Yanga kuchukua ubingwa? Sio habari kubwa sana. Hata watani wao Simba kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu sio habari kubwa sana. Wamechukua mara ngapi? Nani ana ubavu wa kuwaondoa katika utawala wa soka? Fikiria kwamba mara ya mwisho kwa timu nyingine kuchukua ubingwa nje ya wao ilikuwa Azam miaka kumi iliyopita. Msimu wa 2013-2014.
Wanakifanya wanachokitaka katika soka letu. Habari mpya ni hizi ambazo Yanga wanatupa kwa sasa. Kwenda nusu fainali michuano ya Shirikisho Afrika, kuna uwezekano wakaingia hatua ya fainali. Wanahitaji kulinda mabao yao mawili waliyoyapata Temeke katikati ya wiki iliyopita.
Bao moja lilifungwa na Stephane Aziz Ki, halafu jingine likafungwa na Bernard 'Super Ben' Morrison. Na huyu aliyefunga bao la pili ndiye ninayetaka kumzungumzia leo. Naona yupo katika dakika zake za majeruhi za kujaribu kuuutetea mkataba wake Yanga. Hii ndio mida yake baada ya kutoweka uwanjani kwa muda mrefu.
Tazama alivyofunga lile bao. Alipopokea pasi kutoka kwa Fiston Mayele tazama akili yake ya haraka haraka kuubetua mpira dhidi ya kipa wa Mirumo Gallants pamoja na beki wake. Wao walikwenda chini wakiamini kwamba Ben angeupiga mpira chini lakini yeye kwa haraka haraka akaubetua.
Alifanyiwa madhambi huku mpira akiwa ameshauvusha. Kama asingefunga basi mwamuzi angelazimika kuweka penalti. Lakini Morrison hakutaka kumpa wakati mgumu mwamuzi aliyepo uwanjani wala wale waliokuwa chumba cha VAR. Akafunga katika 'angle' ambayo ilikuwa ngumu.
Wachezaji wetu wengi wenye akili za kawaida huwa wana papara pindi wakitazamana na kipa. Pale wangeweza kupiga chini na kipa angecheza. Lakini hata kama wangejikuta katika nafasi ile ambayo Morrison alikuwepo basi wangeweza kuupiga ule mpira nje. Hata hivyo haikuwa hivyo kwa Morrison. Alifunga katika 'angle' ngumu.
Ni katika mechi kama hizi ndipo Morrison anapowachanganya akili viongozi wa mpira wetu. Hachezi mechi nyingi za msimu, lakini hizi chache anazocheza zinakuacha mdomo wazi na wakati mwingine unaamini kwamba umetoka kumuona winga bora zaidi nchini. Hata hivyo tabia zake zinatia shaka huku kiwango chake kikiacha uchonganishi mkubwa kati ya viongozi na mashabiki.
Viongozi huwa wanapagawa na wanachotamani ni kuishi kwa matumaini huku wakitoa ile kauli ambayo hata mashabiki wamezoea. Kwamba "huyu jamaa akitulia atatubeba sana, tatizo hatulii". Mara ngapi tumesema hivyo kuhusu Morrison. Kuanzia kwa mashabiki, viongozi, wachambuzi na makundi mengineyo ya watu wa mpira.
Na sasa nafahamu kwamba kuna viongozi wa Yanga walishajiapiza kutompa tena mkataba mpya Morrison. Amecheza mechi chache msimu huu. Ametoweka mara kadhaa. Hata kocha, Nasireddine Nabi hana furaha sana na Morrison.
Lakini mwenyewe ameanza kampeni yake ya chini chini. Kampeni ya kupata mkataba mpya hapa nchini. Iwe kwa Yanga, watani zao Simba au hata Azam. Ana mechi kadhaa mkononi ambazo zinaweza kubadili mawazo ya kila mmoja wetu. Mwenyewe anafahamu hili kwamba anacheza kwa ajili ya hatima ya soka lake katika dakika hizi za majeruhi.
Ana mechi ya marudiano dhidi ya Marumo Gallants kama akifanikiwa kusafiri kwenda Afrika Kusini maana tunasikia kwamba ana matatizo na mamlaka za dola za nchi hiyo. Hakusafiri wakati Simba walipokwenda kucheza na Kaizer Chiefs na kisha Orlando Pirates. Inatajwa ni kwa sababu hizo.
Lakini kama Yanga wakienda fainali basi Morrison atakuwa na mechi mbili za kubadili mawazo ya Yanga. Atakuwa na mechi mbili za Ligi Kuu zilizobaki dhidi ya Mbeya City na Prisons. Kisha anaweza kuwa na mechi mbili za JKombe la Shirikisho la Azam. Pambano dhidi ya Singida Big Stars, lakini wakishinda basi pambano la fainali.
Ben anajua kubadilisha mawazo ya watu katika mechi chache tu. Jaribu kufikiri kwamba hata Simba hakuchezs mechi nyingi lakini kuna mechi chache alizocheza ziliwatamanisha Yanga wamrudishe tena. Mojawapo ni pambano kati ya Simba na Zanaco. Uwanja ulijaa maji lakini Morrison akaufanya uonekane kuwa mzuri tu.
Tatizo kubwa la Morrison ni kwamba yupo kama alivyo. Unatamani ajirekebishe lakini unagundua kwamba yupo kama alivyo. Binafsi niliamini kwamba pindi angerudi Yanga angeacha utukutu kwa sababu hii ingekuwa fursa ya mwisho kwake kucheza timu hizi mbili kubwa nchini. Sikuwa sahihi. Ben aliendelea kuwa yule yule na kuna viongozi wa Yanga wamemnunia.
Nilikuwa nimeona wazi kwamba mwenyewe angegundua kwamba hakuna nafasi ya kucheza tena Simba hasa baada ya kuwepo kwa mikingamo na migogoro mingi baina yao baada ya kuvuka boda na kwenda kucheza Msimbazi. Nilikosea. Alitua Yanga na akaendelea kuwa mtu. Ilifikia mahala walijiapiza kwamba hawatamuongezea tena mkataba.
Lakini sasa nataka kuona 'utapeli' wake. Na nataka kuona kama akizitumia hizi mechi vema uongozi wa Yanga utaweza kufanya nini juu yake. Lakini kama sio Yanga, je Mnyama anaweza kubadili mawazo na kufikiria kumchukua tena kwa mara nyingine? Hili sina uhakika nalo.
Labda watu wa Azam wanaweza kufikiria kwamba wana uwezo wa kumbadilisha tabia zake. Waliwahi kufikiria hivyo kwa Ibrahim Ajibu lakini haikuwalipa. Mwishowe wakanyoosha mikono kumruhusu aondoke klabuni hapo na kwenda Singida kucheza soka. Ni kitu kinachowezekana. Azam wanatamanisha.
Lakini kwa Yanga mtihani huu wanaupata kwa sababu ya mawinga wao wengine wawili, Tuisila Kisinda na Jesus Moloko kushindwa kuwa na mwendelezo wa ubora kila mara. Walau Moloko alijitafuta kidogo mwanzoni mwa msimu lakini Tuisila habadiliki sana. Alipika bao zuri kwa Aziz Ki Jumatano ile na kama angekuwa anafanya vile karibu kila wiki naamini sasa hivi angekuwa anatamba barani Ulaya.
Wakati wao wakiwa hivi, hapa nchini tuna tatizo pia la mawinga. Tangu Simon Msuva aondoke nchini ni ngumu kupata jibu kutoka kwa mawinga waliopo nchini. Tangu Mrisho Ngassa amalize mpira wake imekuwa shida pia kupata wachezaji wa aina yake. Ndio maana mtu kama Morrison anaweza kutuchezea kadri anavyojisikia.
Na sasa ameanza kurudi katika ubora wake wa kuchanga karata za mwisho. Anapambana vilivyo. Kwa wenzetu mchezaji wa aina yake au ambaye inaonekana umri umesogea huwa anapewa mkataba ambao maslahi yake yatalipwa kwa kadri anavyocheza mechi zake. Labda kitu hiki tu ndio ambacho kinaweza kumbana Morrison.