Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mradi gesi kinyesi unavyohamisha wananchi kutoka umaskini wa kuni

Jikoa 2 (2)= Pg 11 12 Mradi gesi kinyesi unavyohamisha wananchi kutoka umaskini wa kuni

Fri, 12 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mbadala; muda, mateso na bajeti DC, wataalamu: Shida bado uelewa

NARIRI MATHAYO (43), ni mwanamke mwenye watoto watano. Ili apate nishati ya kupikia nyumbani, inamlazimu aamke alfajiri kila siku kwenda kufuata kuni.

Anasimulia kwamba alikuwa anatumia saa tano kufuata kuni kila siku na kuna wakati alirudi nyumbani na mzigo ‘kiduchu; kutokana na wingi wa wasaka kuni.

Nariri anayeishi kwenye nyumba ya udongo kijiji cha Oldonyowas katika Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, anasema ni safari iliyomchosha mno, katika maisha yake ya kila siku.

“Kuna muda mvua ikinyesha, huwezi kwenda msituni kutafuta kuni hii...inanibidi nikanunue kuni nne kwa Sh 1,000 ili niweze kupika na maisha ya hapa kijijini ni magumu, kuipata hiyo hela ni mtihani,” anasema.

MAISHA MAPYA

Kama ulivyo usemi kila jambo lina mwisho, safari ndefu za Nariri kutafuta kuni, sasa zimeisha baada ya kuanza kutumia nishati ya kinyesi cha ng’ombe maarufu kama baiogesi.

“Nilivyoanza kutumia baiogesi kama nishati mbadala kwa ajili ya kupikia baada ya kuhamasishwa, nikaona ni mkombozi wa maisha yangu. Saa tano ni nyingi kupoteza kila siku,” anaeleza.

Kijiji Oldonyowas, kilianzishwa mwaka 1975, zao la operesheni vijiji, umbali wa kilomita 35 kutoka mjini Arusha. Bado hakina umeme licha ya kuwepo nguzo kubwa inayopita kijijini hapo.

Arusha, imo katika orodha ya mikoa inayotumia kuni kwa asilimia 61.3 ya wakazi, nyuma ya Simiyu inayoshika nafasi ya kwanza kwa asilimia 94.3, kwa mujibu wa Ripoti ya Upatikanaji Nishati Tanzania Bara, 2016 ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Baada ya kubainika ukataji mkubwa wa miti kijijini hapo, ilitafutwa njia mbadala kuwasaidia wananchi, ambayo ni kinyesi cha ng’ombe.

Kampuni ya Oikos yenye makao makuu nchini Italia, ilifadhili mtambo wa baiogesi kwa gharama ya Sh. milioni 2.5 na wananchi walitakiwa kulipa kwa Sh 215,000. Lengo ni kutetea mazingira yao.

“Mwaka jana nimeanza kutumia nishati mbadala ya kinyesi cha ng’ombe nililipa Sh. 215,000 kwa ajili ya kupatiwa vifaa kama mabomba na jiko la kupika,” anasema.

Mama huyo anaeleza muda aliyotumia kutafuta kuni, sasa anatumia kwa shughuli nyingine kama vile kilimo na kupika chakula kwa wakati.

Ili mtambo huo ufanye kazi, Nariri anasema anatakiwa kuweka ndoo tatu za kinyesi laini cha ng’ombe.

“Huwa najitahidi kuhakikisha kila siku nalisha mtambo ili nipate gesi nyingi ukiweka kinyesi kidogo utapata gesi ndogo,” anasema.

ALIVYOJIUNGA

Katika kuhakikisha anaipata nishati hiyo ya kupika, ilimbidi aende kukopa kiasi cha Sh 115,000 kwenye kikundi, kwani haikuwa rahisi kupata fedha hiyo kwa mkupuo.

“Niliuza mboga na mayai kupata marejesho haikuwa ni jambo rahisi naamini ilikuwa ni mipango ya Mungu kuipata hii baiogesi,” anasema Nariri, akifafanua mkopo unaopaswa kurejeshwa katika miezui sita.

MAGEUZI KIJIJINI

Matumizi ya baiogesi yamefanya wanakijiji hao kupunguza gharama za maisha, wanaokoa fedha za kuinunua kuni na wanazitumia kwa mengine ya maendeleo.

Neema Lucas, ni mwanakijiji anayesema walikuwa wananunua kuni za Sh.12, 000 kwa wiki hivyo tangu wamepata biogesi hawanunui tena wala kwenda kutafuta kuni.

Licha ya kuwa ni mwanamke wa kawaida, Neema ana ujuzi kafunzwa taaluma kwa mapana, ikiwamo kujua kiwango cha gesi.

“Ili ujue gesi ipo nyingi itaanza kusoma kuanzia namba nne na kuendelea na pale unapokuwa mdogo inakulazimu kuweka kinyesi,” anasema kwa kujiamini huku akitaja changomoto inayowakabili sasa ni ulegevu wa mabomba unaosababisha upotevu wa gesi.

Wanufaika wakuu wa mradi ni wenye mifugo mingi inayozalisha kwa wingi kinyesi kupata nishati hiyo.

Donatha Abraham, anasema kutokana na wingi wa ng’ombe zake, imekuwa rahisi kupata kinyesi kwa wakati kulisha mtambo.

“Ni bora kujaza kinyesi katika mtambo kuliko ule umbali wa kutafuta kuni si unajua hawa wanaume zetu haijalishi ni mjamzito utakwenda kutafuta kuni... nilikuwa nachoka ukiwa na ujauzito uende huko msituni acha tu ...hii nishati imenisaidia,” anasema.

Kwa sasa mama huyo anasema anapata angalau muda wa kufanya shughuli zake nyingine.

GHARAMA KIKAWZO

Wakati wengine wapo wanaopambana hadi kukopa ili kupata baiogas, Monica Mollel kwake yote yameshindikana na kumfanya aendele kuiona kwa jirani, binafsi anabaki kwenye kuni.

Mollel anasema kipato chake ni kidogo na kuna wakati anakosa kutimiza milo ya chakula hivyo hatoweza kumudu biogas.

“Nashindwa kuweka akiba ya kulipia hizo gharama ila napenda kutumia hiyo nishati maana naona wenzangu inawasaidia hawaendi tena kukata kuni,” anasema Magdalena Loshije.

Magdalena anasema, wao kinamama wa jamii ya kimasai wanategemea vibarua vya kilimo cha karoti na fedha anayoipata inaishia kulisha watoto, kugharamia masomo na mahitaji madogo.

MASAHIBU YA KUNI

Kwa wanaoendelea na ukataji kuni kutokana na kukosa nishati ya baiogasi, wanalalamika kukutana na masahibu lukuki mengine yakihatarisha maisha yao.

Paulina Julias, anasimulia aliambiwa ‘aruke vichura’ akamjulisha kuwa hawezi ni bora akachapwa wakamsamehe.

“Wakati mwingine ukishindwa hizo adhabu inamuweka mtu katika mazingira ya kubakwa, mbali na hilo tunaumia wakati unakata kuni huko msituni na wakati mwingine tunarudi na vidonda,” anasema.

WAWEKEZAJI JE?

Ili kutekeleza mradi huo Oikos, ilitafuta kampuni ya ujenzi ambayo iliyotoa mafunzo kuhamasisha wananchi kutumia nishati hiyo na kuwajengia mtambo wa baiogesi.

“Wenye mradi walikuwa wakitafuta kampuni baada ya kutangaza, nilipatikana mimi na kazi kubwa niliyopewa ni kuwaelimisha wananchi kuhusiana na nishati mbadala, nikamjenga mmoja na wengine wakapenda,” anasema Ombeni Urio, Msimamizi wa Ujenzi wa Mtambo wa Baiogesi.

Urio anasema mradi ulikuwa wa bure kwa wananchi, waliotakiwa kuwa na mawe pamoja na kuchimba shimo.

Anasema baadhi ya wananchi waliona usumbufu kuzoa kinyesi na kukikoroga, kwamba kazi ngumu, kwani ni lazima uwekewe kinyesi ili kiweze kuzalisha na mtu anapona usumbufu, uhai wa mtambo unaigia hatarini.

VIONGOZI KIJIJI

Pamoja na kuwapo mitambo hiyo, viongozi wa kijiji hicho wanasema hawajui ni wangapi waliofungiwa nishati hiyo.

Mwenyekiti wa kijij, Laran Mollel, anasema hana takwimu halisi ya wananchi waliofungiwa mtambo huo wa nishati mbadala kijiji kwake, kunakokadiriwa kuwa na jumla ya wakazi zaidi ya 4,000.

Anasema, Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012, inaonyesha kijiji kilikuwa na watu 2,544 wanawake 1,331 na wanaume 1,213.

“Sehemu kubwa ya hiki kijiji hakina umeme licha ya nyaya kupita hapa...wengi wao tumeambiwa tutaletewa umeme mpaka sasa bado,” anasema Ofisa Mtendaji wa Oldonyowas, Jenifer Mcharo.

WATAALAMU

Ofisa Mradi wa Nishati Safi na Usawa (TANGSEN), Thabit Mikidadi, anasema gharama walizopewa ni nafuu kwa mitambo ya baiogesi inauzwa gharama kubwa kuanzia Sh.700, 000.

“Kama wamefadhiliwa sio jambo baya wafadhili wengi wanataka ulipie hata kidogo, ili uwe na uchungu nacho katika kukitunza bila hivyo hao wananchi hawataithamini hiyo baiogesi,” anasema.

Mikidadi anasema kuna mambo mawili kuendeleza baiogesi, la kwanza ni kutoa elimu kwa wenye kipato katika familia kuhusu umuhimu wa nishati hiyo ambayo ni rahisi katika matumizi.

Anaendelea: “Njia nyingine wanaweza kusaidiwa kulipa kidogo kidogo kwa muda utakaopangwa kuliko kulipa fedha zote kwa wakati mmoja.”

DC MURO

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro, anasema matarajio ni kuleta wafadhili ili wasaidie kijiji hicho ili kinyesi cha ng’ombe kiwe mbadala wa ukataji wa kuni.

Anasema mradi ulipokwisha wananchi wameibuka na changamoto ya uelewa jinsi ya mradi kuwa endelevu na wengine wamebaki kuitegemea serikali na wadau wa maendeleo kutaka wasaidiwe muda wote.

Muro anasema, mradi umelenga kufikia kaya 15,000 kwa awamu kutegemea na fedha ya mfadhili na kwa sasa umetekelezwa kwa asilimia 85 na utakuwa ni endelevu.

Columnist: www.tanzaniaweb.live