Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Morocco haikuwa kazi rahisi

Morocco Pic Morocco haikuwa kazi rahisi

Tue, 13 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Ukiwaangalia raia wa Morocco namna wanavyopata raha kupitia soka, unaweza ukatamani kuwa kama wao, au hata ukatamani kuungana nao, lakini ukweli ni kwamba hata nchi yako inaweza ikawafikia na ukawa kama wao, hawajafika pale kwa bahati mbaya, walijipanga, waliwekeza, wakasubiri na leo wamepata walichokuwa wanakikosa.

Nimekuwa mmoja kati ya wadau wakubwa wa Morocco, nimekuwa na ukaribu na baadhi ya viongozi wa chama hilo, ukiwasikiliza mipango yao, utaamini kwamba hawa hawapo hapa kwa bahati mbaya, wamechora ramani ya muda mrefu sana iliyowafikisha walipo.

Ukianzia kule upande wa klabu, bingwa mtetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa sasa ni Wydad Casablanca ya nchini kwao, bingwa mtetezi wa Kombe la Shirikisho Afrika ni RS Berkane ya kwao, bingwa wa Ligi ya Mabingwa kwa Wanawake ni AS FAR ya kwao.

Wamechukua kila kilichostahili kuchukulika. Ukirudi kwenye timu zao za taifa Morocco imefuzu Kombe la Dunia bila ya kupoteza mechi, timu yao ya wasichana wa umri chini ya miaka 17, ilifuzu Kombe la Dunia kule India, timu yao ya wanawake ya wakubwa imefuzu Kombe la Dunia litakalofanyika mwakani kule Australia na New Zealand, baada ya kufika fainali ya AFCON na kufungwa na Afrika Kusini.

Nilikuwa nazungumza na mmoja kati ya wajumbe wa Shirikisho la Soka la Wanawake ambaye pia ni mtendaji mkuu wa timu ya ASFAR ya Wanawake, Bahya Elyahmidi akaniambia: “Lengo halikuwa kuchukua AFCON ya Wanawake, tulijiandaa muda mrefu na mpango mama ulikuwa ni kufuzu Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza kwenye historia yetu na tumefanikiwa.”

Hapa chini ni baadhi ya mambo ambayo chama cha soka cha Morocco na serikali ya nchi hiyo imeyafanya na hatimaye yamewafikisha hapa walipo.

Viwanja nyasi bandia

Baadhi ya wachezaji wa Kitanzania wanaocheza soka nchini humo wamethibitisha kwamba kumekuwa na viwanja vingi sana vya nyasi bandia katika maeneo mbalimbali na vingine havina hata ukubwa sana.

Rais wa chama cha soka cha Wanawake nchini humo, Illa Khadija aliniambia kwamba lengo la kutengeneza viwanja vingi vya nyasi katika maeneo mbalimbali ni kufanya mpira uchezwe kila mahali na kupata idadi kubwa ya wachezaji.

Vilevile viwanja hivyo vilijengwa ili kuufanya mchezo wa mpira wa miguu kuwa karibu sana na watoto wadogo ambao ndio kesho na hatma ya soka la nchini humo.

Kila mkoa una walau viwanja vitatu au vinne vya nyasi bandia na kwenye ile mikoa mikubwa kama Casablanca na Rabat, huko ndio kuna kufuzu kwa sababu kuna viwanja vya nyasi asilia na bandia zaidi ya 10 katika maeneo mbalimbali.

Makocha nchi nzima

Kama kuna sehemu sio kazi sana kusoma ukocha basi ni Morocco, moja kati ya mambo ambayo Morocco waliyaangalia kwenye mpango wao wa kuwa taifa tishio Afrika na baadaye duniani ni kuwa na miundombinu bora, uongozi bora na baadaye kutambua vipaji.

Sasa kwenye kutambua vipaji na kuwa na viongozi bora wanaamini lazima uwe na makocha bora ambao ili uwapate lazima ukubali kuwekeza.

Asilimia 70 ya wachezaji raia wa Morocco kwa wanawake na wanaume wote huwa wana leseni mbalimbali za ukocha kuanzia D, C, B, na A za CAF.

Morocco ni moja kati ya sehemu ngumu sana kupata kazi ukiwa kama kocha, niliongea na mmoja kati ya wajumbe wa zamani wa Wydad Casablanca ambaye aliwahi kuwa rais wa timu ya Nassim iliyouzwa kwa Wydad Casablanca miezi kadhaa iliyopita, Sosalah Mohammed aliniambia kwamba: “Kuna idadi kubwa sana ya makocha nchi nzima, ukiwa hata na leseni B ni ngumu sana kupata kazi, tofauti na ilivyo sehemu nyingine.”

Mjumbe wa soka la Wanawake, Alli Foua aliniambia kwamba idadi ya makocha huwa inatofautiana kila mwaka kulingana na mikoa na wilaya, kuna wilaya hutoa makocha 30 kwa mwaka katika ngazi mbalimbali, kuna nyingine hutoa 50, 60 hadi 70 kila mwaka.

Kwa mfano wilaya ambayo anatokea yeye Assa Zag huzalisha makocha wasiopungua 30, kila mwaka na huko ni vijijini, kando kabisa kabisa ya nchi ya Morocco.

Baada ya kufundishwa na wakufunzi wa CAF, shirikisho la nchi hiyo huwa na utaratibu wa kuita wakufunzi hasa kutoka Ufaransa kwa sababu ya mfanano wa lugha, wakufunzi hao huwapa semina mbalimbali makocha waliohitimu ngazi husika. Jambo hili hutokea kila mwaka.

Ruzuku

Nafahamu kwa soka la wanawake, kila mwezi shirikisho la soka la Morocco huwa linatoa Dirham 35,000 kila mwezi kwa kila mchezaji wa Ligi Kuu kama mshahara, hiyo ni mbali ya pesa ambazo wachezaji watapewa na timu zao.

Kiasi hicho cha Dirham kinakaribia Shilingi 800,000 za Kitanzania.

Mbali ya Ligi Kuu kwenye Ligi Daraja la kwanza kila mchezaji hupewa Dirham 25,000 ambayo ni sawa na 500,000 za Kitanzania.

Kila kocha hupata Dola 500 kila mwezi, kila timu inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake na Ligi Daraja la Kwanza hupewa basi kwa ajili ya safari za kwenda kwenye mechi na mazoezi.

Kwa haraka haraka shirikisho la soka la Morocco hupoteza zaidi ya Dola 200,000 (Sh465 milioni) kila mwezi kwenye kugharamia tu soka la wanawake na kwa upande wa wanaume huwa ni zaidi kwa sababu huhitajika kualika wakufunzi, kulipa makocha na maskauti kwa ajili ya kusaka vipaji na hata kutoa ruzuku kwa timu pia.

Akademi

Mwaka 2009, mfalme wa nchi hii, Mohammed VI alipitisha mpango wa kujengwa akademi kubwa jijini Rabat kwa ajili ya kuirudisha nchi huyo kwenye ramani ya michezo mbalimbali baada ya kupotea kwa muda mrefu.

Akademi hiyo iliyojengwa maeneo ya Sale, imegharimu zaidi ya Dola 70 milioni (Sh162 bilioni) hadi kukamilika kwake na ilichukua miaka mitatu kukamilika.

Imechukua heka 30 za ardhi na ndani yake kuna kila aina ya viwanja vya michezo iliyopo nchini humo, kubwa zaidi pia zimejengwa hoteli zenye hadhi ya nyota tano, nyota mbili na hosteli ambazo hutumiwa na mastaa pale wanapokuwa kambini, unaweza kusema hapo ndio jikoni.

Mwaka 2015, pia ulipitishwa mpango wa kutengeneza akademi ndogo ambazo zitakuwa zikiripoti kwa akademi hii, akademi hizo zipo mikoa yote 12 ya Morocco na kazi kubwa ya akademi hizo ni kuangalia vipaji vya wachezaji wa michezo mbalimbali na kuvituma huko Rabat ambako kuna sehemu ya kulelea wachezaji wa michezo yote.

Morocco ni katika nchi chache zenye ligi za vijana kwa upande wa wanawake.

Columnist: Mwanaspoti