Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Misukosuko iliiandama miradi ya TFF

Mweigwa Simba Celestine Mwesigwa

Thu, 10 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

ILIPOISHIA Katika toleo lililopita, aliyekuwa katibu mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa alikaririwa akisema kwenye suala la kodi kulikuwa na mifumo isiyoeleweka na TFF iliwahi kubambikiwa kodi na mamlaka, ofisi ikapigwa kufuli na watumishi kuzuiwa kuingia ofisini kuendelea na majukumu, SASA ENDELEA

“Kulikuwa na matukio mengi ya presha, vijana wetu hao kina Kibwana, Job, Israel, Kabwili, Nkomola na wengineo walipata ofa ya serikali Morocco kwenda kuweka kambi kujiandaa na Afcon, hivyo tunaenda kumuona Makamu wa Rais ambaye alitualika kwa chakula nyumbani kwake ili kuwaaga watoto ambao alipenda kuwaita wajukuu zake.

“Tunaambiwa wakala wa mamlaka ya kodi amewashusha wale watoto (kwenye basi) sababu TFF inadaiwa. Ikabidi tutafute namna nyingine ya usafiri kuwafikisha vijana Oysterbay. Wakati wa chakula alitoa hotuba nzuri sana, siku iliyofuata tulikutana na wenzetu wa kodi na suala lile lilifika mwisho,” anasema Mwesigwa

Anasema ilikuwa ni bandika bandua, kwani lilikuja suala la nyasi bandia za Uwanja wa Nyamagana (Mwanza), Kaitaba (Kagera) na zile za uwanja wa Simba wa Bunju. “Ililazimika kupatikana fedha ya nje ya mpira ili kuzikomboa, za Nyamagana na Kaitaba, Fifa imetoa nyasi kusaidia na iliwahi kufanya hivyo Gombani (Pemba) na Uhuru (Dar es Salaam) na viwanja hivyo ndivyo viliwahamasisha kuendelea kusaidia, lakini tukaambiwa tuzilipie kodi.

“Nakumbuka Halmashauri ya Jiji la Mwanza ilifikia hatua ya kuchangia ili kuzitoa nyasi hizo na Bukoba pia wadau wao walilazimika kufanya. Nilimuendea Mwigulu (Nchemba) akiwa ni Naibu Waziri lakini ilishindikana, tumemaliza hilo, hatujakaa sawa, klabu ya Simba ikanunua nyasi.

“Ikawa inahaha kupata msamaha wa kodi lakini ilishindikana, lakini tunasahau uwanja ukijengwa Bunju sio wa mtoto wa kiongozi wa Simba, bali utawasaidia Watanzania.

“Tulipambana, mfano Fifa ingesikia ile miradi haikukamilika ingekuwa ndiyo kwaheri, sidhani kama Tanzania tungepata tena msaada kama huo. Kipindi kile nilikuwa mjumbe wa kundi maalumu la miundombinu na miradi ya kuingiza kipato ya Fifa nikiwakilisha nchi za Afrika zinazozungumza Kiingereza. “Angalau nilipata nafasi ya kuwasihii watuvumilie. Kuna kitu hatukukiweka sawa, hatujawasiliana na mamlaka wakatuelewa, lakini halikuwa jambo zuri, lakini mwisho wa siku baada ya viwanja vile kukamilika imefungua njia ya miradi mingine,” anasema.

SAKATA LA KINA MAXIMO

Katika vitu ambavyo Mwesigwa anasema walihangaika navyo ni la mikataba ya makocha wa timu ya taifa (Taifa Stars) waliokuwa wakilipwa na Serikali wakati wa utawala wa awamu ya nne.

Wakati ule ndipo Marcio Maximo na wenzake kutoka Brazil walikuja nchini kuiona Stars, sanjari na makocha wa ngumi, riadha na judo kutoka Cuba na yule wa Netiboli, Semone Macknis kutoka Australia, ambao wote baadae waliondoka nchini, ingawa Stars ilipata makocha wapya Kim Poulsen na Jan Poulsen kwa nyakati tofauti.

“Serikali ilikuwa ikiwalipa kina Maximo, wakaja kina Kim na Jan kwa nyakati tofauti nao walikuwa wakilipwa na Serikali, lakini katikati ya mkataba wakajitoa kuwalipa.

“Wale makocha walikuwa wakilipwa na Serikali, lakini mikataba ni baina yao na TFF, mishahara yao ilikuwa mikubwa, zaidi ya Dola 10,000 kwa mwezi, hiyo si fedha ndogo, tukaanza kuwapunguza wale wa timu ya vijana bado mishahara yao ilikuwa mikubwa lakini tukalazimika kulibeba.

“La makocha halijaisha, timu ya taifa ya Brazil iliyokuja nchini, ilikuwa kwa hisani ya Serikali na wadhamini wengine lakini fedha ambayo Serikali ilipaswa kulipa likahamia kuwa deni la TFF na mamlaka hazikuweza kutuelewa kwenye hilo, lakini asilimia 100 siwezi kusema ilikuwa vikwazo tu, kuna mengine ya maendeleo yalifanyika,” anasema.

TIMU ZA VIJANA

Anasema ulikuwa mtizamo wa uongozi kwamba huwezi kujenga mpira bila kuwa na timu za vijana, akieleza kabla ya kuwa katibu mkuu wa TFF, Kamati ya Utendaji ilifanya maboresho ya Taifa Stars na alipoajiriwa aliikuta timu kambini. “Waligundua huwezi kujenga mpira kwa kuanzia juu, hivyo lazima tupate vipaji nchi nzima, tulitengeneza mahusiano na wizara ya michezo na Tamisemi ambako Kassim Majaliwa alikuwa ni naibu waziri huko na alikuwa ni mdau wa mpira tulikubaliana kuanza na Umitashumta moja.

“Waliofanya vizuri walipata ofa za kimasomo tukishirikiana na wenzetu wa Alliance, tulitaka huo ndio uwe utamaduni wa soka letu ingawa TFF haiwezi kutengeneza vijana ila inaweza kutengeneza sera nzuri ya vijana na klabu zikaishi kwenye utamaduni huo na zingefaidika sana.”

Mwesigwa anasema walikuwa na lengo la kuwa na kituo cha maendeleo ambacho walianza na Tanga ingawa sasa imeongezeka na Kigamboni pia, jambo ambalo ni hatua kwani hakuna mtu anaweza kujenga na kufanikiwa bila kupitia kwa vijana.

Columnist: Mwanaspoti