Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mnyama atashikilia bomba Casablanca kama Cairo 2003?

Simba Bomba Casablanca Mnyama atashikilia bomba Casablanca kama Cairo 2003?

Tue, 25 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ilitokea miaka 20 iliyopita. Umri wa kijana anayejiandaa kuwa na familia. Simba walishikilia bomba pale Cairo. Ni habari inayozungumzwa mara nyingi, kama vile sasa imeanza kuchosha lakini nyakati hizi ni wakati mwingine tena kukumbushana.

Simba walishinda bao 1-0 dhidi ya Zamalek katika Uwanja wa Taifa wakati huo tukiuita 'Shamba la bibi'. Baada ya hapo wakasafiri kwenda kucheza pambano la marudiano pale Cairo. Walifungwa bao moja katika pambano ambalo Juma Kaseja alikabiliana na mashambulizi makubwa kutoka kwa Zamalek waliokuwa na uchu.

Kama tungekuwa na takwimu ambazo dunia ya leo zimeshika hatamu basi inawezekana Zamalek walipiga mashuti 20 yaliyolenga lango na mashuti 17 ambayo hayakulenga lango. Inawezekana pia Zamalek walipiga kona zaidi ya 15. Mwishowe Simba waliishia kufungwa bao hilo hilo tu ambalo liliipeleka mechi katika dakika za nyongeza.

Dakika za nyongeza zilipokata roho, pambano likaenda katika penalti. Ni miaka 20 sasa lakini kwa sisi wengine ni kama juzi. Tunamkumbuka marehemu Christopher Alex Massawe akipiga penalti ya mwisho ambayo iliwapeleka Simba katika robo fainali. Kuna mchezaji mmoja wa Zamalek alikosa penalti. Simba walipata penalti zao zote. Walizipiga kwa umakini mkubwa.

Subiri kidogo. Ile ilikuwa mechi ambayo iliipeleka Simba robo fainali lakini miaka 20 baadae Simba wapo katika mazingira yale yale. Tofauti ni hadhi na mazingira. Juzi Simba walikuwa wanacheza na timu nyingine ya Afrika Kaskazini. Wydad Casablanca. Wakashinda 1-0. Wanahitajika kusafiri maili nyingi kwenda Casablanca kucheza pambano la marudiano.

Tofauti ni kwamba, mechi ile ya Cairo iliipeleka Simba robo fainali. Mechi hii ya Casablanca ni kusaka kwenda nusu fainali. Ni mechi ya machozi, jasho na damu. Ni mechi ya kushikilia bomba. Simba wataweza kushikilia bomba kama walivyofanya miaka 20 iliyopita? Hili ndio swali la msingi zaidi kwa sasa.

Ndani ya wiki tu Simba itakwenda Afrika Kaskazini kujaribu kutetea bao pekee lililofungwa na Jean Baleke juzi pale kwa Mkapa. Ni kazi chafu lakini lazima ifanyike. Simba watahitaji kushikilia bomba kweli kweli kama wanataka kurudia kile walichowahi kukifanya mwaka 2003.

Hapana, unaweza kusema kama wanataka kurudia kile walichokifanya miaka 49 iliyopita. Mwaka 1974 walikuwa timu ya kwanza na ya mwisho kutoka Tanzania kufika nusu fainali ya michuano ya Ligi ya mabingwa wa Afrika. Walicheza na Mehal el Kubra ya Algeria wakatolewa. Hakuna timu nyingine ya Tanzania ambayo imewahi kufanya hivyo. Labda kama Simba wataweza kushikilia bomba pale Casablanca.

Ni jambo linalowezekana? Sijui. Mwaka 2003 wakati walipofanya hivyo pale Cairo walikuwa na mchezaji mmoja tu wa kigeni. Ramadhan Wasso. Mwaka huu wana wachezaji wengi wa kigeni lakini mazingira yamekuwa tofauti. Na hawa Waarabu nao wameongeza ubora.

Kama ilivyo kawaida, juzi pale Temeke Wydad walijaribu kuficha ubora wao. Ndivyo walivyo. Mechi ya Casablanca haitakuwa kama hii ya juzi. Itakuwa ya hasira kutoka kwao ndani na nje ya uwanja. Unapozungumzia nje ya uwanja unaweza kuona namna walivyochafua hali ya hewa kwa kuwasha moto usio na sababu na kisha giza la ghafla kutokea uwanjani.

Wakiwa kwao hawatakuwa na adabu ndani na nje ya uwanja. Wataipelekea moto Simba ndani na nje ya uwanja. Kitu cha kwanza itakuwa kutaka kurudisha bao la Beleke na baada ya hapo wafanye mauaji ya kimbari. Ni hapa ndipo tutakapohitaji zile roho za kina Boniface Pawassa, Said Sued, Juma Kaseja, Suleiman Matola, Ulimboka Mwakingwe na wengine wote ambao waliziweka rehani roho zao usiku ule wa Cairo.

Kitu cha kujilaumu cha kwanza ni kwamba Simba walikuwa katika nafasi nzuri ya kujiweka katika mazingira mazuri kuliko yale ya miaka 20 iliyopita. Kama Clatous Chotta Chama angekuwa katika ubora wake Simba wangeweza kutanua uongozi wao kutoka katika bao moja kwenda katika mabao mawili.

Lakini kwa sababu hilo halikutokea sasa hivi wamejikuta katika mazingira yale yale ya mwaka 2003. Robertinho atakuwa shujaa wa kuandaa mpango mkakati wa kuitoa Wydad kwa kulinda ushindi wake wa Temeke au kujaribu kusaka bao la pili Casablanca?

Hili la pili litakuwa jambo humu kwake. Hili la kwanza ndilo ambalo anaweza kupambana nao. Vyovyote ilivyo haitakuwa mechi rahisi kwake na kuna mambo mengi anahitaji. Jingine ambalo anahitaji ni kipa wake, Aishi Manula kurudi uwanjani haraka iwezekanavyo. Kuna mtu anaweza kuhisi nina kichaa. Kwa nini Aishi wakati Ally Salim amecheza vizuri katika mechi mbili zilizopita?

Majibu ni mepesi. Katika mechi dhidi ya Yanga Salim alikuwa salama. Mambo mawili. Simba waliwadhibiti vyema Yanga. Pia inawezekana Yanga hawakuwa katika ubora wao. Hakukuwa na michomo ya hatari ambayo alikuwa ameifanya katika dakika zote 90.

Katika pambano la juzi Wydad hawakuwa wamefungua makucha yao. Ukiachana na habari ya kufungua makucha yao pia hawakufungua makucha yao majukwaani. Inatisha kuangalia kile ambacho wanafanya majukwaani wakati wanapocheza mechi muhimu ambayo inahitaji matokeo. Wanawatengenezea maadui zao ahera ingawa wapo duniani.

Aishi amewahi kucheza katika mazingira hayo. Ally hajawahi kucheza katika mazingira hayo. Afadhali langoni acheze Aishi kuliko Ally. Sio kwa ubaya. Ni uhalisia. Napenda namna gani ambavyo Ally anajiamini lango. Ilikuwa wiki ya mechi mbili ngumu lakini alijiamini ingawa ukweli uko wazi hakupewa mitihani migumu.

Robertinho pia inabidi akipange kikosi chake katika namna ya uimara kuliko ubora. Ana wachezaji wengi bora kikosini lakini anahitajika kupanga kikosi ambacho kitazingatia uimara kuliko ubora. Jose Mourinho alikuwa kocha bora katika jambo hili. Ni katika nyakati kama hizi na katika nafasi ya Chama rafiki yangu Mourinho angempanga Kennedy Juma.

Kitu cha msingi kwa Mourinho ingekuwa ni kushikilia bomba. Sioni sana ubora wa Simba katika kushinda Casablanca. Kitu ambacho wanapaswa kuonyesha ubora wao katika kushikilia bomba. Sio Simba tu, hata Mamelodi Sundowns wangepaswa kuonesha ubora wao katika kushikilia bomba pale Casablanca. Kama wangekuwa wamefungwa 1-0 pale Pretoria basi wangepaswa kwenda Casablanca kushikilia bomba. Majibu ya mechi hiyo ijayo anayo Robertinho. Haitakuwa kazi rahisi. Kama Simba atafanikiwa kushikilia bomba katika pambano hilo basi ataweza hata kuchukua kombe lenyewe. Atakuwa amemtoa bingwa mtetezi. Kama unamtoa bingwa mtetezi ni nani mwingine ambaye atakutisha?

Columnist: Mwanaspoti