Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Milima, mabonde, tamu Simba kuusaka ubingwa

MAGUSIMBA Milima, mabonde, tamu Simba kuusaka ubingwa

Mon, 6 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

HATIMAYE Simba imetimiza ndoto yake ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya tatu mfululizo, kama ambavyo baadhi ya viongozi wake walikuwa wakijinasibu kuanzia mwanzo wa msimu huu wa 2019/20.

Kazi hiyo ilikamilika rasmi Juni 28, mwaka huu ilipotoka sare ya bila kufungana na Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na kufikisha jumla ya pointi 79 ambazo hakuna timu nyingine yoyote ambayo inaweza kufikisha.

Simba ilitwaa ubingwa msimu wa 2017/18 na 2018/19 na ilikuwa ikihitaji tena msimu huu taji ili kulichukua kombe hilo moja kwa moja.

Haikuwa kazi rahisi msimu huu, kwani pamoja na Ligi Kuu msimu wa 2019/20 kuwa ngumu, lakini ilikabiliwa na changamoto ya mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19, unaosababisha na virusi vya corona ambao nusura uzime ndoto zao.

Karibu dunia nzima ilisimamisha michezo, huku baadhi ya nchi zikifuta kabisa ligi, hivyo kutokuwa na mabingwa msimu huu, badala yake kuteua wawakilishi kwenye mechi za kimataifa.

Hata hivyo ligi ilirejea na Simba kutimiza ndoto zake. Ndani ya uwanja pia hakukuwa na lelemama, kwani ilibidi ipigane na kutoa machozi, jasho na damu, ikipitia njia nzuri na ngumu, tambarare, milima na mabonde na kupata ilichokitaka.

Kwenye makala haya tunaangalia safari nzima ya Simba kuelekea kwenye ubingwa ilivyoanza hadi ilipoishia na jinsi ilivyokuwa ikikusanya pointi zake mwezi hadi mwezi.

AGOSTI POINTI TATU

Simba ilianza kampeni yake ya kutwaa ubingwa msimu huu kwa kuvuna pointi tatu katika mechi yake moja iliyochezwa Agosti 29, mwaka jana.

Mechi hiyo ilikuwa ni dhidi ya Maafande wa JKT Tanzania na ilimalizika ikipata ushindi wa mabao 3-1, ikichezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam. Ilikuwa ndiyo mechi pekee iliyochezwa mwezi huo.

SEPTEMBA POINTI TISA

Mwezi uliofuata, Simba ilicheza mechi tatu na ilishinda zote, ikikusanya jumla ya pointi tisa.

Ilianza kwa kuinyuka Mtibwa Sugar jijini Septemba 13, mwaka jana, ikiwa mjini Bukoba iliisasambua Kagera Sugar mabao 3-0 Septemba 26, na siku tatu baadaye, Septemba 29, iliiadhibu Biashara United ya Mara mabao 2-0.

OKTOBA POINTI SITA

Mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara walicheza mechi tatu Oktoba, lakini safari hii ikikusanya pointi sita tu, baada ya kushinda mbili na kupoteza mechi moja.

Ilikuwa ni baada ya kuichapa Azam FC bao 1-0, Oktoba 23, mwaka jana na ikashinda goli 1-0, Oktoba 27, mwaka jana dhidi ya Singida United jijini Arusha ambako timu hiyo ilihamia kwa muda, kabla ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Mwadui FC, Oktoba 30, mwaka jana, mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga.

NOVEMBA POINTI SABA

Ni mwezi ambao Simba ilivuna pointi saba baada ya kushinda mechi mbili na sare moja.

Zilipatikana kwa kuichapa Mbeya City mabao 4-0 Novemba 2, mwaka jana, ikalazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya Tanzania Prisons Novemba 7, mwaka jana kabla ya kuiangamiza Ruvu Shooting mabao 3-0 Novemba 23, mechi zote zikichezwa.

DESEMBA POINTI TISA

Ilikuwa ni sikukuu ya Krismasi, Simba ilipotoa zawadi kwa mashabiki wake kwa kuichapa Lipuli mabao 4-0 hapa jijini na kama vile haikutosha, Desemba 28, mwaka jana ikaifunga KMC mabao 2-0, huku Desemba 31, mwaka jana ikishinda mabao 2-0 dhidi ya Ndanda FC, mechi zote zikichezwa Dar es Salaam.

JANUARI POINTI 10

Shughuli ilianzia mwaka 2020, mwezi wa kwanza au Januari. Ni mwezi ambao ilikusanya pointi 10 na kusafisha kabisa njia ya kuutwa ubingwa.

Ilikuwa ni Januari 4, mwaka huu ilipoanza kwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Yanga, lakini ikaenda Mwanza na kuichapa Mbao FC mabao 2-1, Januari 16, siku tatu baadaye, Januari 19, iliiadhibi Alliance FC mabao 4-1, na Januari 29, ilitoa kipigo cha mabao 3-2 dhidi ya Namungo FC.

FEBRUARI POINTI 18

Kwa kawaida Februari ni mwezi mfupi, lakini kwa Simba ndiyo mwezi iliyokusanya pointi nyingi zaidi kuliko miezi mingine msimu huu. Ilikusanya jumla ya pointi 18, ikicheza mechi saba.

Ilichapa Coastal Union mabao 2-0 Februari Mosi, kabla ya kuidungua Polisi Tanzania mabao 2-1 Februari 4, lakini ilipoteza mechi kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania Februari 7, mwaka huu.

Baada ya hapo, Februari 11 iliifunga Mtibwa Sugar mabao 3-0, huku iliichapa Lipuli bao 1-0 mjini Iringa Februari 15, mwaka huu na baadaye Februari 18 iliichapa Kagera Sugar bao 1-0 ikiwa mwenyeji na ilishinda mabao 2-0 dhidi ya Biashara Februari 22, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa.

MACHI POINTI TISA

Simba ilifanikiwa kukusanya pointi tisa katika kipindi cha Machi baada ya kushuka dimbani mara nne.

Machi Mosi, mwaka huu iliifunga KMC mabao 2-0, halafu Machi 4, mwaka huu ikaiadhibu Azam FC mabao 3-2, kabla ya kufungwa na Yanga bao 1-0 Machi 8, mwaka huu, ambapo Bernard Morrison alifunga goli hilo pekee. Ilijipoza kwa kuisasambua Singida United mabao 8-0 Machi 11, mwaka huu.

JUNI POINTI NANE

Baada corona, Ligi Kuu iliruhusiwa tena mwezi Juni, na Simba iliingia na moto na kukusanya jumla ya pointi nane zilizoweza kuipatia ubingwa wa Tanzania Bara kwa msimu wa 2019/20.

Ilianza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Ruvu Shooting Juni 14, mwaka huu na Juni 20 iliichapa Mwadui mabao 3-0, ikashinda mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City Juni 24 na Juni 28 ikapata sare ya bila kufungana dhidi ya Prisons.

Columnist: www.tanzaniaweb.live