindikiza mwili katika maeneo kadhaa. Hiki ni kielelezo halisi cha ni jinsi gani aliwatumikia na kuwajali watu wanyonge.

Kwa Dar es Salaam siku ya pili ya kuaga mwili wake (Jumapili), watu kadhaa walipoteza maisha kwenye Uwanja wa Uhuru kwa kile kinachoelezwa ni msongamano mkubwa, ambao ulisababisha hata utaratibu wa kuaga mwili kusitishwa kabla idadi kubwa ya waombolezaji kuaga mwili.

Tukio lingine lililoshangaza wengi ni watu wengi waliopita kwenye jeneza lake kuaga mwili, walizimia na wengine kupoteza hata fahamu na kuwalazimisha askari kuwapa msaada.

Mbali na vilio na majina mbalimbali ambayo waombolezaji wamemwita Hayati Magufuli, pia kwa siku zote za kuaga tumeshuhudia makundi ya wanawake na vijana wakirusha kanga, mashati, tisheti na maua barabarani ambapo mwili ulikuwa unapita.

Kadhalika, katika maeneo kadhaa mitaani na kwingineko wananchi wanaendeleza mjadala kuhusu hali ya nchi hususan masuala ya maendeleo aliyokuwa akiyatekeleza kama yataendelea au ndio mwisho wake.

Wanahoji kama mpango wa elimu bure kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha nne utaendelea, mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, uboreshaji huduma za maji, afya, reli ya kisasa, miundombinu na mradi wa umeme wa Nyerere.

Mengine kudhibiti ujambazi, vita ya rushwa, uwajibikaji serikalini, matumizi mazuri ya fedha za umma, kwa kutaja baadhi.

Wakuu na wawakilishi wa nchi kadhaa za Afrika waliohudhuria mazishi ya kitaifa jijini Dodoma juzi, wengi walielezea kifo cha Magufuli kuwa ni pigo kwa taifa, huku wakimwelezea kuwa amelifanyia Taifa mambo makubwa kiuchumi, ingawa wameelezea imani kwa Rais Samia Suluhu kuwa atayaendeleza.

Tunaamini viongozi wetu wa serikali wameyaona yote yaliyotokea baada ya JPM kufariki dunia kabla ya kutekeleza mambo yote ya maendeleo ambayo serikali yake iliyaahidi, hivyo msiba wake utakuwa somo tosha kwao; kwamba wanyonge wanategemea mengi na makubwa kutoka kwao.

Tulimsikia juzi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akishindwa kuzungumza bungeni wakati wa kuaga mwili, akisema alikuwa akijisikia vibaya kuona mwili huo ukiwa umelala mbele yake, lakini somo kwao ni matukio waliyoyaona wananchi wakimuaga Magufuli mitaani na barabarani.

Tunawashauri viongozi wetu wauchukulie msiba huo kama fundisho kwao katika kukidhi matarajio ya Watanzania, hususan kwa kuendeleza mambo makubwa aliyoyaacha ili isionekane ameacha ombwe.

Columnist: ippmedia.com