Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Miradi ya PPP, manufaa  na faida kwa taifa

6b1e5748c6c5aa7c6ba9ffd7e88de74d Miradi ya PPP, manufaa  na faida kwa taifa

Tue, 22 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

DHANA ya Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP), kama tulivyoona katika makala ya wiki iliyopita, chimbuko lake ni maandalizi hafifu ya miradi, hali iliyosababisha kuwa na miradi isiyokuwa na manufaa na iliyoleta hasara kubwa kwa taifa.

Kwa mujibu wa Kamishna wa PPP, Dk John Mboya, Ubia kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma hautahusisha mambo ya ubinafsishaji wa mashirika ya umma au huduma ya umma inayohusika; ubia wa kampuni iliyoazishwa na serikali na mwekezaji kwa pamoja kufanya biashara (Joint Venture), ambapo pande zote mbili zinawajibika kuendesha mradi, na kugawana faida na hasara.

Pia hitaji la mbia kubeba vihatarishi hasi kwa kiwango kikubwa halipo; kugeuza huduma ya umma kuwa ya kibiashara; na taasisi ya serikali kukopa wala kuingia katika ahadi za kulipa madeni kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

Dk Mboya anabainisha kuwa wahusika wakuu ni Taasisi ya Serikali na Kampuni iliyoundwa na Mbia (SPV), na kwamba taasisi ya serikali inaeleza na kufafanua kinaganaga inataka huduma ya aina gani, kwa ubora gani, kwa viwango gani, itolewe kwa wananchi gani, na kwa wakati gani.

“Kampuni Binafsi (SPV) inafafanua jinsi itakavyotoa huduma hiyo yaani ubunifu, uwezo wake kifedha, kimenejimenti, kitaalamu, teknolojia, n.k. Lengo kuu la Mkataba ni kutoa huduma ya umma kwa gharama nafuu,” anaeleza Dk Mboya.

Akifafanua kuhusu SPV, anaeleza kuwa ni kampuni inayoanzishwa na Mjasiriamali Mkuu kwa ajili ya kuingia mkataba na taasisi ya serikali wa kujenga na/au kuendesha au kutoa huduma ya umma husika.

Anabainisha kuwa SPV inawajibika kutimiza kikamilifu matakwa ya mkataba; inawajibika kuwa na rasilimali fedha, raslimali watu, teknolojia, na nyenzo zote zinazohitajika kwa kipindi chote cha mkataba; inapokea malipo kutoka taasisi ya serikali, watumiaji wa huduma, au kutoka kwa wote wawili kwa pamoja baada ya kutoa huduma husika; na itakabidhi mali zote za mradi baada ya muda wa mkataba kukamilika.

Zipo sifa zinaongoza miradi ya PPP ambazo kwa mujibu wa Kamishna wa PPP ni mradi uendane na vipaumbele vya taifa; mbia kutekeleza jukumu lililopaswa kutekelezwa na mamlaka ya serikali kwa muda maalumu; mbia kwa kiasi kikubwa anabeba vihatarishi vikiwemo vya fedha, ufundi na kiutendaji vinavyoambatana na utekelezaji wa mradi kwa niaba ya mamlaka ya Serikali au kwa kutumia mali za serikali.

Nyingine ni uwezo wa serikali na watumiaji huduma kumudu gharama za mradi na gharama za huduma katika kipindi chote cha uendeshaji; na mradi kuwa na thamani ya fedha ikilinganishwa na utekelezaji wa mradi kwa ununuzi wa kawaida unaotumia bajeti ya serikali.

Akizungumzia mfumo wa malipo katika PPP Dk Mboya anasema upo wa aina mbili; Mfumo wa Malipo na Ushiriki wa Serikali na Mfumo wa Malipo kwa Mbia.

Katika mfumo wa malipo wa mbia, watumiaji wa huduma za mradi wanamlipa mbia; mfano barabara ya kulipia; serikali inatenga fedha kumlipa mbia kwa miradi ya huduma za kijamii kama vile hospitali, shule na magereza.

Katika Mfumo wa Ushiriki wa Serikali, baadhi ya miradi ya PPP inaweza kuhitaji msaada wa serikali. Serikali inaweza kutoa ruzuku, uwekezaji wa hisa na ushiriki wowote utakaochambuliwa kwenye andiko la mradi.

Kamishna wa PPP anaeleza kuwa kuna aina mbili za miradi ya PPP, akiitaja kuwa moja ni mapendekezo ya miradi kutoka serikalini inayoandaliwa na Mamlaka za Serikali na ya pili ni wawekezaji wa sekta binafsi wanaruhusiwa kuwasilisha mapendekezo ya miradi kwa utaratibu wa miradi inayoandaliwa na sekta binafsi.

“Kanuni za PPP za mwaka 2020 zimeainisha kwa kina taratibu za kuzingatiwa kwa aina zote za miradi. Miradi midogo (chini ya Dola milioni 20) na mikubwa zaidi ya dola milioni 20. Maafisa Masuuli wa Wizara wamekasimishwa mamlaka ya kuidhinisha maandiko ya miradi midogo,” anaeleza Dk Mboya.

Katika kupata miradi hiyo, hupitia hatua za maandalizi zikiwamo uandaaji wa Andiko Dhana la mradi; kuandaa Upembuzi Yakinifu wa Awali; Upembuzi Yakinifu; Manunuzi ya mbia kutoka sekta binafsi inayohusisha utangazaji wa mradi hadi kuandaa na kuingia mkataba wa PPP; Utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini; na kurejesha mradi serikalini.

Akielezea mpango wa kuzingatia PPP, Dk Mboya anafafanua kuwa Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani kote inakabiliwa na uhaba wa rasilimali fedha kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Mapato ya kodi hayatoshelezi kugharimia miradi ya maendeleo… Serikali imepanga PPP ichangie kugharamia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambao umeweka kipaumbele kwa vyanzo bunifu ikiwemo PPP,” anasema.

Anasema kwamba utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/22-2025/26 unahitaji mchango wa sekta binafsi ikiwemo PPP kufikia Shilingi trilioni 40.611.

“Miradi ya PPP imeainishwa kufikia azma hiyo, na serikali inaandaa mpango madhubuti wa kutumia vyanzo mbadala kugharimia Bajeti ya Serikali,” anabainisha.

Kutokana na msingi huo, Dk Mboya anasema serikali imeainisha miradi ya PPP itakayotekelezwa ili kuchangia kikamilifu kugharimia Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa Mwaka 2021/22 – 2025/2026 ambao umeweka kipaumbele kutumia vyanzo bunifu ikiwemo PPP.

“Hadi mwezi Mei, 2021 jumla ya miradi 41 ipo katika hatua mbalimbali za maandalizi. Thamani ya miradi katika hatua zote inakadiriwa kuwa Shilingi za Tanzania 3,042,234 milioni sawa na trilioni 3.042. Miradi inaandaliwa katika sekta za mawasiliano, ujenzi, afya, elimu, biashara na maji,” anabainisha.

Akiwasilisha Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Mwaka 2021/22 bungeni Juni 10, mwaka huu, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, alizitaja shughuli zitakazotekelezwa kupitia PPP.

Alisema ni ununuzi wa mbia wa miradi ya ujenzi wa viwanda vya dawa muhimu na vifaa tiba itakayotekelezwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) katika mikoa ya Pwani, Mwanza na Mbeya; kukamilisha ununuzi wa mtoa huduma wa kudumu wa mradi wa uendeshaji wa Huduma ya Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka jijini Dar es Salaam Awamu ya Kwanza; na ununuzi wa mbia wa miradi ya ujenzi wa Hoteli ya Nyota Nne na Kitu Changamani cha Biashara katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).

Nyingine ni kukamilisha upembuzi yakinifu na kuingia katika hatua ya ununuzi wa mbia wa Mradi wa Kusambaza Gesi Asilia katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara; kukamilisha upembuzi yakinifu na kuingia katika hatua ya ununuzi wa mbia wa ujenzi wa Reli ya Kisasa ya Tanga – Arusha - Musoma pamoja na matawi ya Engaruka na Minjingu; na kukamilisha upembuzi yakinifu na kuingia katika hatua ya ununuzi wa mbia wa mradi wa ujenzi wa reli ya Standard Gauge ya Mtwara – Mbamba Bay na matawi ya Mchuchuma na Liganga.

Pia kukamilisha upembuzi yakinifu na kuingia katika hatua ya ununuzi wa mbia wa Mradi wa Ujenzi wa Hosteli za Chuo cha Elimu ya Biashara katika Kampasi za Dodoma na Dar es Salaam; kukamilisha upembuzi yakinifu wa awali na kuingia katika hatua ya maandalizi ya upembuzi yakinifu wa mradi wa ujenzi wa hosteli ya wanafunzi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania, Kampasi ya Dar es Salaam na Mbeya; kukamilisha upembuzi yakinifu wa Mradi wa Kituo cha Tiba ya Ugonjwa wa Saratani chini ya Taasisi ya Tiba ya Ocean Road - (Mloganzila); na ununuzi wa mbia wa mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza simu za mkononi chini ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Wengi wanajiuliza kwa nini PPP? Dk Mboya anaeleza takriban manufaa na faida 14 za PPP ikiwamo kupunguza utegemezi wa Bajeti ya Serikali katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa kutumia mitaji kutoka sekta binafsi ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo; kuepuka mikataba ya ubia isiyokuwa na tija na

serikali kupata ubunifu, utaalamu na teknolojia kutoka kwa sekta binafsi;

Anazitaja nyingine kuwa ni vihatarishi vya mradi vikiwemo vya kiufundi, kifedha na kiutendaji kutekelezwa kwa namna iliyo bora; kuongeza ubora wa huduma na ufanisi - malipo kwa huduma yanalipwa kwa kuzingatia utendaji; utaratibu wa PPP huwezesha miradi kukamilika kwa wakati na kuepusha miradi kuchelewa na kwa gharama kubwa.

Pia kuwezesha serikali kuwa na ukwasi wa fedha za kutekeleza majukumu mengine ya umma; kuimarisha na kukuza sekta ya fedha - sehemu kubwa ya mitaji ya kutekeleza miradi ya PPP inatarajiwa kutoka Sekta ya Fedha ambapo wabia wanakopa kwa asilimia 70 na asilimia 30 ya mtaji hutoka kwa wanahisa; na kuongeza ajira (utekelezaji wa Ilani ya CCM).

Kwa serikali, mapato ya kodi huongezeka na mianya hasi kupungua, wakati kwa mfanyakazi ajira ya uhakika, kwa mwekezaji faida; na kwa mtumiaji wa huduma, huduma ya umma kwa gharama nafuu na huduma kupanuka.

Lakini kwa wananchi wazawa wanashiriki kwa njia mbalimbali zikiwamo umiliki wa hisa; ajira – ngazi ya uongozi na ngazi ya wafanyakazi wa kawaida; mikataba ya ujenzi – hususani kandarasi shirikishi; mikataba ya utaalamu– uhasibu, sheria, injinia, n.k; na biashara shirikishi hususani wafanyabiashara wadogo na wa kati.

“Miradi ya ubia ni mkombozi katika kuboresha Bajeti ya Serikali na kuharakisha maendeleo ili kufikia uchumi wa kati wa juu na hii itafikiwa endapo tutatumia kikamilifu Sheria na Kanuni za PPP.

“Kupita njia ya mkato na za haraka haraka bila kuandaa miradi vizuri kutaleta hasara kwa taifa, tutarudia makosa ya huko nyuma kabla Sheria ya PPP na hii haikubaliki duniani kote kwa nchi zilizofanya vizuri eneo hili,” anaeleza Kamishna wa PPP wakati akihitimisha mada yake kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini.

Columnist: www.habarileo.co.tz