Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mila na Desturi zinazofaa zirejeshwe katika malezi

459ceb43d7356e6c9d3193997c77b54e Mila na Desturi zinazofaa zirejeshwe katika malezi

Sun, 18 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MILA na desturi ni muhimu katika mustakabali wa malezi ya watoto katika jamii, licha ya kuwa na mila nyingine ambazo zimekuwa mbaya katika kumdidimiza mwanamke au mtoto, na hivyo kupigwa vita kila kukicha.

Kuhakikisha malezi bora ya watoto hususan wale wa kike, katika umri fulani zamani kulikuwa na desturi nzuri za kumfundisha mtoto wa kike anapopevuka na kuwa mkubwa au akikaribia kuolewa.

Katika nyakati hizo, akinamama na shangazi walikuwa wakijifungia na mtoto wa kike na kumfundisha masuala mbalimbali ya kufanya ili kuheshimika katika jamii, kuepuka kuanza mahusiano mapema na mengineyo.

Pia kwa wanaokaribia kuolewa walifundishwa kukaa na waume katika ndoa, kuheshimiana, kuvumiliana na masuala mengine ya mila na desturi pamoja na heshima kwa wakubwa.

Lakini katika siku za karibuni mambo yamekuwa tofauti kwa watoto wa kike kupata mafunzo katika mitandao ya kijamii, hivyo kusababisha watoto wa kike kuwa tofauti na nyakati zile.

Katika mafunzo ya mitandaoni kwa kiasi kikubwa wamepindisha masuala ya usawa wa kijinsia na kuwajengea watoto wa kike na wanawake kiburi badala ya kuwaeleza msingi wake wa usawa wa kijinsia kuwa ni kupinga vitendo vya unyanyasaji.

Lakini pia, wasichana wanapoolewa wamekuwa wakishindwa kutofautisha marafiki na matumizi ya mitandao, hivyo kusababisha ndoa kuvunjika mapema huku wakiacha watoto wakiteseka kwa malezi ya upande mmoja.

Katika kuona hilo, si jambo la ajabu kumkuta mwanamke aliyeolewa akishinda baa au katika vijiwe akipiga soga huku majukumu ya malezi akimwachia dada wa kazi bila kujali familia yake imeishije.

Katika jambo la kushangaza unaweza kumkuta mama wa familia hajui hata mtoto ameendaje shule, anaendeleaje kwani hajawahi kuwasiliana na walimu pamoja na masuala mengine katika malezi ya jamii.

Hivyo ili kurejesha heshima ya mwanamke katika ndoa pamoja na watoto wa kike ni vema mila za zamani katika kutoa mafunzo kwa watoto wa kike zirejee katika familia na kamwe akinamama tusikubali kuacha mitandao ya kijamii kufundisha watoto.

Pia na pale watoto wa kike wanapokaribia kuolewa kuwe na mafunzo makini kwa akinamama na shangazi na siyo kuwaachia watoa mada ambao wamekuwa wakiangalia pesa zaidi badala ya kutoa mafunzo huku wakiachana na sherehe za kumpatia vyombo pekee.

Ni dhahiri kuwa msichana akiingia katika ndoa na kuwa mama bora ndiyo chanzo cha familia bora na baadaye malezi bora yatakayosaidia kupata watoto wenye heshima kwa mustakabali wa vizazi vijavyo.

Ni kweli kuwa baadhi ya watu wanaeleza kuwa watoto wa siku hizi hawaelewi, lakini kupitia malezi tangu mtoto akiwa tumboni, anapozaliwa mpaka anapofikia umri wa kujitegemea ili kuwa na kizazi chenye maadili.

Ili kufikia lengo hilo ni vema kuwe na mjadala wa pamoja kuangalia jinsi ya kukabiliana na tatizo la malezi hususan nyakati hizi za sayansi na teknolojia kwa kuhakikisha kila mila na desturi za zamani haziachi zikapotea.

Mbali na mila na desturi, ni vema kwa watoto kuwajengea maadili mema ya kuwa na hofu ya Mungu ili kuwasaidia kukua katika maadili mema kwani hakika mtoto akiwa mcha Mungu ataepuka mambo mengi ya ujana hivyo kuokoa vizazi vijavyo.

Kwa hakika teknolojia zilizopo imekuwa rahisi kwa watoto na vijana kujifunza mambo mengi hivyo bila jamii kuingilia kati kuna hatari ya kuwa na vizazi visivyo na maadili katika miaka ijayo, hivyo kuwa hatari kwa familia, jamii na taifa

Columnist: habarileo.co.tz