Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mnyama alipoturudisha katika hesabu zinazowezekana Kampala

Simba SC Uganda 1140x640 Simba SC

Tue, 28 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ni mechi ambayo haitakumbukwa kwa mpira wowote mzuri, lakini nani anajali? Labda Vipers. Simba watakumbuka kwamba waliondoka uwanjani na pointi tatu muhimu. Hiki ndicho walichokihitaji kuliko mpira mzuri. Wakati mwingine unahitaji pointi tatu kuliko kila kitu kingine.

Bao lao lilikuja kupitia kwa beki mkongoman, Henock Inonga. Vichwa viwili ndani ya ndani ya boksi, halafu Inonga akausukumizia mpira katika nyavu za Vipers.

Ulikuwa ulinzi mbovu kutoka kwa walinzi wa Vipers, lakini kwa mara nyingine tena, nani anajali? Shauri zao. Si ajabu ndio maana wana pointi moja katika mechi mbili walizocheza nyumbani. Lakini wana pointi moja kwa ujumla baada ya mechi tatu huku wakiwa wamefungwa mabao sita.

Vipers walipoteza pasi zao ovyo na hawakuwa makini katika eneoa mwisho. Namna ambavyo walihamisha mpira kutoka nyuma kwenda mbele walionekana kuwa bora lakini katika eneo la mwisho walikosa umakini wa kutengeneza mashambulizi ya maana. Wana wachezaji binafsi wenye vipaji lakini kitimu bado wana uchanga mwingi katika kucheza kitimu.

Kama wangekutana na Simba ya miezi 36 iliyopita maisha yangekuwa magumu kwao. Bahati mbaya walikutana na Simba ambayo nayo kwa sasa imeanza kubutuabutua kutokana na kukumbwa na presha kubwa ya matokeo baada ya kupoteza pointi nyingi katika michuano ya kimataifa pamoja na Ligi msimu huu.

Na sasa Simba imeturudisha katika hesabu zinazowezekana katika kundi lake. Hii ilikuwa mechi muhimu kwao kama walitaka walau kushika nafasi ya pili katika kundi. Wanahitaji kushinda pambano jingine dhidi ya hawa hawa Vipers pale Temeke. Watakuwa na pointi sita mkononi. Hakuna masikhara katika hili. Wiki moja iliyopita walifungwa na Raja Casablanca pale Temeke.

Katika ule moto wao maarufu wa nyumbani hatoki mtu ambao huwa wanashinda mechi zao zote za nyumbani kabla ya kutafakari jambo jingine, ushindi huu wa Kampala utakuwa umefidia kichapo cha Raja. Kuanzia sasa warudi katika hesabu za kawaida.

Kwanza kabisa inabidi washinde mechi yao ya Temeke, lakini hapo hapo wafunge sala kuhakikisha Raja anaondoka na pointi zote tatu pale Conakry akienda kucheza na Horoya. Imeanza kunitia wasiwasi kidogo kwamba huenda Raja wasiisaidie kazi Horoya pale Conakry. Mechi yao ya juzi iliyochezwa katika ardhi ya Morocco haikuwa nyepesi ingawa Raja alishinda 2-0.

Simba wana pointi tatu wakati Horoya ana pointi nne. Endapo ataambulia sare au akimfunga Raja pale kwake atakuwa amejiweka katika nafasi nzuri. Kinachotia wasiwasi ni kwamba Vipers hawa ambao wanaonekana kuwa vibonde wa kundi wana safari ya kwenda Guinea kucheza pambano lao la mwisho dhidi ya Horoya.

Wakati huo huo, Simba watakuwa safari kwenda Morocco kucheza na Raja. Hesabu zozote ambazo zitaipitisha Simba katika kundi hili inabidi zipigwe kabla ya mechi hizi za mwisho. Lakini zaidi ni vizuri kuombea Raja ashinde ugenini kwa Horoya ili aweze kufuzu katika kundi akiwa na mechi mbili mkononi. Labda anaweza kucheza mechi zake mbili za mwisho dhidi ya Vipers na Simba akiwa hana hasira.

Hata hivyo, Simba wasilitegemee jambo hili kwa sababu daima Waarabu wanacheza kwa nidhamu kubwa, hasa wakiwa nyumbani wakihofia kutowaudhi mashabiki wao. Simba inabidi ijifanyie kazi nzuri katika mechi zake mbili za nyumbani zinazofuata.

Kwa sasa ni wazi kwamba washindani wao wakubwa ni Horoya. Simba inabidi wawafunge kwanza Vipers kisha wamalizane na Horoya katika uwanja wa Taifa. Pambano hili dhidi ya Horoya litakuwa ni kuua panya wawili kwa rungu moja. Kwanza watajipandisha lakini watamshusha Horoya pale pale walipo.

Zote hizi ni hesabu za vidole ambazo tumepata unafuu wa kuzifanya kwa sababu ya ushindi wa Simba Kampala juzi lakini ukweli ni kwamba sio lazima kila kitu kitakwenda kama kinavyofikirika. Simba walikuwa wanadai kwa Mkapa hatoki mtu lakini mbona Raja walishinda? Imefika mahala sasa Simba wapambane zaidi uwanjani.

Vipers au Horoya yoyote kati yao anaweza kutibua hesabu katika uwanja wa Taifa. Haitakuwa mara ya kwanza licha ya hivi karibuni kukumbushwa tena na Raja. Tangu ujio wa wachezaji wengi wa kigeni nchini timu zetu zimeimarika nidhamu lakini hapo zamani lilikuwa jambo la kawaida kwa timu za nje kuja kuharibu shughuli katika uwanja wa Mkapa.

Ndani ya uwanja Simba wanahitaji kuimarika zaidi katika safu ya ulinzi lakini pia kuwa na umiliki mzuri wa mpira katika eneo la kiungo. Safu ya ulinzi ya Simba inapitika kwa urahisi. Ni vile tu Vipers walikosa umakini katika eneo la mwisho la uwanja wangeweza kuondoka na matokeo mazuri katika pambano la juzi.

Silaha kubwa ya Simba kwa sasa ni viungo wao washambuliaji, Clatous Chama na Saidoo Ntibanzokinza ambao wana uwezo wa kutengeneza nafasi katika eneo la mwisho la uwanja, hasa Chama ambaye akili yake kubwa ipo katika kupika mashambulizi zaidi. Kibu Dennis alikuwa na mechi nzuri juzi lakini haitakuja kutokea Kibu akawa Luis Miquissone. Kuna kushuka kwa ubora ndani ya kikosi cha Simba lakini kwa sasa wanachoweza kufanya ni kuziba mwanya huo kwa kucheza kwa juhudi kubwa uwanjani.

Simba wanamuhitaji Moses Phiri aliye fiti zaidi katika hatua zinazofuata kwa sababu washambuliaji wetu wazawa, John Bocco na Habib Kyombo wanaonekana bado hawapo sawa katika michuano hii. Hii ni michuano ambayo unahitaji watu walio na umakini mkubwa.

Nje ya uwanja pia niliona kundi kubwa la viongozi wa Simba wakiwa wamekwenda Kampala. Bado utengano ni mkubwa. Wale waliokuwa upande wa mgombe aliyeshindwa nadhani walikacha kusafiri kwenda Kampala. Sidhani kama wamefurahishwa na matokeo waliyoyaona.

Simba kuna kundi fulani la watu ambalo linataka lionekane lina thamani kubwa dhidi ya wengine. Hapa ndipo inapoanzia migogoro isiyo na maana klabuni. Labda matokeo haya yataokoa mpasuko na pia kumfanya Mwenyekiti aliyepo madarakani apumue kidogo. Kama Simba isingepata matokeo Kampala basi hali yake ingekuwa mbaya kwa sasa.

Columnist: Mwanaspoti