Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

‘Mkapa ametuacha watetezi wa uhai katika mikono salama’

725ec9ce5faa7b9b11dbb67626feb808 ‘Mkapa ametuacha watetezi wa uhai katika mikono salama’

Mon, 3 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

Kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa kimewashitua wengi na kuleta simanzi kwa Watanzania. Wengi wanamkumbuka Mkapa kwa namna mbalimbali kutokana na jinsi alivyowagusa katika maisha na shughuli zao za kila siku.

Watetezi uhai chini ya Shirika la Kutetea Uhai Tanzania, (Pro-Life Tanzania), tunamkumbuka kwa namna ya pekee kutokana na jinsi alivyoshirikiana nasi kuhakikisha uhai wa binadamu, tangu kutungwa mimba hadi kifo, unalindwa na kutetewa.

Tunapenda kutumia maombolezo haya kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa kumuenzi Mzee Mkapa kwa kuulinda na kuutetea uhai wa kila binadamu, ambaye bado yumo tumboni mwa mama, aliyezaliwa, mtoto kwa mzee, mwanaume kwa mwanamke, mlemavu na asiye mlemavu.

Katika miaka hii ambapo uhai wa binadamu haupewi heshima na hadhi inayostahili, jukumu hili linakuwa siyo tu wajibu, bali wito wa kila mmoja. Nchi nyingi duniani zimetunga sheria za kuua uhai wa binadamu kabla ya kuzaliwa.

Bila huruma, baadhi ya wahudumu wa afya ama kupitia taasisi wanazofanyia kazi, au wao binafsi, wanatekeleza mauaji haya ya kimbari, wakishiriki katika kuondoa kizazi cha baadaye cha nchi zao.

Yapo mashirika ya hiari ya kitaifa na kimataifa yanayozishinikiza serikali za nchi ambazo hazijaridhia kisheria kuua watoto ambao hawajazaliwa kwa kutumia lugha laghai.

Mara nyingi tunashuhudia shinikizo kutoka mashirika hayo, yakiungana na yale yanayojiita ya Haki za Binadamu yakizitaka nchi kutunga sheria zinazohusu Haki ya Afya ya Kizazi na Ujinsia, eti kwa faida ya wanawake na watoto.

Tunamshukuru Mkapa kwa kutuunga mkono kuyapinga yote hayo katika enzi za utawala wake. Mwaka 1997 kulikuwa na shinikizo kubwa kutoka mashirika na taasisi kadhaa kuitaka Tanzania itunge sheria ya kutoa mimba.

Ili kupata uhakika wa minong’ono hiyo, Septemba 2, 1997 Pro-Life Tanzania tulimwandikia barua Mheshimiwa Mkapa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzana wakati huo, kutaka kuonana naye ili kupata ufafanuzi na uhakika wa jambo hilo.

Januari 16, 1998 shirika lilipata majibu kutoka Ofisi ya Rais kuwa, baada ya kufanya utafiti jambo hilo halikuwapo na hivyo hapakuwa tena na sababu ya kumtaka Mheshimiwa Rais akutane nasi kuzungumza jambo ambalo halikuwapo.

Tulishukuru kupata majibu hayo ya uhakika kutoka Ofisi ya Rais. Hata hivyo pamoja na uthibitisho huo, watu na mashirika yenye uchu wa kumwaga damu za watoto wasio na hatia yaliendelea na shinikizo la kulitaka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutunga sheria za kuruhusu wanawake kutoa mimba katika mazingira maalumu.

Ndipo Shirika letu likaandaa maandamano ya amani kuonesha kukerwa kwetu na mashinikizo ya kuhalalisha utoaji mimba na vitendo vya utoaji mimba. Maandamo haya yalifanyika Septemba 11, 1999 na kupokelewa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya, Tatu Ntimizi.

Katika hotuba yake, Naibu Waziri Ntimizi alisisitiza hoja ya azma ya serikali kulinda na kutetea uhai wa binadamu, hadhi na heshima yake. Akinukuu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ntimizi aliwathibitishia waandamanaji kuwa, Katiba ya Tanzania inalinda uhai wa kila binadamu na kwamba, vitendo vya kutoa mimba ni ukatili na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Tunamshukuru Mkapa kwa kuruhusu maandamano hayo kufanyika na kwa kuwahakikishia Watanzania azma ya serikali ya kuendelea kuuenzi na kuulinda uhai wa binadamu Shinikizo kubwa na la hatari zaidi la uwezekano wa kutungwa sheria ya utoaji mimba lilitokana na Itifaki ya Maputo iliyodai kuwa, msukumo wake unazipa wajibu nchi wanachama kuhakikisha zinalinda na kuboresha afya za wanawake, hususani afya ya uzazi.

Ingawaje kipindi cha Urais wa Mkapa kiliishia Novemba 2005, msimamo wake, ambao ndio msimamo wa serikali ulirithishwa kwa uongozi ulioshika madaraka baada yake.

Ndiyo maana Shirika letu likiamini kwamba msimamo wa serikali kuhusu katazo la utoaji mimba haujabadilika, lilimwandikia Waziri Mkuu (Januari 5, 2009) kuomba kuzuia shinikizo hilo kwa sababu ndani ya Itifaki ya Maputo vilikuwamo vipengele vya utoaji mimba.

Hoja yetu ilikuwa kuwa, kama utoaji mimba utaruhusiwa kwa kisingizio chochote, basi Tanzania itakuwa imefungua milango ya utoaji mimba hata pasipo sababu yoyote.

Vilevile tulihoji kuwa, kuua mtoto ambaye hajazaliwa siyo dawa kwa mimba iliyosababishwa na shambulio la aibu, wala kubakwa, wala mimba kuhatarisha afya ya mwili na akili ya mama au mtoto.

Tulijenga hoja kuwa, katika hali kama hizo, Wizara ya Afya iimarishe huduma za mama na mtoto kabla, wakati na baada ya kujifungua. Hakuna nchi duniani iliyotibu ugonjwa utokanao na mimba kwa kuua mimba hiyo.

Barua yetu ilijibiwa na Waziri Philip S. Marmo (Mbunge) ambaye alikuwa Waziri wa Nchi, Sera, Uratibu wa Bunge) mnamo Januari 30, 2009. Katika barua hiyo, Marmo anatuthibitishia kuwa:

“Japo Tanzania imeridhia itifaki hizo mbili, hakuna sheria yoyote iliyotungwa kusimamia au kuruhusu utoaji mimba.” Akaongeza: “Kwa domestication process (taratibu) nchini Tanzania kama ilivyo katika nchi nyingine ni kuwa, itifaki na mikataba ya kimataifa haiwezi kuwa sheria ya nchi hadi zitakapotungiwa sheria za Bunge…” Kwa bahati nzuri Bunge letu lilikataa shinikizo hilo.

Ndugu watetezi uhai kote nchini, hakuna hazina iliyo bora na kubwa kwa nchi yoyote kama hazina ya watu wake. Watu ndio nguvu kazi. Watu ndio mtaji wa maendeleo.

Watu ndio walinzi wa taifa. Watu ndio nguvu ya dini na imani. Ndani ya watu ndimo zilimo mbegu za uzazi. Ukiwaua unaliua taifa. Kwa mantiki hiyo tuna kila sababu ya kumshukuru na kumuenzi Mheshimiwa Benjamin William Mkapa kwa kuwa mtetezi mkuu wa uhai wa binadamu.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lazima ijivunie tunu hii azizi inayoendelea kurithishwa kutoka awamu moja ya uongozi hadi nyingine yaani, tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza iliyoongozwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Awamu ya Pili chini ya Mzee Ali Hassan Mwinyi, Awamu ya Tatu chini ya uongozi wa Mzee Mkapa, Awamu ya nne chini ya Jakaya Kikwete na hata sasa katika Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli.

Hongera viongozi wetu kwa kuthamini tunu ya uhai. Watetezi wa uhai wanaamini kuwa, hakuna Rais wa baadaye atakayemsaliti Benjamin Mkapa kwa kuruhusu nchi kupitia Bunge, kutunga sheria ya kuua watoto wete ambao hawajazaliwa na wanaotegemea upendo na huruma ya baba na mama, lakini hasa ulinzi wa uhai wao unaotolewa na serikali.

Shirika la Kutetea Uhai Tanzania linampa pole Rais Magufuli kwa msiba huu mkubwa. Aidha, linamshukuru na kumpongeza kwa kufuata nyayo za Mzee Mkapa kwa kusimamia ulinzi wa uhai wa kila Mtanzania, aliyezaliwa na yule ambaye hajazaliwa.

Rais Magufuli kama alivyokuwa Mkapa, daima amekuwa akitukumbusha Watanzania kuwa, watu ndio kichocheo cha maendeleo, bila watu hakuna maendeleo.

Anawahimiza Watanzania kuendelea kuzaa kwani nchi yetu itaendelea kuwa tajiri kwa kutokana na mtaji wa wingi wa watu wake wanaochapa kazi. Ndiyo maana Pro-Life Tanzania tunasema: “Kwa heri Mzee Mkapa, umetuacha pazuri na kwenye mikono salama.”

MUNGU IBARIKI TANZANIA Mwandishi wa makala haya ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kutetea Uhai (Pro- Life) Tanzania.

Anapatikana kwa 0784458341.

Columnist: habarileo.co.tz