Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Morocco, kipimo cha ndoto zetu za alinacha

Taifa Stars Saudia Morocco, kipimo cha ndoto zetu za alinacha

Tue, 21 Nov 2023 Chanzo: Dar24

Unataka kwenda Kombe la Dunia pale Marekani, Canada na Mexico? Jibu ni rahisi tu. Leo cheza na Morocco kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. Tawala mechi. Shinda mechi. Shinda huku dunia ikiona wazi kwamba umeshinda.

Baada ya miezi kadhaa cheza nao tena pale Casablanca au Rabat halafu pata walau sare na timu hii ambayo mwishoni mwa mwaka jana ilifanya maajabu ya kuwa timu ya kwanza kutoka Afrika kutinga katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia pale Qatar.

Sina ndoto na Kombe la Dunia. Naona tunataka kuwatia vijana katika huzuni isiyo na sababu. Wanasiasa wameanza kuingia kati tena baada ya Taifa Stars kuichapa Niger pale Marrakech, Jumamosi jioni. Naamini Kombe la Dunia sio anga zetu kwa sasa.

Tunachoweza kufanya ni kujaribu kushindana katika mechi hizi kwa ajili ya mambo matatu. Kwanza ni kuongeza pointi katika msimamo wa viwango vya ubora vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa). Pili tunapaswa kuzitumia mechi hizi kwa ajili ya kuendelea kuimarika kama timu.

Tatu tunapaswa kuzitumia mechi hizi kama sehemu ya kujipima kuelekea katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Ivory Coast, Januari mwakani. Kuwapa presha wachezaji wetu kwamba wanatakiwa kwenda Kombe la Dunia 2026 sio sawa.

Kombe la Dunia lina viwango vyake. Kombe la Dunia sio kitu cha masihara. Wote tuliona kilichotokea Misri 2019 baada ya miaka 30 ya kujaribu kutinga michuano ya Mataifa ya Afrika kwa mara ya pili. Tulicheza mechi za soka kwa aibu kidogo.

Wachezaji wetu walishindwa kupiga pasi nne. Mtangazaji mmoja wa michuano ile alihoji ni namna gani Taifa Stars ilifanikiwa kutinga katika michuano ile. Haikuwa dharau. Alikuwa anasema ukweli. Kina David Mwantika walishindwa kupiga walau pasi tatu.

Kuanzia pale mpaka sasa walau tumeanza kucheza, lakini bado sidhani kama tupo tayari katika kiwango cha kuiwakilisha Afrika kwenye michuano mikubwa duniani. Naamini tutakwenda Ivory Coast na tutajaribu kuufanya mpira utembee. Boli litatembea kuliko kilichotokea Misri.

Idadi ya wachezaji wanaocheza nje imeongezeka. Sasa hivi tunatuma tiketi zaidi ya 14 kwa wachezaji wanaocheza nje. Sawa, hawachezi Manchester City, Arsenal, PSV, Borussia Dortmund au Napoli, lakini kidogo mpira wanautembeza.

Na hapohapo kuna wachezaji wetu ambao wanacheza timu kubwa kama Simba na Yanga na wamekuwa wakinufaika kwa kucheza kiushindani zaidi katika michuano ya CAF. Hii imeisaidia timu ya taifa kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, Kombe la Dunia ni sayari nyingine.

Twendeni Ivory Coast tukautembeze mpira. Baada ya hapo tuwe watu wa kudumu katika michuano hii ya Mataifa ya Afrika. Na sio tu tuwe watu wa kudumu, hapana. Tuwe tunashindana hasa katika michuano hii, baada ya hapo tunaweza kuwaza Kombe la Dunia.

Lakini hili la kuwaza Kombe la Dunia linapaswa kuandamana na kuendelea kuimarika kwa wachezaji wetu katika viwango vya kimataifa. Wachezaji wetu wasogee zaidi katika ligi mbalimbali zinazoeleweka barani Ulaya.

Jana tu nilikuwa namlalamikia kijana wetu, Kelvin John kwamba kiwango chake kimedumaa kwa sasa na hatuoni mwanga. Wachezaji kama yeye ndio ambao walipaswa kuungana na Mbwana Samatta na Novatus Dismas kuupeleka mpira wetu juu zaidi.

Hatuwezi kuliwaza sana Kombe la Dunia tukiwatumainia zaidi wachezaji wazawa wanaocheza Simba na Yanga. Kombe la Dunia ni kitu kingine. Ni sayari nyingine. Ukiwauliza Waafrika wasio na upande wowote kwamba nani akaiwakilishe Afrika katika Kombe la Dunia kati ya Tanzania na Morocco wengi watakuambia Morocco ni mwakilishi sahihi.

Hata mimi ukiniuliza nani ni mwakilishi sahihi wa Kombe la Dunia kati ya Morocco au majirani zetu DR Congo nitakuambia Morocco ni mwakilishi sahihi zaidi. Ukiniambia nani mwakilishi sahihi wa Kombe la Dunia kati ya Zambia na Senegal nitakuambia Senegal ni mwakilishi sahihi.

Uzalendo sio kusema uongo. Uzalendo sio kujidanganya. Tusije kuwashambulia wachezaji wetu kwa sababu wameshindwa kwenda Kombe la Dunia. Tuanze kuambiana ukweli kwa kile ambacho tunakitamani halafu tuendelee kuwekeza.

Hawa Wamorocco wamewekeza katika kila njia. Wamewekeza sana katika soka la vijana. Wakawekeza katika klabu ambazo zimeendelea kusumbua Afrika, halafu wamewekeza kwa watoto ambao wamezaliwa Ulaya kina Sofyan Amrabat, Hakim Ziyech, Achraf Hakimi na wengineo. Hawakufika nusu fainali za Kombe la Dunia kwa bahati mbaya.

Kuna nchi zimewekeza katika soka la ndani, lakini linapokuja suala la Kombe la Dunia maji yanakwenda shingoni. Mfano ni rafiki zetu Misri. Tazama namna ambavyo kwa muda mrefu walishindwa kufuzu kucheza Kombe la Dunia licha ya klabu zao kutamba katika soka la ndani la Afrika.

Na hata walipokwenda Kombe la Dunia baada ya miaka mingi kupita bila ya kufanya hivyo, walishindwa kuvuka walau makundi licha ya Waafrika wengi kuweka mioyo yao kwao. Hii ndio namna ambayo inakwambia Kombe la Dunia ni sayari nyingine.

Mwisho wa siku acha vijana wetu wafurahi. Wakishindwa tusiwazodoe na kuwatolea maneno machafu kama ambavyo mashabiki wamekuwa wakifanya. Hii majuzi tulifungwa na Uganda katika pambano la kuelekea kufuzu kwenda Ivory Coast na watu wakawaweka katika vitanzi wachezaji. Bahati nzuri tu walikwenda kupindua kibao kule Algeria.

Sawa, ni kweli kwamba Kombe la Dunia halina mwenyewe na ndio maana tupo katika ratiba, lakini tusiwaweke vijana wetu katika presha kubwa. Tuache wafurahie maisha. Tusiwe wanyonge kwa timu kama Niger, lakini lazima tukiri ubora wa viwango vya kina Morocco.

Kwenda kucheza na kina Kylian Mbappe, Harry Kane, Bukayo Saka na wengineo ni ndoto inayotisha. Kabla ya kuwaza kwenda huko tawala pambano la soka dhidi ya Morocco kwenye Uwanja wa Mkapa kisha pale Casablanca. Tawala pambano dhidi ya Zambia pale Lusaka kisha Uwanja wa Mkapa.

Columnist: Dar24