Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mo Dewji atachoka Simba

MO Dewji Apinga Goli Walilofungwa Na Power Dynamos.jpeg Mo Dewji

Sun, 21 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kuna vitu vingine vinaumiza sana. Ni kama hili la mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa Klabu ya Simba. Limekaa muda mrefu na sasa linatia kizunguzungu.

Mchakato ulianza vizuri miaka saba nyuma. Alianza bilionea Mohamed Dewji kwa kuitisha mkutano na wanahabari kisha kuweka nia yake ya kuwekeza ndani ya Simba.

Kwa wakati ule Dewji alisema wazi anahitaji kununua asilimia 51 ya hisa za klabu ya Simba kwa kiasi cha Shilingi 20 bilioni. Ni fedha nyingi hata kwa kuzitamka tu. Zilikuwa fedha nyingi zaidi kwa wakati ule.

Wakati Dewji anataka kuwekeza Simba, bajeti yao kwa mwaka haikuwa inafika Shilingi 2 bilioni. Simba ilikuwa katika umasikini mkubwa. Maisha yao yalikuwa ya kuunga unga.

Simba haikumudu kusafiri kwenda mikoani kwa usafiri wa ndege. Walizurura na basi kama vile kampuni ya usafirishaji. Iliumiza sana.

Simba ingekwenda Songea kwa basi. Sio basi tu sema Coaster kwa masafa marefu kama hayo! Ingekwenda Bukoba na Mwanza kwa basi. Ilikuwa ni umasikini mkubwa.

Simba ilikuwa ikisajili wachezaji wa bei nafuu. Haikuweza kushindana sokoni na Yanga ya Yusuf Manji au Azam FC. Ilikuwa na hali mbaya sana.

Ilikuwa ni jambo la kawaida kusikia wachezaji wa Simba wamekaa miezi kadhaa hawajalipwa mishahara. Ilikuwa kawaida kusikia wengine wanadai fedha za usajili. Ilikuwa ni kitu cha kawaida.

Wakati huo Simba ilikaa miaka mitano bila kutwaa taji la Ligi Kuu Bara. Kuna misimu kadhaa ilimaliza katika nafasi ya tatu na ya nne. Haikuwa na ushindani tena. Iliumiza sana kwa mashabiki.

Ndio nyakati hizi Dewji alijitokeza na kusema anataka kununua asilimia 51 ya hisa kwa Shilingi 20 bilioni. Nani angekataa? Hakuna. Ilikuwa ni kama Nabii ameshuka kuja kuokoa kizazi kinachoteseka sana.

Baada ya nia ya Dewji kuwekeza, mchakato ukaanza mara moja. Serikali ikaja na mwongozo kuwa mwekezaji mmoja hawezi kuwa na hisa nyingi kuliko wanachama wa timu. Ilisema hizo ni timu za wananchi hivyo mwekezaji angetakiwa kuwa na asilimia zisizozidi 49. Walikuwa sahihi.

Kuna watu wengi walitoa jasho na damu zao kuanzisha timu za Simba na Yanga. Hawa ndio walipaswa kuwa wamiliki halali. Ni wazo ambalo hata Dewji mwenyewe alikubaliana nalo.

Uzuri ni kwamba baada tu ya Katiba ya Simba kubadilishwa na kuruhusu mfumo mpya kuanza kazi wakati taratibu nyingine za kisheria zikisubiriwa kukamilika, Dewji alianza kutoa fedha zake ndani ya timu. Alibadilisha karibu kila kitu.

Simba ikaanza kusajili wachezaji mahiri tena. Ikaweka kambi za maana. Ikafanya maandalizi yake nje ya nchi. Walikwenda hadi Ulaya mara kadhaa kutokana na jeuri ya fedha za Dewji.

Simba ikaajiri watendaji wenye wasifu mkubwa. Ndio nyakati hizi tuliona mtu kama Senzo Mbatha alikubali kutoka Afrika Kusini na kuja kufanya kazi Tanzania. Nani aliwahi kuwaza hilo? Hakuna. Ila iliwezekana.

Utawala wa Simba ukarejea tena kwenye soka la ndani. Ikatwaa mataji ya Ligi Kuu Bara kwa miaka minne mfululizo. Ni jambo ambalo lilionekana kuwa gumu sana lakini kwa uwekezaji wa Dewji ikawezekana kirahisi tu.

Baada ya miaka 15, Simba ikafuzu tena katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Mara ya mwisho ilikuwa 2003, ila miaka michache tu ya Dewji wakarejea tena kwenye ubabe wao Afrika.

Baada ya hapo ikawa ni kawaida kuona Simba inafika robo fainali kwenye mashindano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Ikawa kivutio kikubwa Afrika. Wachezaji wakubwa wakatamani kucheza Simba.

Ndio tunaona hawa kina Clatous Chama, Meddie Kagere, Luis Miquissone na wengineo wakasajiliwa Simba kwa gharama kubwa. Simba ikamudu kuwalipa mishahara mikubwa tena kwa wakati. Kwanini? Kwa sababu Dewji alikuwa akitoa fedha.

Thamani ya Simba sokoni ikapanda. Wadhamini wakaanza kuwekeza fedha nyingi ndani ya Simba. Bajeti ya Simba iliyokuwa chini ya Shilingi 2 bilioni ikapanda maradufu.

Msimu uliopita tu Simba ilikuwa na bajeti ya zaidi ya Shilingi 11 bilioni. Kwanini? Kwa sababu Dewji aliwekeza na kuhakikisha thamani ya klabu inakua juu. Pato la Simba likawa juu pia.

Hata hivyo, nasikitika kuona baada ya miaka saba bado tunazungumza kitu kile kile. Ule mchakato wa mabadiliko ndani ya Simba bado haujakamilika. Bado hadi leo Dewji hajawa mwekezaji rasmi. Inashangaza sana.

Majuzi nimeona tena Simba imeunda kamati nyingine ya mabadiliko ya Katiba yao. Sina hakika kama ndio inakwenda kumaliza tatizo la uwekezaji ama inaturudisha nyuma zaidi.

Ukweli ni kwamba Dewji amefanya alichopaswa kufanya kwa miaka mingi. Hili jambo lilitakiwa liwe limemalizika kitambo. Ila ni kama vile hakuna nia ya dhati ya kulimaliza.

Kuna nyakati amekuwa akilalamika kuwa itafika wakati atachoka na kuachana na jambo hilo. Ni kweli, hata ingekuwa wewe ungechoka. Ni mchakato gani usiokamilika kwa miaka saba? Inafikirisha sana.

Kama Simba hawatakuwa makini Dewji atachoka kweli. Ataondoka zake. Hakuna atakachopoteza. Simba itaanza kurudi nyuma tena. Hali itakuwa mbaya zaidi hasa katika nyakati hizi ambazo GSM anamwaga fedha za kutosha Yanga.

Kwa sasa Simba inatakiwa kuchagua moja. Kukamilisha mchakato ili iwe rasmi kuwa Dewji ni mwekezaji wao, ama kuachana na hilo jambo. Vinginevyo itakuwa ni kupoteza muda tu.

Columnist: www.tanzaniaweb.live